Na Madina Issa
KATIKA kufikia azma ya kuwa Chuo kikuu chenye hadhi ya ubora katika kufundisha lugha ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kimeazimia kuungana na vyuo vikuu na taasisi mbali mbali ili
kufikia lengo hilo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) Prof.Idris Ahmada Rai aliyasema hayo wakati wa utiaji saini mkataba wa mashirikiano kati ya kituo cha Swahili Flagship cha Chuo Kikuu cha
Indiana cha Marekani na SUZA.
Prof.Rai alisema SUZA imedhamiria kuwa chuo kikuu cha ubora kwa kiswahili duniani hivyo mashirikiano hayo yataweza kuyafikia malengo hayo kwa vile wanafunzi na wakufunzi mbali mbali kutoka vyuo vikuu
tafauti duniani wataweza kufika SUZA kupata taaluma hiyo ya lugha ya kiswahili.
Rai alisema mkataba huo una madhumuni makuu ya kukuza ushirikiano baina ya chuo cha SUZA na Kituo cha swahili Flagship kwa kubadilishana uzoefu baina ya wakufunzi pamoja na wanafunzi wa vyuo hivyo.
Aidha alisema malengo mengine ni kubadilishana vifaa vya kusomeshea kama vile CD, DVD na vifaa vyengine mbali mbali.
Makamu mkuu huyo alisema chuo chake kitahakikisha kinafikia lengo la kuwa chuo kikuu bora kwa Kiswahili duniani kama alivyoagiza mkuu wa chuo hicho ambaye pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Hivyo aliwataka wanafunzi wanaotaka kujifunza lugha ya kiswahili nchini na nje ya nchi kujiunga na chuo cha SUZA kwani ni kituo bora kwa kufundisha lugha hiyo.
Nae Mkurugenzi wa kituo cha Swahili Flagship cha Chuo cha Indiana cha Marekani Dk. Alwiya Omar, alisema kituo chake kimeazimia kuleta wanafunzi katika chuo cha SUZA ili kujifunza lugha ya kiswahili kwa
kuelewa chuo hicho kina ubora wa kufundisha lugha hiyo.
Dk. Alwiya alisema katika makubaliano yao na SUZA watahakikisha wanakipatia chuo hicho vifaa mbali mbali vya kusomeshea kwa lengo la kuongeza ubora katika ufundishaji.
Aidha alisema mbali na vifaa hivyo watahakikisha kuwa wanashirikiana na Chuo kikuu cha SUZA katika kuandaa warsha mbali mbali zenye lengo la kuwaandaa wakufunzi kuwa na mbinu za kisasa za ufundishaji.
Akitoa shukrani baada ya kutiliana saini mkataba huo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Taaluma, Dk. Ahmada Khatib alisema chuo chake kitahakikisha kinayatumia ipasavyo mashirikiano
hayo kwa lengo la kuwapatia elimu bora wanafunzi wataofika kupata taaluma hiyo ya lugha ya kiswahili.
Dk. Ahmada alisema chuo chake kimo katika mikakati ya kufundisha kiswahili hata katika masomo mengine yanayofundishwa chuoni hapo.
Aidha alisema walimu wanaofundisha kiswahili chuoni hapo watumie mbinu za kisasa za ufundishaji ili waweze kwenda sambamba na mazingira ya sasa.
Hii ni taasisi ya pili kutiliana saini na chuo cha SUZA mkataba mashirikiano ambapo wiki iliyopita walitiliana saini na taasisi ya utafiti na sera za umma Zanzibar (ZIRPP).
No comments:
Post a Comment