Habari za Punde

DK SHEIN AHIMIZA KUTUMIKA SHERIA WAFANYAKAZI WA VYOMBO VYA BAHARI

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amezindua boti mpya ya Kilimanjaro111 na kueleza haja kwa wafanyakazi wa vyombo vya baharini kutumia sheria na taratibu zilizowekwa na Mamlaka husika badala ya kutoa huduma hiyo kwa matakwa yao na kuwasumbua wasafiri.

Alieleza kuwa kufanya kazi katika vyombo hivyo vya bahari bila ya kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na Mamlaka husima inaharibu biashara na kuondoa imani kwa wasafiri kwani nia ya wamiliki wa vyombo hivyo ni kutoa huduma kwa wananchi na ni tofauti na watoa huduma wanavyofanya.


Dk. Shein aliaysema hayo leo katika uzinduzi wa boti mpya ya Kilimanjaro 111 inayomilikiwa na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Limited chini ya Mkurugenzi wake Mkuu Salim Said Baghressa.

Dk. Shein alieleza kuwa jitihada za pamoja zinahitajika katika suala zima la utoaji wa huduma katika usafiri wa vyombo vya baharini na kukemea baadhi ya mambo yanayofanywa na wahudumu hao ikiwa ni pamoja na kuuza tiketi kinyume na sheria.

Katika mazungumzo yake Dk. Shein aliipongeza Kampuni ya Coastal Fast Ferries Limited kwa kufanya kazi zake na kutoa huduma nzuri za usafiri na kuepuka hali hiyo kutokea katika vyombo vyake vya usafiri.

Dk. Shein alisema kuwa siku zote abiria wanatakiwa kupewa huduma bora ambazo zitawavutia katika safari zao.

Alisema kuwa ipo haja ya kuiga huduma zinazotolewa katika usafiri wa angani ikianzia viwanja vya ndege pamoja na huma ndani ya ndege.

Aidha, Dk. Shein aliitaka Wizara na taasisi husika kusimamia vizuri taratibu na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanaoingia banharini wanafuata taratibu na sio kila mtu anaingia katika eneo hilo na kusababisha usumbufu kwa wasafiri.

Dk. Shein alisisitiza kuwepo nidhamu ya bandarini na Kuitaka Wizara husika kubadilika huku akieleza haja ya kuvitumia vyombo vya habari kwa kuielimisha jamii juu ya shughuli na taratibu za bandari.

“Wasiohusika na shughuli za bandarini wasiingie, na wale wenye kazi maalum wapewe vibali vitakavyoonesha shughuli zao”,alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa lengo la serikali ni kubadilisha haiba ya mji wa Unguja ikiwa ni pamoja na bandari yake na kueleza kuwa tayari visiwa vyote vilivyokuwa karibu na Zanzibar vimebadilika.

Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa Bwana Said Salim Baghresa kwa kutimiza ahadi yake ya kuleta boti mpya kwa ajili ya usafiri hapa nchini, hatua ambayo pia, itachangia uiimarishaji wa sekta ya utalii.

Alisema kuwa tayari serikali imeaza juhudi za kuimarisha huduma za usafiri kwa ajili ya kuimarisha sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa sehemu ya kushukia abiria katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume sanjari na azma ya kuimarisha uwanja wa ndege wa Pemba kufanya kazi usiku na mchana na kupelekea ndege kubwa aina ya Boing kuruka na kutua.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa usafiri wa watu walio wengi hapa Zanzibar ni usafiri wa bahari hivyo serikali bado ina azma ya kununua meli yake ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi na sio kushindana kibiashara ambapo pia inaendelea kuwashajiisha wafanyabiashara kuwa na meli kubwa na ya mizigo ili kutoa huduma hiyo.

Alisema kuwa bado kuna tatizo la uhaba wa vyombo vya baharini hivyo meli ya abiria na mizigo kati ya Unguja na Pemba, Tanga, Dar-es Salama na sehemu nyengine katika ukanda wa Afrika Mashariki inahitajika na serikali imo katika mchakato huo.

Dk. Shein pia, aliitaka Wizara husika kushirikiana na Salim Baghressa katika kuhakikisha ujenzi wa terminal ya abiria katika bandari ya Malindi Zanzibar linafanyiwa kazi kama ilivyo azma ya mfanyabiashara huyo.

Nae Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Masoud Hamad Masoud alisisitiza azma ya serikali ya kununua meli mpya kama historia ya usafiri wa baharini kwa upande wa Zanzibar inavyojionesha.

Waziri huyo pia, alieleza mchakato unaoendelea wa kuanzisha Chuo cha Mabaharia hapa Zanzibar ambapo Kamati ya kuanzisha chuo hicho inaendelea na kazi vizuri ambapo Mkurugenzi Salim Baghressa nae ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo.

Mapema Bwana Salim Baghressa alieleza kuwa uzinduzi wa boti hiyo unaenda sambamba na kusherehekea pia, miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kueleza kuwa hatua hiyo yote imekuja kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu nchini chini ya viongozi wenye hekima na busara kama Dk. Shein.

Alieleza kuwa ujenzi wa boti hiyo umechukua zaidi ya miezi 10 katika Mji wa Hobart huko Australia na kueleza kuwa ametimiza ahadi aliyoahidi ya kuleta vyombo vipya vitakavyolingana na matakwa ya wananchi ambapo chombo hicho kinachukua abiria 540m na kutumia dakika 90 kati ya Unguja na Dar-es Salaam.

Baghressa alieleza kuwa kampuni yao ya Coastal Fast Ferries Limited aliyoanzishwa mwaka 2008 tayari imeshawekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 20, hiyo ni kutokana na meli zake mpya tano, ikiwemo Kilimanjaro 1, Zanzibar Explorer, Kilimanjaro 11, Sea Rocket Limousine na Kilimanjaro 111.

Aidha, Baghresa alitoa compyuta mbhili kwa ajili ya waongoza meli zao na ya pili kwa ajili ya Mamlaka ya Usafiri Baharini ambapo alisema vyombo vengine vitaruhusiwa kutumia mtandao huo kwa gharama zao kwani gharama za mwanzo tayari wameshatoa.

Pia, Baghresa alieleza kuwa imefika wakati wa Zanzibar kuwa na ‘Passenger terminal’ ambayo itakuwa ya mfano na kivutio kwa watu na wasafiri wanaoingia na kutoa visiwani na kueleza kuwa si kweli kama ameomba kujenga terminal kwa boti zake pekee na hayo ni maneno tu yanayovumisha mitaani.

1 comment:

  1. Ni habari njema, ila nilidhani serekali itatilia umuhimu zaidi suala la usafiri baina ya Pemba na Unguja, kwani hicho ndicho kilio chetu cha mda mrefu. tuna vyombo vya kutosha baina ya Dar na Znz. Serikali inashindwa kuingia ubia na Bakhresa ikawapatia wananchi wake usafiri wa uhakika? to me, this is all about business, no goodwill.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.