Habari za Punde

KIWANDA CHA KUKAUSHIA NGOZI CHAFUNGWA

Chadaiwa kuchafua chanzo cha maji

Na Asya Hassan

IDARA ya Mazingira imesitisha shughuli zote zinazofanywa na kiwanda cha kukaushia ngozi za ng’ombe kilichopo Kianga wilaya ya Magharibu Unguja.

Kiwanda hicho ambacho kipo kwa zaidi ya miaka 10, kimelazimika kufungiwa kutokana na kuendesha shughuli zake kinyume na sheria pamoja na kuharibu mazingira.


Mkurugenzi Idara ya Mazingira Sheha Mjaja Juma, alisema upo ulazima wa kufungiwa kiwanda hicho kutoka na kuendesha shughuli zake bila ya kuzingatia uchafuzi wa mazingira.

Alifahamisha kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikitiririsha maji ambayo huishia kwenye chemchem, ambayo ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa Kianga na maeneo jirani na kijiji hicho.

“Maji yanayotokana na shughuli za ukaushaji yanatiririka hadi kwenye chemchem ambayo ni chanzo cha maji kwa wananchi wa eneo hili”, alisema Mjaja.

Aidha alisema maji hayo yanayotoka katika kiwanda hicho ni machafu na yenye harufu mbaya ambapo yanaweza kuathiri afya za watu na wanyama wanaotegemea chanzo cha maji katika chemchem hiyo.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa maji hayo yanayotiririka katika chemchem, yamekuwa na chumvi nyingi ambayo hutumika kwa kazi za ukaushaji ngozi hizo hali inayofanya kuua miti pamoja na vipando vya
wakulima.

“Maji haya ni machafu yana chumvi ambapo imekuwa ikikausha vipando vya wakulima wanaolima katika bonde hili”,alisema Mjaja.

Mjaja alisema kuwa shughuli za ukaushaji wa ngozi katika kiwanda hicho kumekuwa kukitoa harufu mbaya ambayo inahatarisha afya kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa endapo mmiliki huyo atafuata sheria zilizowekwa na serikali juu ya kuhifadhi mazingira ataendelea na biashara yake na kuifanya kuwa kiwango cha juu zaidi
katika kumuingizia kipato.

Kwa upande wa mwenyekiwanda hicho Abdul-rahman Haji Mohammed, alisema kuwa yeye haoni sababu ya kufungiwa kiwanda chake kwani walishawahi kwenda maofisa kutoka Idara hiyo na kumtaka achimbe shimo kwa ajili ya kuhifadhi maji hayo machafu na tayari shimo hilo lipo katika hatua mzuri.

Alisema kuwa yeye anafanya hivyo kwa kujitafutia riziki hivyo kufungiwa kufanya shughuli hiyo kutamfanya aishi maisha ya dhiki kwani hiyo ndiyo kazi tegemeo katika kuiendesha familia yake.

Alifahamisha kuwa kiwanda chake kazi yake ni kukausha ngozi na kuhifadhi, hivyo kinahitaji kuwa katika sehemu ya uwazi ili ngozi hizo zipate hewa.

Hata hivyo alifahamisha kuwa yeye alipata kibali rasmini cha kuendesha biashara hiyo kutoka Mambo msige na kupata kibali cha kusafirisha ngozi hizo kupeleka nchi mbalimbali kama vile China, India na Pakistan
kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbali mbali.

Nae mwananchi alie katika mradi wa kuhifadhi maji wa Tasaf Chausiku Khamis, alisema kuwa wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa kuotesha miti ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi maji kutokana na
kuongezeka kiwango cha chumvi katika mashamba hayo.

Alisema kuwa wao hawana lengo la kumuhamisha au kumfungia biashara yake ila wanachotaka ni kuhifadhi mazingira ya kazi zake na kuwacha usumbufu unao wapata wananchi hao.

Hata hivyo aliitaka halmashauri inapotoa vibali kwa kuwapa watu kwa ajili ya ujenzi lazima wawape elimu juu ya kutunza mazingira na sio kutowa vibali hivyo na kuwasababishia wananchi usumbufu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.