Habari za Punde

Maoni ya Kamati ya Kudumu - Bajeti ya Afisi ya Rais




MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/ 2013

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyeezi Mungu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana kwa mara nyengine ili tuendelee kujadili majukumu tuliyopewa na Wananchi wetu, likiwemo jukumu hili la kujadili suala la Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Taasisi mbali mbali za Serikali ikiwa leo tunajadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, pili, naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama  mbele ya Baraza lako tukufu ili niweze kuwasilisha Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi  Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2012/2013.


Mheshimiwa Spika, naomba nisiwe mwizi wa fadhila kwa kumpongeza  Mheshimiwa Waziri na Watendaji wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano yao wanayotupa katika shughuli za   kamati na Baraza kwa ujumla. Vile vile napenda kuishukuru Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwasilisha mbele ya kamati yetu pamoja na Baraza lako tukufu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2012/2013 ili, kama Katiba na Kanuni zetu zinavyoelekeza, yaridhiwe na Wajumbe wako kwa njia ya mjadala kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa kuwashukuru kwa dhati Wajumbe wa Kamati yetu kwa mashirikiano yao makubwa wanayonipa katika kutekeleza majukumu ya kazi zetu. Aidha, naomba niwashukuru Wajumbe wa Kamati kwa michango, maoni na ushauri wanaoutoa wakati tunapokuwa pamoja katika shughuli zetu za Kamati pamoja na shughuli za Baraza letu kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, naomba niwataje waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kama ifuatavyo:-

1.       Mhe. Hamza Hassan Juma                -         Mwenyekiti
2.       Mhe. Mwanajuma Faki Mdachi           -         Makamu Mwenyekiti
3.       Mhe. Ali Salum Haji                            -          Mjumbe
4.       Mhe. Mgeni Hassan Juma                 -         Mjumbe
5.       Mhe. Mohammed Haji Khalid            -        Mjumbe
6.       Mhe. Salma Mohammed Ali                 -        Mjumbe
7.       Mhe. Ussi Jecha Simai                          -        Mjumbe
8.       Ndg. Rahma Kombo Mgeni              -         Katibu
9.       Ndg. Ramadhan Kh. Masoud           -         Katibu


Mheshimiwa Spika, baada ya Utangulizi huo, sasa kwa niaba ya Kamati yetu, sasa  naomba nianze kuichangia Hoja ya Waziri kwa uniruhusu kuwasilisha maoni ya kamati yetu kama ifuatavyo:-

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kwa kuanzisha Tovuti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na kutayarisha barua pepe za watendaji wa ofisi hiyo. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaipongeza Idara hii kwa kuanzisha Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kamati inaamini kuwa kuanzishwa kwa tovuti na kitengo hicho kutaiwezesha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kufanya kazi zake kwa ufanisi lakini pia kuiwesha Ofisi hii kufahamika nje na ndani ya nchi yetu.

