Habari za Punde

KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA ZANZIBAR KITAKUWA CHA KISASA

Na Ramadhan Makame, Beijing

MSAIDIZI Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group International (BCEGI), Li Qiong amesema jengo la kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Zanzibar litakuwa la kisasa.

Mkurugenzi huyo alieleza hayo alipokuwa na mazungumzo na mawaziri na viongozi waandamizi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ofisi ya jengo hilo mjini Beijing nchini China.


Alisema kampuni yake inaelewa umuhimu wa kiwanja cha ndege kwa uchumi wa Zanzibar hasa katika mipango yake ya kuongeza idadi ya watalii wanaovitembelea visiwa hivyo.

"Tuna taarifa kuwa Zanzibar ni visiwa vizuri vilivyojipatia umaarufu kutokana na utalii, hivyo lazima tuhakikishe jengo la abiria la kiwanja cha ndege cha Zanzibar linakuwa na ubora wa hali ya juu", alisema Qiong.

Aidha alifahamisha kuwa ujenzi unaoendelea mbali ya kuwa wa kisasa lakini pia kampuni yake itahakikisha jengo hilo linamalizika kwa wakati.

Alisema kampuni yake inaringia uzoefu iliyonao na teknolojia iliyonayo katika shughuli mbali mbali za ujenzi ikiwemo nyumba za makaazi, hoteli na viwanja vya michezo.

Alifahamisha kuwa hivi sasa BCEGI imekuwa miongoni mwa kampuni bora za ujenzi sio nchini China pekee, kwani imekuwa na miradi mbali mbali ya ujenzi barani Afrika, Ulaya, Asia pamoja na nchi za Amerika.

Kwa upande wake mkuu wa msafara wa viongozi wa serikali ambao wapo China kwa ajili ya mafunzo ya uwekezaji vitega uchumi, Pandu Ameir Kificho alisema serikali itashirikiana na kampuni hiyo ili mradi huo
wa ujenzi umalizike kwa wakati.

Aidha alisema serikali itakuwa tayari na kuwa karibu wakati wowote na kutoa msaada wake endapo itahitajika ili mradi wa ujenzi utekelezeke kwa mafanikio.

Awali ujumbe huo ulitembezwa katika moja ya ujenzi wa nyumba za biashara katikati ya jiji la Beijing ambapo kandarasi ya ujenzi huo inafanywa na kampuni hiyo.

BCEGI mbali ya kujenga jengo la kupumzikia wageni katika kiwanja cha ndege cha Zanzibar kwa Afrika pia imepata kandarasi ya ujenzi nchini Zambia.

Aidha pia ilikuwa ikiendelea na miradi ya ujenzi nchini Libya, lakini haieleweki kama itaendelea hasa baada ya kupinduliwa na kuuawa kwa Kanali Muamar Gaddafi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.