Habari za Punde

Maalim Seif: Upigaji Chapa Waandaliwe ‘Kidigitali’


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali baada ya kufanya ziara katika kiwanda cha upigaji chapa kilichopo Saateni mjini Zanzibar.

Wafanyakazi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali wakisikiliza maelezo ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, alipofanya ziara katika kiwanda cha Upigaji chapa kilichopo Saateni.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohammed Aboud Mohammed akimuelekeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif katika jengo linalotarajiwa kuhamishiwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali huko Maruhubi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia ramani ya matengenezo ya jengo lililokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi, ambapo ofisi za Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali zinatarajiwa kuhamia hapo baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Anaetoa maelekezo ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali Bw. Iddy Suweid

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akiangalia kitabu kilichopigwa chapa katika kiwanda cha upigaji chapa cha serikali Saateni wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho. (Picha, Salmin Said, OMKR). 

 Na Hassan Hamad, OMKR

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi wa Idara ya Mpigaji Chapa Mkuu wa Serikali hawana budi kuwaandaa wafanyakazi kitaaluma, ili wamudu kufanya kazi katika mazingira za kisasa, kufuatia kazi inayoendelea ya kuiimarisha utendaji wa taasisi hiyo. 

 Maalim Seif alisema hayo jana huko Saateni, alipokuwa akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Idara hiyo, alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji na kujionea hatua za maandalizi ya kuhamishia shughuli za Idara hiyo katika eneo la Maruhubi. 


 Alisema wafanyakazi wa Idara hiyo wanastahili pongezi kubwa kutokana na ujasiri wanaouonesha wa kufanyakazi katika mazingira magumu, ikiwemo kuendelea kutumia mashine za muda mrefu uliopita, pamoja na kukabiliwa na tatizo la kuvamiwa na maji eneo lao wakati wa mvua nyingi. 

 Alieleza kuwa baadhi ya mashine zinazoendelea kufanya kazi hadi sasa kiwandani hapo ni zile zilizofungwa tokea karne ya 19, hali inayomaanisha wafanyakazi hao wanafanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano kuzifanyia matengenezo na hadi sasa ziendelee kufanya kazi. 

Aidha, Maalim Seif alisema katika juhudi za kuimarisha utendaji wa Idara, Serikali imo katika hatua ya kununua baadhi ya mashine mpya za kisasa, hivyo wafanyakazi wanahitaji waandaliwe katika mazingira hayo, ikiwemo matumizi ya teknolojia ya Digitali. 

Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye alifuatana na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema mitambo na mashine hizo mpya zitafungwa moja kwa moja katika eneo la Maruhubi, ambako kuna sehemu ya kutosha na iliyo na mazingira salama. 

 “Serikali imeamua kukifanya kiwanda hiki kiwe cha kisasa kabisa, mambo ya ‘manual’ yamekwisha, hivyo viongozi mhakikishe wafanyakazi wanapata mafunzo kujiandaa kuyakabili mazingira mapya, alihimiza Maalim Seif. 

Wafanyakazi wa Idara hiyo walimpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais kwa uamuzi wake wa kutembelea taasisi hiyo na kujionea mazingira halisi, ambapo pia walimueleza baadhi ya matatizo yanayowakabili katika shughuli zao za kila siku za kazi. 

Miongoni mwa matatizo hayo ni madai ya siku nyingi ya posho zao, malalamiko yao ya kuwa na mazingira bora ya kiafya, ikiwemo dai la kupatiwa maziwa na kulipwa posho nyeti. 

Waziri Aboud akizungumza katika mkutano huo, aliahidi watayafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na wafanyakazi , ili kila mmoja aweze kupata haki anayostahiki na kazi hizo ziendelee kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.

1 comment:

  1. Makini hao wamama wanatia huruma, wanaonesha majonzi kama vile wapo msibani!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.