OFISI YA FARAGHA YA RAIS
Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza kwa dhati ziara za nje na ndani ya nchi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais na wajumbe wake mbali mbali. Kamati yetu inaamini kuwa ziara hizi zinaongeza chachu ya maenedeleo katika nchi yetu. Hata hivyo, kamati inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Ofisi ya Faragha kuwa katika ziara hizo kadri itavyowezekana kuwakumbuka kuwajumuisha Wajumbe wa Kamati ili nao wapate nafasi ya kujifunza na kuishauri Serikali ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, kamati vile vile imefarajishwa na maelezo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Mkataba wa Makubaliano na Serikali ya Ras el Khaimah katika nyanja kadhaa za kiuchumi na maendeleo, kama vile masuala ya Afya kwa kusaidiwa katika matibabu ya maradhi ya kisukari, figo, moyo na saratani. Mheshimiwa Spika, kamati inaomba ipatiwe ufafanuzi wa makubaliano hayo kwa maana Zanzibar iatapatiwa madaktari na vifaa kutoka Ras el Khaimah? Au madakatari wetu watakwenda kujifunza huko? Au tutajengewa hospitali itakayojihusisha na maradhi hayo? Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yatakayotolewa na Mheshimiwa Waziri, ni muhimu kukumbuka kuwa miongoni mwa mashaka makubwa yanayoikabili sekta ya Afya katika nchi yetu ni ukosefu wa vifaa vya kisasa pamoja na uhaba mkubwa wa wataalamu kwa maana ya madaktari wa maradhi ya tofauti. Hivyo, kamati yetu inawaomba viongozi wetu wanapopata fursa ya kupatiwa misaada ya Afya basi washawishi sana misaada hiyo ijikite kwa kupatiwa vifaa na kuwapatia madakatari wetu nafasi za masomo nje ya nchi ili wakapate mafunzo katika maradhi ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa sana hapa Zanzibar. Mheshimiwa Spika, Sukari, Saratani, figo, sindikizo la damu na maradhi ya baridi ni miongoni mwa maradhi kadhaa na mazito yanayoitesa Zanzibar, amabayo yanahitaji vifaa na wataalamu wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, kamati inaendelea kuipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuweza kulifanyia matengenezo Jengo la Ikulu ya Mnazi mmoja na lile la Chake Chake. Hata hivyo, kamati yetu inaikiumbusha Seriakali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuyafanyia matengenezo makubwa Majengo ya Ikulu ya Mkoani na Dodoma. Kwa ujumla majengo haya ni chakavu na hayana hadhi ya makaazi ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Spika, kamati yetu pia inaomba ipatiwe ufafanuzi wa kutosha kuhusu suala la kuliimarisha Jengo la Ikulu ya Kibweni kwa kulipaka rangi katika kuta zake za nje pamoja na kuimarisha bustani ya Ikulu hiyo. Mheshimiwa Spika, tunaomba ufafanuzi kwa sababu Jengo hilo lilipakwa rangi ambayo inaonekana haikuwa na kiwango lakini mazingira ya bustani yake hayaridhishi. Mheshimiwa Spika, kamati yetu pia inaikumbusha Ofisi hii kuyafanyia matengenezo majengo ya Ikulu ya Mkoani na Dodoma ambayo kiukweli hayana hadhi ya kuwa Makaazi ya Mheshimiwa Rais. Aidha, tunakumbushia suala la kuwekwa uzio katik eneo la Nyumba ya Seriakali iliyopo Mkokotoni, ambako mazingira yake yanachafuliwa na wanyama wanaofungwa katika eneo hilo. Kamati bila ya kusahau, inaiuliza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ule mpango wa kulihami Jengo la Serikali liliopo Fumba, ambalo eneo lake linanyemelewa kuliwa na bahari, umefikia wapi? Au ndio limetiwa kapuni?

IDARA YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA URATIBU WA SHUGHULI A WAZANZIBARI
Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazochukuliwa na Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje. Kamati inaamini kuwa wazo la kuanzishwa kwa Idara hii pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Idara hii kutawawezesha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuisadia nchi yao kiuchumi na kijamii. Kamati katika kazi zake ilipewa taarifa kuwa Idara hii katika siku za usoni inatarajiwa kuhamishiwa katika eneo ambalo itaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kamati inafarajishwa na taarifa hii kwa sababu eneo wanalolitumia hivi sasa ni finyu na halitoshelezi kwa shughuli zao za kiofisi. Kamati vile vile inaishauri Idara hii kushirikiana na Wazanzibari waliopo Zanzibar ambao waliishi nje ya nchi kwa miaka mingi kwa lengo la kupata taarifa zitakazawasaidia katika kazi zao. Kamati yetu pia inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Idara hii kuendelea kujifunza katika nchi zilizofanikiwa na utekelezaji wa dhana ya Diaspora. Miongoni mwa nchi hizo ni Ghana, India na nchi za “latin America”.

