Habari za Punde

Rage: Jezi ya Mafisango haitarithiwa
JK amlilia, atuma ranmbirambi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KUFUATIA kifo cha mchezaji Patrick Mafisango wa klabu ya Simba, imeamuliwa kuwa, jezi nambari 30 aliyokuwa akivaa, sasa haitatumika tena, ikiwa ishara ya kumuenzi kwa heshima.

Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage, ametoa kauli hiyo wakati akisoma taarifa maalum ya salam kutoka klabu hiyo, kwenye shughuli za kuuaga mwili wa marehemu Mafisango zilizofanyika katika viwanja vya TCC, Chang'ombe jana.

Hata hivyo, Rage alishindwa kumalizia taarifa hiyo kutokana na uchungu na taarifa hiyo ikamalizwa kusomwa na msaidizi wake Geofrey Nyange Kaburu.

Wakati wa shughuli hiyo, watu kadhaa walianguka kwa kushindwa kuvumilia, akiwemo kiungo wa timu ya Simba Haruna Moshi 'Boban', ambaye alifika msibani hapo akiwa amevaa kandambili za rangi ya bluu, na 'T-Shirt' ya Kilimanjaro, ambayo ni sare ya wachezaji wa timu ya Taifa waliofika eneo hilo.

Boban, aliinuliwa na wachezaji wenzake wa Simba wakati wakielekea kuaga mwili wa marehemu, na alipofika mbele ya jeneza alishindwa kujizuia akaregea na kupoteza nguvu, na kusaidiwa na wenzake, wakiwemo wachezaji wa timu ya Taifa.

Wakati huohuo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage, kuomboleza kifo cha marehemu Patrick Mafisango.

Mafisango alipoteza maisha wakati gari alilokuwa akiendesha lilipopata ajali katika eneo la Chang’ombe, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia juzi Mei 17, 2012.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuhuzunishwa na upotevu wa maisha ya mchezaji huyo ambaye katika miaka yake michache ya uchezaji nchini Tanzania amechangia maendeleo ya soka kupitia klabu yake ya Simba.

"Nimepokea kwa mshtuko na huzuni habari kifo cha Patrick Mafisango katika ajali ya gari ambayo nimejulishwa ilitokea asubuhi ya kuamkia jana (juzi) katika eneo la Chang’ombe mjini Dar es Salaam," alieleza Rais Kikwete na kuongeza:

"Nakutumia wewe Mheshimiwa Mwenyekiti salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa kwa klabu ya Simba na wanamichezo wote nchini. Nakuomba kupitia kwako uwafikishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa wana-familia wote wa marehemu Mafisango, wana-Simba wote popote walipo na wanamichezo wa Tanzania kwa jumla."

Rais ameongeza kwa kusema: "Wajulishe wote kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Aidha, wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mweyezi Mungu, mwingi wa rehema aiweke mahali pema peponi roho ya marehemu Patrick Mafisango. Amen."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.