Habari za Punde

Nabii Awachapa Makofi Waumini

Ni kwa kutoa sadaka ‘kiduchu’

Joseph Ngilisho, MANYARA

WAUMINI madhehebu ya huduma ya mti wa uzima ‘Ebenezer Gospel Church’ katika mji mdogo wa Mirerani wamemlaani mhubiri kutoka jijini Dar es Salaam, kwa kuwachapa makofi akighadhibishwa na udogo wa sadaka walizotoa.

Mbali ya kuwachapa makofi waumini, Mhubiri huyo aliyejipachika cheo cha nabii alizipiga mateke sadaka hizo na kusema kuwa Mungu hawezi kupokea sadaka kiduchu.

Waumini hao walisema Mhubiri huyo kutoka jijini, alialikwa na mhubiri wa mji wa Mirerani wa madhebu hayo Baraka Joshua, wakimshangaa na kumlaani kwa vitendo vyake hivyo ambavyo vimevuka mipaka ya kiimani.
Mhubiri Baraka Joshua alimualika nabii huyo kwa lengo la kutoa semina ya kuwajenga kiimani na kiroho waumini hao, lakini wakashangazwa na vitendo hivyo vya kuvunjwa membari na kupigwa mateke kwa sadaka zao.

Muhubiri huyo (jina lake limehifadhiwa), inadaiwa alipoozwa na Mchungaji wa kanisa hilo, Baraka kwa kupewa bure gari aina ya Mark II, Balloon kama sadaka.

Wakizungumza na waandishi wa habari, waumini hao walidai kuwa vitendo hivyo vilifanyika kwenye kanisa lao, huku waumini hao katika hali isiyo ya kawaida wakishangaa kuyaona maajabu hayo na kufanya baadhi ya waumini wasusie semina hiyo ya kiroho.

“Hii hatujawahi kuliona kabisa yaani huyo nabii alikuwa anatumia lugha kali huku akiwachapa waumini wenzetu akiona wametoa sadaka kidogo na kuwambia Mungu hawezi kupokea sadaka kidogo kama hiyo”, alisema.

Waumini hao walifahamisha kuwa kila waumini walipokuwa wakitoa fedha kidogo kama noti za shilingi 500, 1000 na 2000 alikasirika huku akihoji mbona hazioni noti za shilingi 5,000 na 10,000.

“Hata kwenye biblia tunaelezwa Yesu alikuwa anaangalia imani ya utoaji siyo wingi wa fedha za sadaka, sasa sisi tumeshangazwa na vitendo hivyo vya kupiga teke sadaka ya waumini kanisani na kuvunja mimbari”, alisema.

Walisema nabii huyo kwenye mahubiri yake alitamba kuwa yeye ana gari aina ya Mercedes Benz na alikuwa na suti 15 na alizigawa kama sadaka kwa watu tofauti na aliwahi kufunga siku nne kwa kula udongo akimtumikia Mungu.

Waliongeza kuwa muhubiri huyo alidai kuwa alikuwa ana fedha benki kiasi cha shilingi 14 milioni, lakini alizigawa zote kwa watu masikini naye akaishiwa fedha zote akabaki hana hata shilingi 100 lakini Mungu akampa fedha nyingine.

Hata hivyo, askofu wa Ebenezer Gospel Church lenye makao makuu Dar es Salaam, Hezron Kyogo alidai kuwa kwenye imani ya kanisa lao hawakubaliani na vitendo hivyo vya kuvunja madhabahu na kupiga teke sadaka ya waumini.

Kyogo alisema nabii huyo anayedaiwa kufanya kitendo hicho siyo muumini wa kanisa lao ila alikaribishwa kuendesha semina na mchungaji Baraka.

Hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo Joshua alikanusha vikali mimbari kuvunjwa na sadaka kupigwa teke na nabii huyo ila alikiri kumpa gari lake aina ya Mark II Ballon, nabii huyo ikiwa kama sadaka yake.

Hata hivyo, baadhi ya waumini wa madhehebu hayo walishangazwa na kitendo cha mchungaji Baraka kutoa gari kwa nabii huyo na kudai kuwa hivi sasa amebakiwa na gari moja bovu aina ya Escudo ambalo halitembei.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.