Mheshimiwa Spika, Idara hii kwa mujibu wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri hutangaza dhana ya Diaspora kupitia ZBC TV na Redio. Kamati yetu inaamini kuwa kuitangaza dhana hii mpya kwa kutumia vyombo hivi pekee haitoshelezi. Hivyo, kuna haja ya kuitangaza dhana hii kwa kutumia vyombo vya habari zaidi ya hivyo ili iweze keeleweka vyema. Aidha, kwa kuwa dhana hii bado ni mpya kuna haja kwa viongozi mbali mbali wa nchi hii kupatiwa elimu ambayo itawapa uelewa zaidi kuhusu suala la diaspora na umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kwa lengo la kuwawezesha Wazanzibari wanaoishi za nje kuisaidia nchi yao, kamati yetu inaona kuwa, kuna changamoto za msingi zinazoikabili Zanzibar katika utekelezaji wa Ushirikiano wa Kimataifa na dhana nzima ya Diaspora. Miongoni mwa   changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar katika suala la Ushirikiano wa Kimataifa ni kwamba kwa kuwa suala la Ushirikiano wa Kimataifa limewekwa katika masuala ya Muungano, Zanzibar imekuwa ikishiriki katika Vikao vya Kikanda na vya Kimataifa kwa mwa mvuli wa Muungano huku ikichukuliwa kama vile kushiriki kwake katika vikao hivyo sio suala la lazima bali ni ihsani ya Jamhuri ya Muungano. Baya zaidi katika vikao hivyo kuna mambo yanayojadiliwa na kupitishwa si ya Muungano lakini bado Zanzibar inashiriki kwa mwa mvuli huo ambao kwa muda mrefu sasa umeonekana kuwa ni kero kwa wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa spika, kwa kuwa kuna mchakato wa utoaji wa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya, kuna umuhimu kwa Wazanzibari kuhakikisha kuwa masuala ya Mambo ya Nje yanakuwa si ya Muungano ili Zanzibar iwe na uwezo wa kushiriki katika vikao mbali mbali ikiwa nchi kamili.

KITENGO CHA USALAMA WA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, kitengo cha Usalama wa Serikali kimepewa Majukumu muhimu sana kwa lengo la kuimarisha usalama katika taasisi na vituo muhimu vya Serikali. Hata hivyo, Kitengo hiki, mbali na jitihada kinazozichukua katika kutekeleza majukumu yake, hakipatiwi fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza kazi ilizopangiwa. Aidha, kitengo hiki hakina usafiri wa kufuatilia kazi zao, ingawa kwa mujibu wa Bajeti ya mwaka 2012/2013, kimetengewa fedha kwa ajili ya usafiri. Kamati inaisistiza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kukipatia kitengo hiki fedha za kutosha ili kiweze kutekeleza kazi zake kwa ufanisi zikiwemo kazi za kuyakagua majengo ya Taasisi za Serikali yaliyopo Tanzania Bara, ambayo yanashindwa kukaguliwa kutokana na ukosefu wa fedha. Aidha, kamati inaona kuwa kuna haja kwa kitengo hiki kupatiwa usafiri wa gari na vespa ili kiweze kufuatilia kwa ufanisi kazi ilizopangiwa. Kamati pia inaiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kukisaidia kitengo hiki kwa kukiwezesha watendaji wake kupatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili nao waweze kuimarisha utendaji wao.

Mheshimiwa Spika, kamati kwa mara nyengine inakikumbusha Kitengo cha Usalama wa Serikali kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Serikali zinafuata Sheria na taratibu kwa kuhakikisha kuwa Watumishi wa Serikali wanaajiriwa baada ya kufanyiwa upekuzi kwa maana ya “Vetting”. Kamati kwa upande mwengine inaona kuwa kuna haja kwa Serikali kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa kigeni wanaofanya kazi katika sekta binafsi nao wanafanyiwa upekuzi kwa lengo la kuimarisha usalama katika sehemu wanazofanyia kazi pamoja na nchi kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu mkubwa suala hili likafanyiwa kazi ili kuweza kuzifahamu tabia za wafanyakazi hao wanaofanyakazi katika sekta binafsi ili tuepukane na madhara yanayoweza kutokea.

