Habari za Punde

MAALBINO WASIFANYWE CHAMBO CHA KUJIPATIA UTAJIRI

Na Kunze Mswanyama,Dar

WATANZANIA wametakiwa kuacha dhana potofu dhidi ya walemavu wa ngozi (albino), kwamba viuongo vya miili yao vinaleta utajiri iwapo vitapatikana akiwa hai au amefariki.

Mwandishi wa habari Mwandamizi wa shirika la Utangazaji la Uingereza Vicky Ntetema alieleza hayo jijini Dar es Salaam, ambapo alibainisha kuwa kupata utajiri kwa viungo vya almbino ni imani potofu.


Alisema dhana kuwa viungo vya mlemavu wa ngozi vikipatikana vinaweza kumpatia ujatajiri mtu ni mpotofu na ni mawazo ya kizamani yasiyoendana na enzi za karne hii.

Alisema utajiri unapatikana kwa mtu kujituma kwa kufanyakazi kwa bidii na sio kufanya ukatili wa kumtoa roho binaadamu mwenzio kwa kumfanyia vitendo vya kishirikiana kwa fikra kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwa tajiri.

Alifahamisha kuwa maalbino hawatofautiani na watu wengine wa kawaida ila walichokikosa katika ngozi yao ni ‘melaini’ ambayo ndiyo inayosababisha ngozi kwa nyeusi.

Katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es salaam,uliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Polisi,Mahakama,Viongozi mbalimbali wa Kidini na kada nyingine ikiwemo waandishi wa habari waandamizi.


Ntetema ambaye amekuwa akifanyakazi za utetezi wa haki za maalbino alisema wapo watu wanawahusisha maalbino kuwa ni sawa na majini na kwamba dhana hiyo nayo ni potofu kwani ni binaadamu wa kawaida.

Aidha alipingana vikali na wale wenye fikra kuwa unapofanya mapenzi na mlemavu wa ngozi unaweza kupoa UKIMWI, na kueleza kuwa kuendeleza upotofu huo ni kusambaza maradhi hayo.

Aliwasihi wananchi kutowabagua, kuwanyanyasa na kuwaogopa kwani u-alibno hauambukizwi bali hurithiwa kutokana na wazazi husika kuwa na jeni zenye ulumavu huo wa ngozi na kwamba ulemavu huo ni makosa ya mama au kwamba mama alifanya ngono na shetani wa kizungu au mzungu.

Aliwataka wote wenye watoto hao kutowaficha bali wawaweke hadharani ili waonwe na kusaidiwa lakini pia alitahadharisha kutowaweka juani kwa kuwa kutasaidia kuleta saratani ya ngozi na hakuwezi kuifanya ngozi hiyo kuwa nyeusi, bali wajikinge na jua kwa kuvaa kofia, nguo zenye mikono mirefu na suruali.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2009, askari wanne wa mkoani Shinyanga walishikiliwa kwa kosa la kuwasaidia wahalifu wa mauaji hayo ambao wengi ni waganga wa kienyeji kuficha ushahidi ili wasipatikane na hatia ya makosa hayo ya mauaji na kujeruhi ambapo baadhi ya albino wamenyofolewa mikono, miguu na sehemu zao za siri hivyo kubaki wakiteseka maisha yao yote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.