Serikali yapania kuyaimarisha, kutengeneza ajira
Watendaji wasipuuze malalamiko ya wafanyakazi
Asema kasi ya uzalishaji dawa mfumko wa bei
Na Salum Vuai, MAELEZO
KUWAPATIA wafanyakazi maslahi bora na haki zao za msingi pamoja na kutengeneza ajira mpya kwa vijana, ndio ajenda kuu za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani 'May day' yaliyofanyika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na wafanyakazi wa sekta na wizara mbalimbali pamoja na watendaji wa ngazi tafauti serikalini, Dk. Shein alisema serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa wafanyakazi na hivyo inafanya jitihada kuimarisha maslahi yao kila uwezo unaporuhusu.
Alifahamisha kuwa, wafanyakazi ni watu muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote duniani, kwani wao ndio rasilimali inayotegemewa katika kuzalisha mali na kunyanyua uchumi wa nchi.
"Kwa kutambua umuhimu huo, serikali ya Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kujenga mazingira mazuri kwa wafanyakazi ili waweze kuzalisha zaidi, kuongeza pato la Taifa na kuendesha maisha yao", alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema katika kuhakikisha hali za wafanyakazi kimaisha zinaimarika, serikali imekuwa ikiendeleza ushirikiano na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi, kushauriana juu ya njia bora za kuinua maisha ya wafanyakazi hao.
Dk. Shein aliwakumbusha watendaji wa ngazi mbalimbali za serikali, kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuhakikisha wanawatendea haki wafanyakazi wao, kwa kuwasikiliza badala ya kuwapuuza au kuwakimbia, ili waweze kuwa na ari ya kujituma na kuliletea maendeleo taifa lao.
Alisema, wasipotendewa haki, wafanyakazi hawataacha kulalamika na kupoteza imani na serikali yao, hasa pale wanapofahamu ugumu wa kazi wanazofanya kulinganisha na maslahi duni wapatayo.
Alifahamisha kuwa, katika mchakato wa serikali kupandisha viwango vya mishahara, malalamiko yote yaliyotolewa na wafanyakazi yasikilizwe, na kama wapo waliopunjwa basi walipwe stahiki zao pamoja na malimbikizo.
"Huwezi kumtwisha mtu mzigo mzito kichwani bila kumpa kata ya kumrahisishia kuubeba, ukifanya hivyo utakuwa unamuumiza, lazima wafanyakazi walipwe kwa mujibu wa jasho lao kulingana taratibu za utumishi serikalini", alisisitiza.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa, haki hizo ni lazima ziende sambamba na uwajibikaji wa wafanyakazi hao, akinukuu maneno ya Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, aliyewahi kusema, "Haki na wajibu ni watoto pacha".
Aliwahimiza wafanyakazi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuacha tabia ya kuchelewa kazini na kuondoka kabla ya wakati, kwani pamoja na kulilia haki na maslahi nao wanapaswa kuhakikisha kipato wanacholipwa ni cha halali.
Alisema kwa kuonesha namna serikali inajali wafanyakazi wake na kuwatakia unafuu ya maisha, aliamua kuanzisha wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika pamoja na ile ya Utumishi ya Umma na Utawala Bora, kwa lengo la kujenga mazingira mazuri wa wafanyakazi pamoja na kuandaa njia za kutengeneza ajira mpya kwa vijana.
Mbali na kupandisha mishahara katika sekta ya umma, alisema pia mageuzi makubwa yamefanyika kuhusiana na maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi kwa kuwaongezea mishahara ya kima cha chini kutoka shilingi 70,000 hadi 145,000, sambamba na kutimiza mapendeklezo ya Umoja wa Mataifa kwa kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa majumbani, na kuwaongezea mshahara wa shilingi 60,000 kutoka 30,000.
Aliwataka vijana wasisubiri ajira za serikali pekee, bali wawe tayari kujiajiri, pamoja na kuwashauri waajiri kushirikiana na serikali katika kutatua tatizo hilo kwa kuongeza fursa za ajira za heshima kwa vijana.
Kuhusu mfumko wa bei, alisema dawa pekee ni kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, ambapo katika hilo, serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha kilimo kwa kuwapunguzia bei za pembejeo wakulima.
Aliendelea kusisitiza haja ya kudumisha amani na utulivu nchini, pamoja na kutumia fursa na uhuru wa kutoa maoni bila ya jazba hasa katika mchakato wa kupendekeza maoni ya katiba mpya, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa mwezi Agosti mwaka huu.
Akisoma salamu za wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) Khamis Miwnyi Mohammed, alisema kilio kikubwa cha wafanyakazi ni mfumko wa bei, kodi kubwa na mishahara duni, ambayo haikidhi haja katika kuendesha maisha yao na familia zao.
Aidha, alieleza ZATUC haikufurahishwa na hatua ya kutoshirikishwa wakati wa mchakato wa kupanga mishahara mipya mwaka uliopita, na hivyo kukosa fursa ya kutoa mapendekezo yao kwa niaba ya wafanyakazi nchini.
Katibu huyo alisema wafanyakazi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto iikiwemo wale wa sekta binafsi kunyimwa haki zao ipasavyo, pamoja na kudhalilishwa na kubaguliwa.
Hata hivyo, aliishukuru serikali kwa kutoa ushirikiano na shirikisho lake, katika kuimarisha hali za wafanyakazi wa ngazi za chini na kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), Salahi Salum Salahi, alisema kupanda kwa bei za bidhaa, ukubwa wa kodi unaiathiri pia sekta ya uajiri, na hivyo kusababisha kurudisha nyuma mpango wa kuwaongezea maslahi wafanyakazi wake.
Aidha alisema, jumuiya yake haiamini kuwa migogoro kazini ni njia nzuri ya kumaliza matatizo ya wafanyakazi, bali kujituma na kuzalisha kwa wingi, ndiko kutakaosaidia kuwainulia kipato waajiriwa wao.
No comments:
Post a Comment