Mheshimiwa Spika, kamati imebaini kuwa Sheria ya Upekuzi kwa wafanyakazi ina mapungufu kwa maana kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kinapobaini kuwa kuna udanganyifu umefanyika katika suala la upekuzi wa wafanyakazi wapya, wao hutoa ushauri tu kuwa wafanyakazi hao wasiajiriwe lakini Sheria haianishi waajiri na waajiriwa waliodanganya katika zoezi zima la uajiri wachukuliwe hatua gani. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inapendekeza Sheria hiyo kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kukiwezesha Kitengo cha Usalama wa Serikali kuweza kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki katika udanganyifu wa ajira.

Mheshimiwa Spika, katika kuunganisha suala la usalama katika utekelezaji wa Sughuli za Serikali, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya Taasisi za Seriakali wahasibu na washika fedha wao huchukua pesa za mishahara kutoka benki bila ya kuwepo Uinzi wa Polisi, ambao kupatikana kwake huwa hauna gharama yoyote ile.Mheshimiwa Spika, Suala hili kiusalama ni hatari na halikubaliki. Hivyo, kamati inaziagiza Taasisis za Serikali kuhakikisha kuwa pesa za mishahara zinazochukuliwa benki zinakuwa na ulinzi wa polisi. Aidha, Kamati inaziagiza Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa watumishi wao wakiwemo washika fedha na wahasibu kutozilaza funguo za ofisi majumbani mwao ili kuepuka uwezekano wa upotevu wa funguo hizo. Kamati inazishauri taasisi za Serikali kuweka sehemu maalum za kuweka funguo hizo (combination lock.) Kamati pia inaona kuwa kuna umuhimu katika milango ya wahasibu na washika fedha kuwekwa milango ya “Grills” kwa lengo la kuimarisha usalama katika ofisi hizo. Kamati yetu bila ya kusahau inazikumbusha Tasisi za Serikali kuweka vifaa vya kuzimia moto “Fire Extinguishers” katika majengo yao ili ziweze kukabiliana na maafa ya moto yanayoweza kutokea.

OFISI YA USAJILI NA KADI ZA UTAMBULISHO
Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi hii kwa kuendelea na jukumu la kusajili na kutoa Vitambulisho vya Ukaazi vya Mzanzibari. Hata hivyo, kamati inaona kuwa kuna haja ikatolewa elimu zaidi kwa wananchi kwa lengo la kuwahamasisha kuchukua vitambulisho vyao katika vituo walivyopangiwa. Mheshimiwa Spika, tunalisema hili kwa sababu wakati kamati ilipokuwa Pemba kikazi ilifahamishwa kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi waliokuwa hawajachukua vitambulisho vyao.

Mheshimiwa Spika, kamati inaipongeza Ofisi hii kwa kutoa elimu kuhusu kuelimisha matumizi bora ya Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kupitia ZBC TV. Hata hivyo, kuna haja kwa Ofisi hii kutoa elimu hiyo kwa kuvitumia vyombo vya habari zaidi ili elimu hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza hatua ya utayarishaji wa Rasimu ya Marekebisho ya Usajili Nambari 7 ya 2005 inayoruhusu Utoaji wa Vitambulisho vya Wageni wanaoishi nchini. Kamati inashauri kuwa marekebisho ya rasimu hiyo yanahitajika kuwa madhubuti ili kuepuka changamoto zilizojitokeza hapo kabla katika suala zima la utoaji wa vibali vya ukaazi kwa wageni wanaoingia nchini.

IDARA YA URATIBU WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri inaeleza kuwa Idara hii kupitia Mabaraza ya Halamashauri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekamilisha utayarishaji wa Sheria ndogo ndogo za Serikali za Mitaa. Kamati inaikumbusha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuziwasilisha Sheria hizo hapa Barazani ili zipitiwe na Kamati ya Sheria Ndogo Ndogo ambayo imejumuishwa katika Kanuni mpya za Baraza, toleo la mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mradi wa ZUSP kwa kununu vifaa kama vile gari, vespa na Honda kwa ajili ya kuliimarisha Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji Pemba, Idara ya Mipango Miji na Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kamati inaamini kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo utaziwezesha taasisi hizi kufanya kazi zao zikiwemo kazi za kusafisha miji kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kamati vile vile inafarajishwa na maelezo ya kuwa Serikali imekwishaziwasilisha katika Benki ya Dunia hadudi rejea za kumtafuta mshauri wa Kusimamia Uwekaji wa Taa za Barabarani. Mheshimiwa Spika, suala la uwekaji wa taa hizi katika mitaa na miji yetu lina umuhimu wa pekee hasa ikitiiliwa maanani kwamba maeneo mengi ya Manispaa ya Zanzibar kutokana na ukosefu wa taa hizo nyakati za usiku huwa hayako salama kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, tunaipongeza kwa dhati Serikali kwa kuchukua hatua za kulenga kumtafuta mjenzi wa utanunuzi wa ukuta unaopita pembezoni mwa pwani ya Forodhani bila shaka kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya maeneo hayo na kuweka usalama wa wananchi wanaoutumia maeneo hayo.

MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MIKOA

Mkoa wa Mjini Magharibi
Mheshimiwa Spika, kamati inatoa pongezi kwa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuwapatia mafunzo mbali mbali Masheha pamoja na Kamati zao za Maendeleo. Bila shaka mafunzo hayo yatawawezesha kutakeleza majukumu yao kwa ufanisi. Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri inaainisha kuwa Mkoa umefanya ziara kufuatilia uharibifu wa mazingira na kufanya vikao na wadau wengine ili kuzungumzia usafi wa mji na uzururaji wa wanyama. Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihda hizo, uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Mjini Magharibi umeenea kila pahala kuanzia nchi kavu hadi baharini. Kamati inataka kuelewa baada ya ufuatiliaji huo, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Mkoa wa Mjini Magharibi imechukua hatua gani katika kudhibiti uharibifu huo katika maeneo hayo hususani maeneo ya Mbuyu Mnene, Amani, Maruhubi, Ukanda wa bahari wa kizingo na kadhalika. Kuhusu suala la usafi kamati inaipongeza Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia taasisi zake pamoja na vikundi mbali mbali vya mazoezi na Jumiya zisizo za Kiserkali kwa kuchukua hatua za kuusafisha mji wetu kila Jumamosi ya Mwisho wa mwezi. Hata hivyo, tunaiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuongeza vifaa vya usafishaji kwa lengo la kuimarisha usafi katika miji yetu.

Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa malengo ya Mkoa kwa mwaka 2012/2013 ni kutatua migogoro ya ardhi inayoukabili Mkoa. Kamati inataka kufahamu kwa mwaka 2011/2012, Mkoa ulikuwa na migogoro mingapi ya ardhi na mpaka sasa imeshaitatua migogoro mingapi? Mheshimiwa Spika, tunalisema hili kwa sababu suala la migogoro ya ardhi limedumu kwa miaka mingi sasa na kila mwaka liwekwa kama ni malengo ya Mikoa na taasisi nyenginezo. Mheshimiwa Spika, kamati yetu ina wasi wasi kama migogoro hiyo itaweza kutatuliwa kwa sababu kuna shutuma kwamba migogoro hiyo inawahusisha baadhi ya wale waliopewa madaraka katika Mikoa, Wilaya na Shehia. Hivyo, kamati inashauri kuna haja migogoro hiyo ikatatuliwa na watu au taasisi ambazo hazikuhusika ama kushutumiwa kuwemo katika migogoro hiyo.

Mheshimiwa Spika, ofisi ya Mkuu wa Mkoa inaanza matayarisho ujenzi wa jengo jipya la Ofisi yake huko Amaan na kufanya matengenezo ya jengo la ofisi yake hapo Vuga. Kamati inapongeza hatua hizo zinazotaka kuchukuliwa na Ofisi hii. Lakini kamati yangu haifurahishwi na matumizi mabaya ya eneo la mbele ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi hapo Amani kwa kuwekwa yadi ya Magari jambo ambalo limeharibu mandhari nzima ya eneo hili. Kamati inaikumbusha Serikali  kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kuwa na mkakati wa  kujenga Majengo mapya na ya kisasa ya Serikali kwa Wakuu wa Mikoa na taasisi za Serikali ili kuwawezesha wafanyakazi wa taasisi hizi kufanyakazi katika mazingira mazuri. Mheshimiwa Spika, .Kuna haja kwa Serikali kuwa makini na suala la kupanga utekelezaji wa ujenzi wa majengo mapya ya taasisi za Serikali, vyenginevyo kuachiwa taasisi moja pekee kutaka kujenga jengo lake kwa kutegemea pesa za Matumizi Mengineyo, kutapelekea ujenzi wa nyumba hizo kuchukuwa muda mrefu hadi kukamilika kwake.

