Habari za Punde

DK SHEIN AWAASA WAISLAMU KULEA WATOTO WAKIZINGATIA MAADILI

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka waumini wa dini ya Kiislamu kulea watoto wao kwa kufuata maadili na taratibu za dini ya Kiislamu.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Bweleo, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi wakati alipokuwa akisalimiana na wananchi wa Bweleleo katika msikiti mkuu wa Ijumaa wa Bweleo mara baada ya kumaliza Ibada ya sala ya Ijumaa.


Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa iwapo watoto watapata maadili mazuri na kufutishwa taratibu na miendelndo ya Kislamu watoto watakuwa na malezi mazuri ambayo yatafuata misingi ya dini ya Kiislamu.

Alieleza kuwa umefika wakati kwa jamii ya Kiislamu kuwalea watoto wao katika misingi iliyoachwa na Mtume Muhammad (SAW) pamoja na misingi ya Qur-an takatifu ili watoto na vizazi vijavyo viwe bora zaidi.

Alhaj Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto na kuwataka wazee na jamii nzima kwa ujumla kuhakikisha kuwa suala la malezi bora kwa watoto lina nafasi kubwa katika maisha ya kila siku.

Nao waumini na dini ya Kislamu na wananchi Bweleo walimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuiletea maendeleo Zanzibar na kumuhakikishia kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha watoto wanakuwa na malezi bora.

Mapema Khatibu wa msikiti huo alisisitiza haja ya kuwalea watoto katika maadili mema na kutoa mifano kadhaa juu ya maelezi ya watoto kutoka katika Qur-an tukufu pamoja na Hadithi za Mtume Mohammad (SAW).

Wakati huo huo Dk. Shein alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Usalama Barabarani ya Oman Balozi Dk. Wahid Al-Kharus huko Ikulu mjini Zanzibar, ambapo katika mazungumzo hayo Dk. Shein alieleza kuwa anaamini kuwa ajali za barabarani zinaweza kupungua kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitatu ijayo kutokana na mashirikiano ya pamoja.

Alieleza kuwa uwezekano wa kufikia malengo kabla ya miaka 10 ijayo unawezekana na kusisitiza kuwa ajali haziathiri familia tu bali hata serikali nayo imekuwa ikiathirika kutokana na matukio kadhaa ya ajali za barabarani zinazotokea siku hadi siku.

Dk. Shein alieleza kuwa kuna Sheria maalum zimewekwa kwa ajili ya kudhibiti ajali za barabarani hivyo kuna kila sababu ya kufuatwa kikamilifu.

Akitoa mfano wa Malaria, Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wananchi katika kupiga vita Malaria hivyo uwezekano mkubwa upo wa kupiga vita ajali za barabarani na kuweza kufanikiwa katika maradhi hayo.

Sambamba na hayo Dk. Shein alitoa pongezi kwa kuanzishwa suala zima la Usalama Barabarani ambapo alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliowekwa katika kupiga vita ajali za barabarani.

Nae Dk. Al-Kharus alisifu maandalizi na maadhimisho ya miaka kumi ya Usala Barabarani na kutoa shukurani zake kutokana na kupokelewa matakwa ya wanafunzi na kusisitiza kuwa kuna haja ya kuishirikisha jamii katika suala zima la usalama wa barabarani.

Sambamba na hayo, alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kushiriki kikamilifu katika hafla hiyo ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maandamano maalum yalioandaliwa katika uzinduzi wa miaka kumi ya usalama barabarani ambao ulifanyika hivi karibuni katika hoteli ya Bwawani hivi karibuni na hatimae matembezi hayo yalianzia hotelini hapo hadi hospitali Kuu ya MnaziMmoja mjini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.