Habari za Punde

UZINDUZI WA MRADI 100% ZANZIBARI PAMOJA NA UTAMBULISHO WA TAASISI YA SWAHILI PERFORMING ARTS




Taasisi ya Swahili Performing Arts Center, kwa kushikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania inafuraha kuvitangazia vyombo vya Habari juu ya kufanyika kwa mradi wa sherehe za maridhiano na umoja wa kitaifa utakaofanyika kuanzia tarehe 4 Oktoba hadi 3 Disemba 2011, nchini
Zanzibar.

Mradi huo, ulipewa utambulisho wa 100% Zanzibari (tafsiri; Mzanzibari asilimia mia) utajumuisha burdani za sanaa za maonesho asili kama vile muzeka wa Taarab, Ngoma za Utamaduni na michezo ya Kuigiza. Shangwe hizo zimepangwa kufanyika kwa awamu katika mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba
kwa muda wa miezi mwili mfululizo.


Madhumuni ya mradi huo ni kusherehekea maadhimisho ya miaka miwili tangu kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa baina ya vyama vikuu viwili vya siasa hapa nchini, hali ambayo imezaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuipitia ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.

Ufunguzi rasmi wa mradi huo utafanyika tarehe 8 Octoba 2011 katika ukumbi wa Ngome Kongwe mjini Unguja ambapo magwiji wa Taarab asilia, Culture Music Club na Nadi Ikhwan Safaa, wanategemewa kufanya onesho la pamoja.

Mbali na vikundi hivyo, wasanii na vikundi vyengine vitakavyoshiriki katika mradi huo ni pamoja na Prof. Gogo na kikundi cha Maendeleo (Kangagani, Pemba), Ngoma ya Mpe Chungu (Makunduchi, Unguja), Juhudi Taarab (Chake-Chake, Pemba) na Mdahoma na kikundi cha Nyota ya Umoja (Nungwi, Unguja). Wengine watakuwa ni Msewe wa Kambini (MchangaMdogo, Pemba), wasanii wa Unguja na Pemba Taarab All-Stars, Mkota Ngoma (Mkoani,Pemba) pamoja na Mchezo wa Tinge (Tundauwa, Pemba).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sanaa wa Swahili Center, Mahsin Basalama,ushiriki wa vikundi vyote 11 utakuwa ni kwa kupitia njia ya kambi za mabadilishano baina ya vikundi viwili, kimoja kutoka Unguja na chengine kutoka Pemba, katika kila wiki ya mradi huo. Ratiba ya mradi huo imeonyesha kuwa kambi na maonesho yake yatafanyika katika miji na vijiji kadhaa katika mikoa yote nchi nzima ikiwemo Mji Mkongwe, Makunduchi,Nungwi, Michenzani-Kisonge, Mkoani, Kangagani na Gombani (Chake-Chake).

Hivyo, kilele cha sherehe hizo zimepangwa kufanyika kwa shangwe kubwa hapa ifikapo tarehe 3 Disemba 2011 nje ya Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.

Tarehe za maonyesho katika mikoa ni kama ifuatavyo: Mjini Magharibi (19 Novemba), Mkoani (15 Oktoba), Makunduchi (22 Oktoba), Kangagani (29 Oktoba) na Nungwi (4 Oktoba). Maonesho yote yatakuwa ni bure kwa wananchi wote.

Akizungumza na waandishi wa Habari, muasisi-mwenza na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center, Kheiri Abdalla Jumbe, aliwahakishia wananchi wa Zanzibar maonesho ya kiwango cha juu na yanayozingatia mila na tamaduni.

“Lengo la mradi wa 100% Zanzibari ni kuimarisha misingi ya umoja tulionao sasa kupitia sanaa za maonesho asilia zenye burudani na mafunzo kwa jamii yote”, alisema Jumbe.

Wakati huo huo, mwakilishi wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Bi. Veslemoy Salvesen, alisema kuwa ni faraja kubwa kwa nchi yake kudhamini mradi huo ikiwa ni sehemu yake ya kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiutamaduni nchini Zanzibar.

Bi. Salvesen alisema “ Tunafuraha yakufadhili mradi huu kwa vile tunaamini kuwa maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar yataleta maendeleo. Pia tunaona fakhari kushirikiana na taasisi ya Swahili Center katika mradi wao wa kwanza.”

Swahili Performing Arts Center (Kituo cha Sanaa za Maonesho cha Waswahili) ni taasisi ya iliyoanzishwa na wazalendo wataalumu kwa dhamira ya kuchangia katika maendeleo ya sanaa za maonesho asilia za Zanzibar pamoja na zile za ufukwe wa Waswahili kupitia uwezeshaji (wasanii), uzalishaji wa kazi za sanaa, maonesho na ushirikishaji jamii. Dira ya Swahili Center ni
kuurejeshea hadhi utambulisho wa utamaduni wa Kiswahili.

Taasisi hiyo imesajiliwa rasmi Juni 2011 na tayari imeshafungua ofisi katika jengo la Old Dispensary liliopo katika barabara ya Mizingani, Mji Mkongwe-Zanzibar.

Kwa taarufa na maelezo zaidi, tafadhali wasiliana nasi kupitia anuani
zifuatazo: -

Kheiri A.Y. Jumbe
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Email: kheiri.jumbe@swahili-center.org
Mobile: 077.3620202

Au

Mahsin Ally Salim Basalama
Mkurugenzi wa Sanaa
mahsinbasalama@swahili-center.org
Mobile: 077.8338164

The Swahili Performing Arts Center
Ground Floor, Old Dispensary Building
Mizingani Road, Stonetown
Zanzibar, United Rep. of Tanzania
Email: info@swahili-center.org
Homepage: www.swahili-center.org
Facebook: Swahili Performing Arts Center

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.