Mkoa wa Kaskazini, Unguja
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini, Unguja, kamati inautaka Mkoa huu kulitekeleza suala la kusimamia shughuli za Ulinzi na Usalama kwa vitendo kwa sababu katika eneo la Mkoa huo kumejitokeza vitendo vingi vya uhalifu katika baadhi ya hoteli za kitaalii jambo ambalo linatishia usalama wa wenyaji na wageni kwa maana ya watalii na mali zao. Aidha, kuna haja kwa Mkoa huu kusimamia masuala ya ulinzi na usalama kwa vitendo kwa kuwa katika Mkoa huu kuna baadhi ya maeneo zipo bandari bubu zinazotumika kusafirisha na kuingiza wageni kinyume na Sheria na taratibu.

Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaukumbusha Mkoa huu kuhakikisha kuwa vibanda vilivyojengwa katika fukwe za bahari pembezoni mwa hoteli za kitalii vinabomolewa kwani vinaharibu mazingira ya fukwe lakini pia vinaikosesha Serikali mapato kwa kuwa tumebaini kuwa vibanda hivi vimejengwa kwa maslahi ya wenye hoteli na pengine baadhi ya watendaji katika Ofisi za Wilaya na Mikoa.

Mkoa wa Kusini, Unguja
Mheshimiwa Spika, kamati inaupongeza Mkoa huu kwa kuwa na jengo lake ambalo hivi sasa linatumika kwa shughuli za ofisi. Tunaiomba Mikoa mengine iige mfano wa Mkoa huu kwa kuwa na majengo yao ya kisasa. Hata hivyo, Kamati yetu inauagiza Mkoa wa Kusini kupitia kamati yake na Ulinzi na Usalama kufuatilia kwa kina masuala ya ulinzi na usalama katika Mkoa huo  kwani kumebainika kuwa kuna baadhi ya wenyeji na hata wageni wanamiliki nyumba wanazikodisha kinyume na Sheria kwa wageni na kupelekea kutishia usalama wa Mkoa na kuikosesha Serikali mapato.

Mheshimiwa Spika, kamati pia inauagiza Mkoa huu kuhakikisha kuwa vibanda vyote na miamvuli iliyojengwa katika fukwe za bahari na kupelekea kuharibu mazingira vinabomolewa mara moja kwa lengo la kdhibiti mazingira katika maeneo hayo. Aidha, kamati inauagiza Mkoa wa Kusini Unguja kwa kushirikiana na Ofisi za Wilaya na Masheha, Idara ya Ardhi kuhakikisha kuwa nyumba zote walizokodishwa wageni zinaorodheshwa na kutoa taarifa  Polisi,Uhamiaji, Zipa, na ZRB ili kila taasisi iwajibike kwa lile linalowahusu. Pia kamati yangu inazitaka Ofisi zote za Wakuu wa wilaya kushirikiana na masheha kuzibua njia zote zilizozibwa na wawekezaji za kuteremkia Pwani ili wananchi kuweza kupita kwa urahisi wanapokwenda na shughuli zao mbali mbali za kiuchumi na kawaida huko pwani.

