Afungiwa mwaka, timu yatwangwa faini
Mtende Rangers yatinga ligi kuu Zanzibar
Na Salum Vuai, Maelezo
WAKATI mchezaji mmoja wa timu ya JKU akimpiga kichwa mwamuzi uwanjani na kusababisha mchezo uvunjike, kitendo hicho kimeisaidia timu ya Mtende Rangers kupanda daraja la Ligi Kuu ya Zanzibar msimu ujao.
Mchezaji Khamis Kombo Faki wa wajenga uchumi wa JKU, alidaiwa kufanya kitendo hicho wakati wa mchezo wa ligi daraja la kwanza kati ya timu yake na Mtende Rangers uliochezwa Aprili 26, mwaka huu katika uwanja wa Dimani, kwa kumpiga mwamuzi Issa Haji Vuai na kusababisha apasuke kichwa na kushonwa nyuzi tatu.
Wakati kitendo hicho kikifanyika katika dakika ya 34 ya mchezo, JKU ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Amour Omar Janja.
Barua ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ya Aprili 30, 2012 iliyotumwa kwa makatibu wa timu timu za JKU na Mtende Rangers, imefahamisha kuwa, baada ya kuzingatia ripoti za kamisaa na mwamuzi wa mchezo huo, chama hicho kimebaini kuwa, kitendo hicho cha utovu wa nidhamu ndicho kilichosababisha mchezo huo kutokumalizika kwa wakati wake wa kawaida.
Aidha, barua hiyo iliyosainiwa na Massoud Attai Massoud kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa ZFA, ilieleza kuwa, kujeruhiwa huko kwa mwamuzi ndiko kulikomfanya ashindwe kuendelea kuchezesha na hivyo kupuliza firimbi ya kumaliza pambano hilo.
Kutokana na kitendo hicho, ZFA imeamua kumfungia mchezaji Khamis Kombo Faki kucheza mechi zinazoandaliwa na chama hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Aprili 30, mwaka huu, kwa mujibu wa kanuni za kuendeshea mpira daraja la kwanza kifungu cha 15 (a).
Sambamba na kifungo hicho, mwanandinga huyo pia amepigwa faini ya shilingi laki moja kwa mujibu wa kifungu 15 (b), ambayo ametakiwa ailipe si zaidi ya tarehe 15 Mei, 2012, vyenginevyo adhabu zaidi itachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyengine, timu ya JKU nayo imepigwa faini ya shilingi laki mbili ambayo imetakiwa kulipa si zaidi ya tarehe 30 Mei, mwaka huu.
ZFA pia imeamua kuipa Mtende Rangers ushindi wa magoli mawili na pointi tatu, hatua inayoifanya sasa ifikishe pointi 40 na kuwa mabingwa wa ligi hiyo, na hivyo kucheza ligi kuu msimu ujao.
Kwa uamuzi huo, Mtende inaungana na mabingwa wa Pemba katika ligi daraja la kwanza timu ya Duma ambayo pia inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi, kucheza ligi kuu, huku zikisubiri mshindi kati ya Bandari kutoka Unguja na Hard Rock ya Pemba zitakazopambana kutafuta timu ya tatu itakayopanda ngazi pamoja nazo.
No comments:
Post a Comment