Habari za Punde

WAWAKILISHI WATAKA EWURA ISHITAKIWE

Na Mwantanga Ame
UAMUZI wa Shirika la kudhibiti Nishati na Maji (EWURA), juu ya kuchukua jukumu la kuiuzia Zanzibar huduma ya umeme badala ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umewachafua Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuiomba serikali kulishitaki shirika hilo.
Wawakilishi hao walitoa kauli hiyo karibuni wakichangia hotuba ya Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui, aliyowasilisha jana asubuhi kwa wajumbe wa baraza hilo Zanzibar.
Hapo awali Waziri huyo akiwasilisha bajeti hiyo katika maelezo yake alisema katika ukaguzi walioufanya katika baadhi ya viwanda wamebaini vimekuwa vinakabiliwa na matatizo mengi likiwemo suala la huduma ya umeme gharama zake kuwa ni kubwa.
Mwakilishi wa Wete Asaa Othman Hamad, alisema hali hiyo, serikali inapaswa kutolivumilia shirika hilo na ipo haja ya Waziri wa Nishati Zanzibar kuifungulia mashtaka taasisi hiyo.
Alisema Zanzibar hapo awali wakati inataka kutumia huduma za Shirika hilo ilifanya makubaliano na shirika la TANESCO na sio EWURA ambapo hivi sasa wamekuwa wakitakiwa kununua huduma hiyo huko.
Alisema huo ni ukiukwaji mkubwa wa mkataba wa makubaliano juu ya ununuzi wa huduma hiyo ya umeme kwani hawaoni haja ya kununuliwa katika duka la rejareja wakati makubaliano ni katika duka la jumla.
Alisema inawezekana ikawa shirika hilo linafanya kwa makusudi ili kuwakatisha tamaa watumiaji wa huduma hiyo ya umeme, jambo ambalo hivi sasa watu wengi wanashindwa kuwa na huduma hiyo majumbani na baadhi ya sehemu za uzalishaji kulikosababishwa na gaharama kuwa ni kubwa.
Alisema Shirika hilo la EWURA tangu kupewa Mamlaka ya kuuzia umeme Zanzibar imekuwa ikipandishia viwango vikubwa ikilinganishwa na mikoa mingine ya Tanzania ambayo hununua kwa bei ya chini huku Zanzibar ikitozwa kiasi kikubwa.
Mwakilishi huyo aliyekuwa akitoa maoni yake hayo kwa hasira alisema ni vyema kwa Waziri wa wizara hiyo hivi sasa akajiandaa kulishitaki shirika hilo kwani sio lenye mamlaka ya kuiuzia umeme Zanzibar na imekuwa ikifanya biashara kinyume na sheria.
“Kwa nini Zanzibar iuziwe umeme na EWURA  inawezekana kuna watu hawataki kununua umeme Zanzibar kwani gharama kuwa ni kubwa,  EWURA haikupaswa kuiuzia umeme Zanzibar maana wamefungua duka la rejareja hivi sasa tutanunua mpaka lini huu umeme rejareja si wanatuumiza kusudi hawa Waziri tunaomba ukawashtaki hawa” alisema Mwakilishi huyo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Rashid Seif, alisema inasikitisha kuona Shirika la EWURA, limejipa majukumu la kuiuzia umeme Zanzibar jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwani inaitoza Zanzibar gharama kubwa.
Alisema hatari iliyopo kama serikali itashindwa kuliingilia kati suala hilo linaweza kuuwa viwanda na kudhoofisha uwekezaji kwani wanaweza kukimbia baada ya kuona gharama ni kubwa.
Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba, alisema matatizo ya wafanyabiashara bado suala hilo linaonekana kufanywa kuwa ni nyimbo kwani serikali imeeleza limemalizika lakini bado Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inaendelea kuwatoza kodi mara mbili.
Alisema hiyo ni kero ambayo inahitaji serikali kuiangalia kwa umakini kwani hata Wajumbe wa Baraza hilo imeshawachosha na ni vyema kwa serikali ikafikiria kuifuta TRA isifanye kazi zake Zanzibar.
Mwakilishi huyo aliwataka Wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanawatetea vizuri wananchi na sio kufanya udanganyifu kwa kukubali nyimbo za kujiridhi juu ya maslahi yao, kwani wanasahau viapo wanavyokula na ndio maana wanapoanguka katika uchaguzi hubakia wakibeba masusu ya matenga ya biashara.
Aidha, alihoji ni kwa nini serikali imekitoa kiwanda cha kuku kilichopo Mtoni kugeuzwa kuwa ni ghala la kuhifadhia saruji badala ya kutumika kwa ufugaji wa kuku ambapo walimuomba Waziri huyo kumtaja aliyepewa kiwanda hicho na alieruhusiwa kujenga mbele ya kiwanda cha maziwa.
Aidha, Wawakilishi hao pia walieleza ipo haja kwa serikali kuangalia suala la utoaji wa leseni za biashara kutokana na hivi sasa kuonekana kuna maduka mengi hayana leseni na yapo kwa ajili ya kuwahudumia wafanyakazi wa Baraza la Manispaa binafsi.
Mwakilishi wa Chambani, Hassan alisema ipo haja ya  Wizara ya Biashara ikajiandaa vyema kuweka mazingira bora ya biashara hasa katika kukabiliana na tatizo la magendo ya karafuu kutokana na baadhi ya wanunuzi wa zao hilo kubuni mbinu mpya kwa wasafirishaji zao kwa kuwaongezea bei zaidi.
Mwakilishi wa Micheweni Subeit Khamis Faki akichangia bajeti hiyo alisema mazingira ya biashara bado yanahitaji kuangaliwa hasa katika ufufuaji wa viwanda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.