Habari za Punde

Gari JWTZ Yapinduka Yaua Mmoja, 24 Wajeruhiwa

Na Mwantanga Ame

MWANAJESHI mmoja wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amefariki dunia na wengine 24 wamenusurika vifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la Fuoni wilaya ya Magharibi Unguja.

Ajali hiyo imetokea jana saa 7:15 za mchana wakati gari aina ya IVECO lenye namba za usajili 5668 JW 08, lilokuwa likiendeshwa na askari Yahya Juma Hussein, akitokea Mjini, kuelekea kwenye kambi ya mafunzo
ya Wanajeshi.


Mwanajeshi aliyefariki katika ajali hiyo ametambulika kwa jina la Yassin Mohammed Yassin, alitokea Tanzania bara ambaye alifariki baada ya kuumia vibaya sehemu za kichwani.

Ajali hiyo, imetokea baada ya kudaiwa dereva Yahya, alikuwa akimkwepa mwendesha baiskeli jambo ambalo lilisababisha gari hilo kumshinda na kupinduka.

Wakati ajali hiyo ikitokea sehemu kubwa ya majeruhi waliumia kutokana na shehena ya mzigo iliyopakiwa vikiwemo vitanda, maturubali, mitaimbo na masusuru ikiwa ni vifaa walivyokuwa wakitaka kutumia kwa
kujengea mahema ya kambi hiyo.

Wengi wa majeruhi walioshuhudiwa na Zanzibar Leo, katika hospitali ya Rufaa Mnazimmoja, walionekana kuumia viungo vya miguu na sehemu za mabega na wamepatiwa matibabu yaliyoongozwa na Daktari wa Jeshi hilo Haroub, akishirikiana na baadhi ya manesi wa hospitali hiyo, huku waliovunjika viungo wakivishwa P.O.P.

Hali ya Hospitali ya Mnazi mmoja ilionekana kuwa na pirika nyingi za askari wa Jeshi hilo kushughulikia wagonjwa wao, baada ya baadhi ya vifaa kukosekana katika hospitali hiyo ikiwemo huduma ya X- RAY.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya majeruhi hao baada ya kupatiwa matibabu ya huduma ya kwanza waliondoshwa hospitalini hapo na kusafirishwa kupelekwa katika hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi
Tanzania ya Lugalo Mjini Dar es Salaam.

Wakati askari hao wakisafirishwa wakiwa chini ya viongozi wa Jeshi hilo na Jeshi la Polisi, eneo la barabara za Mji wa Zanzibar yalishuhudiwa magari kadhaa yakipiga vingora kwa ajili ya kuweka tahadhari ya kupishwa njia ili wagonjwa hao wawahi kusafirishwa.

Hadi saa 9.30, za mchana askari waliosafirishwa kutoka katika wodi ya viungo katika hospitali hiyo, walishuhudiwa askari 15 ambao walisafirishwa kwa boti zendazo kasi katika bandari ya Zanzibar.

Askari waliojeruhiwa ni pamoja na Blandina Barnabas, Bibeta Odo, Happy Shayo Silili, Hidaya Abdalla, Oliva John, Salum Manguri, Kashinde Wakula, Amana Abdi, Rashid Kibabu, Angrina Kapinga na Khamis Makame.

Wengine ni Tado Kwetupia, Haji Daud, Steven Joseph, Godfrey Bernadict, Oliva Ngoma, Salum Ali, Kaunda Sakoni, Juma Talib, Yusta Gabriel, Teresia, Fadhil Saleh na Josephat Tendeu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Unguja, alitafutwa kwa simu ili aelezee kadhia ya ajali hiyo lakini hakuweza kupatikana.

2 comments:

  1. Eeh Mungu mlaze mahala pema peponi kaka yangu Yassin

    ReplyDelete
  2. Mungu amlaze peponi ndugu yetu yasin

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.