Yavunja rekodi ya miaka 20 kwa kupokea watalii 175,067
Na Salum Vuai, Maelezo
IDADI ya watalii waliofika Zanzibar mwaka 2011, ilifikia 175,067, kiwango ambacho hakijawahi kurikodiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Akitoa taarifa za maendeleo ya sekta ya utalii kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Ali Khalil Mirza, alisema
kiasi hicho kimevuka lengo la watalii 160,000 ambao Zanzibar ilitarajia kupata mwaka huo.
Aidha alisema, idadi hiyo ni kubwa kulinganisha na ya mwaka 2010, ambapo watalii 132,836 walitembelea visiwa vya Zanzibar.
Akifafanua zaidi, Mirza alieleza kuwa, watalii hao ni kutokana na takwimu rasmi zilizopatikana katika uwanja wa ndege pamoja na bandari, lakini akaongeza kuwa asilimia 20 hadi 25 mbali na hao, ni watalii wa ndani ambao hufika kutoka Tanzania Bara wakati wa sikukuu mbalimbali zikiwemo Pasaka, Krismasi na mwaka mpya.
Alifahamisha kuwa, mafanikio hayo yamepatikana kutokana na jitihada za serikali kuimarisha miundombinu zikiwemo barabara, pamoja na kuweka mazingira mazuri katika maeneo yenye vivutio vya utalii nchini.
Pamoja na hayo, Mirza alisema harakati za kiutalii zimeongezeka hasa kutokana na kuwepo huduma nyingi za usafiri wa ndege za kukodi (charter flights), kati ya Zanzibar na mikoa ya Tanzania Bara ikiwemo
Arusha ambao ni miongoni mwa maeneo mashuhuri kwa utalii.
Pia alisema kuongezeka kwa vyombo vya kisasa vya usafiri wa baharini, nako kumechangia kuiletea Zanzibar ufanisi katika sekta hiyo.
Aidha alieleza kuwa, mwelekeo wa kamisheni yake kwa sasa, ni kuitangaza zaidi Zanzibar katika nchi nyengine ambazo si miongoni mwa masoko yake ya utalii.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Russia, India, Falme za Kiarabu, Japan pamoja na China, akisema kuingia kwa watalii wa nchi hizo, kutaongeza tija kwa Zanzibar ambayo soko lake kuu ni nchi za Italia,
Uingereza, Afrika Kusini na Ujerumani.
"Mafanikio hayo yamezidi pia kwa kutanuka wigo wa ukaazi kwa watalii wanaokuja nchini, ambapo zamani wengi walikuwa wakikaa kati ya siku tatu na nne, lakini sasa hufika siku sita hadi saba", alibainisha Mirza.
Hata hivyo, alipoulizwa kiasi cha fedha kilichopatikana kutokana na utalii na biashara nyengine zinazohusiana na sekta hiyo, alisema hilo ni jukumu la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kamisheni yake, imeonekana kuwa kwa mwaka sekta ya utalii inaiingizia Zanzbar si chini ya dola 140 bilioni.
Aidha, alisema sekta hiyo inachangia asilimia 27 ya pato lote la nchi, na kwamba kati ya miradi ya vitega uchumi yote iliyopo Zanzibar, asilimia 72 vinaambatana na utalii.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, ufanisi uliopatikana mwaka jana, ni faraja kubwa kwani umeufanya uchumi wa Zanzibar ukue, baada ya kuporomoka kwa biashara ya utalii mwaka 2008/09, kulikosabishwa na
mtikisiko wa uchumi ulioikumba dunia.
Katika kipindi hicho, Zanzibar ilipokea watalii 134,000 mwaka 2008, na 2009, idadi hiyo ilishuka na kufikia 132,000.
Mirza alifahamisha kuwa, miongoni mwa mikakati ya kamisheni yake kwa sasa, ni kukifanya kisiwa cha Pemba kuendesha utalii wa kimazingira (Eco-Tourism), kwa lengo la kulinda mandhari ya kisiwa hicho na kutoa ajira za kutosha kwa wananchi wa huko.
Haya tena, tusibweteke na taarifa hiyo! tukaze kamba na kuimarisha vivutio vyetu vya utalii ili kukuza uchumi na ajira kwa vijana wetu.
ReplyDeleteKama kuna jambo mbalo serikali inabidi kufanya ktka kukuza utalii basi ni kuendelea kuutunza na kuuendeleza mji mkongwe.
Sielewi serikali inahiofia nini kuwanyima vibali wamiliki wote wa majengo ya mji mkongwe wanaotaka kuongeza ghorofa?
Na kama inabidi kuwaruhusu basi waambiwe waongeze hizo ghorofa kwa kutumia mbao!
Serikali ikumbuke suala la umiliki wa mji mkongwe sasa sio tena la wazaliwa au wamiliki wa majengo bali ni la Wazenj wote pamoja na dunia(UNESCO)