Habari za Punde

Wanafunzi 244 Waliofaulu Michipuo Wakabidhiwa Zawadi na Mbunge wa Jimbo la Kitope.

  Na Othman Ame (OMPR)

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitapendelea kuona Wanafunzi wa Skuli mbali mbali Nchini wanendelea kupata Taaluma yao madarasani katika Mazingira yasioridhisha.

Indhari hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi katika hafla Maalum ya kukabidhi Sare na Baskeli kwa Wanafunzi waliofaulu masomo yao ndani ya Jimbo la Kitope iliyofanyika katika uwanja wa Skuli ya Msingi Kinduni.


Jumla ya Wanafunzi 244 waliofaulu mitihani yao ya kuingia Mchepuo, Darasa la 11 na la 12 kwa mwaka 2012 wamekabidhiwa sare, Baskeli 13 kwa wale walioingia Darasa la 13 na Baskeli 7 kwa Walimu Wakuu wa Skuli saba za Jimbo la Kitope.

Tukio hilo limekwenda sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Vuai Ali Vuai Kukabidhiwa Baskeli tatu kwa Walimu wa Skuli ya Msingi ya Kidagoni Jimbo la Nungwi kufuatia ahadi ya Balozi Seif aliyoitoa wakati wa ziara yake mkoa wa Kaskazini Unguja Mapema mwezi machi Mwaka huu.

Gharama za zawadi zote hizo zinakadiriwa kufikia shilingi milioni sita na laki tano { 6,500,000/- }.

Balozi Seif alisema Taifa bora wakati wote huimarika kufuatia juhudi za Jamii kuelekeza zaidi katika masuala ya Elimu ambayo huzaa kikazi kilicho makini Kitaaluma.

Amewapongeza Wanafunzi wa Jimbo la Kitope kwa juhudi zao zilizopelekea kufaulu vyema Mitihani yao tofauti na baadhi ya wanafunzi waliotumia hila na kupelekea kufutiwa matokeo yao.

“Mmekubali kukaa Madarasani. Mkamsikiliza vyema Mwalimu wenu nini anakupeni na hatimae kumudu vyema Mitihani yenu. Kwa hili hongereni sana ”. Alionyesha Bashasha zake Balozi Seif.

Aliwaeleza Wanafunzi hao kwamba kinachohitajiwa na Taifa kwao ni kuhakikisha wanakuwa Walimu, Wahandisi, Madaktari pamoja na Wana Anga bora . Na hili halitopatikana iwapo hawatajihusisha zaidi kwenye Masomo ya Sayansi.

Balozi Seif alitoa ahadi kwa Wanafunzi hao kwamba endapo watamudu na kufaulu vyema katika masomo yao ya Sayansi atahakikisha wanapatiwa Maabara safi na ya Kisasa itakayokidhi mafunzo yao ya baadaye.

Mapema Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wizaya ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Vuai Ali amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope kwa juhudi zake zilizopelekea Wanafunzi wote wa Jimbo hilo kusoma katika Vikalio.

Nd. Vuai alisema lengo la baadaye la Wizara ya Elimu Mafunzo ya Amali Zanzibar ni kuwa na Mkondo mmoja tu wa Masomo kwa Skuli zote Unguja na Pemba.

Kwenye Hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Ndugu Vuai Ali Vuai katika kuhamasisha kutanzua uhaba wa Madarasa ya kusomea alishawishi mchango wa papo kwa papo uliopelekea walioshuhudia hafla hiyo kutoa ahadi ya kuchangia Ujenzi wa Jengo jengine la Skuli ya Kinduni.

Mchango huo wa papo kwa papo umezalisha ahadi za matofali 3,000 gari za Mchanga na Fedha Taslimu kutoka kwa Maafisa na Viongozi wa Sekta tofauti wakati Mke wa Mbunge wa Jimbo hilo Mama Asha Suleiman Iddi akaahidi kuchangia gharama zote za Ujenzi wa Msingi wa Jengo hilo pamoja na Saruji yake.

1 comment:

  1. Hivi jamani wabunge wengine wako wapi?
    Au ndio wanainvest kwenye ndoa tu, kama mbunge, naskia ana wake watatu!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.