Mheshimiwa Spika, kamati pia inawakumbusha Viongozi katika Mkoa, Wilaya na Shehia za Mkoa wa Kusini kuhakikisha kuwa mapato yanayokusanywa katika hoteli za kitalii yanasimamiwa ipasavyo kwa lengo la kufaidisha Serikali na wananchi wake. Mheshimiwa Spika, kamati inalikumbusha suala hili kwa viongozi hawa kwa kuelewa kuwa katika Mkoa wa Kusini, mapato yanayotokana na kodi ya hoteli za kitalii yanavuja kutokana na kutosimamiwa vyema na viongozi hao. Kamati yetu pia inawakumbusha viongozi hawa kuwa kwa mujibu wa Sheria za Kodi wanatakiwa wajielewe wao ndio wasimamizi wa kodi ktika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kutokana na udhaifu unaoneshwa na baadhi ya viongozi hao na wengineo pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali wanaopelekea kupotea kwa mapato ya Serikali, kamati inashauri pale inapobainika kutokea kwa upotevu huo, hatua za kisheria zinafaa zichukuliwe kwa wahusika. Aidha, kamati inashauri kuwa somo la kodi liingizwe katika mitaala ya skuli za sekondari ili kuwawezesha wananchi kuyajua majukumu yao ya kulipa kodi tangu wakiwa wadogo, vyenginevyo wananchi wengi huwa hawana utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari zao lakini pia huchangia kuwasaidia wageni nao kwa njia moja au nyengine kushiriki kutolipa kodi.



Mkoa wa Kusini, Pemba
Mheshimiwa Spika, kamati inaupongeza Mkoa wa Kusini Pemba kwa jitihada inazozichukua katika kutekeleza majukumu iliyojipangia likiwemo jukumu la kuwa na mpango wa kujenga nyumba ya Mkuu wa Mkoa, kuanza matayarisho ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chake na kununua jengo kwa ajili ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani. Mheshimiwa spika, jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Pemaba kiukweli halina hadhi ya kuwa Ofisi ya Mkoa. Aidha, haipendezi kwa Mkuu wa Mkoa kutokuwa na nyumba ya Serikali na badala yake kutegemea nyumba ya kukodi ambayo bila shaka huwa na gharama zake. Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa nyumba na Ofisi za Serikali kwa Viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya lina umuhimu wa pekee na linahitaji kutekelezwa kwa vitendo, vyenginevyo suala hili litaishia kwa kuelezwa katika Hotuba mbali mbali za viongozi pasina kutekelezwa. Mheshimiwa Spika, kamati yetu inaona kuwa, mbali na jitihada za Serikali kuzitengea pesa taasisi zake kwa ajili ya ujenzi wa Majengo ya Serikali, kiuhalisia pesa hizo hazitoshi katika kufanikisha ujenzi wa majengo ya kisasa na yanayokubalika kiofisi na hasa ikitiiliwa maanani katika miaka hii tuliyonayo wakati gharama za ujenzi zinapanda kila leo, bajeti ya majengo na masuala mengine ya maendeleo inapungua. Kamati yetu bado ina mashaka kuwa ujenzi uliokusudiwa, utaendelea kutekelezwa kwa utaratibu ule ule uliozoeleka wa Ofisi hii na nyenginezo kusubiri pesa za Matumizi Mengineyo kila baada ya mwezi ama miezi. Ukweli ni kuwa pesa za Matumizi Mengineyo hazina uwezo wa kujenga jengo linalohitajika kiofisi bali litajengwa jengo la kubahatisha, lisilovutia na ukamilkaji wake huchukua miaka na miaka.

Mheshimiwa spika, kamati yetu haitochoka kupiga mayowe hapa Barazani kuhusu Serikali kuwa “serious” katika kuhakikisha kuwa linakuwa na Mradi utakaotekelezwa kwa Ujenzi wa nyumba na ofisi mbali mbali za Serikali. Mheshimiwa Spika, suala hili linawezekana ikiwa Serikali itafikiria kukaa kitako na kuwatafuta marafiki wetu wa kweli kwa maana ya Wachina na wengineo ili waangalie uwezekano wa kutusaidia.

Mkoa wa Kaskazini, Pemba
Mheshimiwa spika, kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini, Pemba, ingawa jengo lao ni la kale, angalau wanafanya kazi zao katika eneo linalotizamika. Hata hivyo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kaskazini, Pemba, ni miongoni mwa Ofisi za Wakuu wa Mikoa ambazo zinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na Watumishi wa Serikali kwa maana ya wawakilishi kutoka taasisi mbali mbali za Serikali, hali ambayo imepelekea kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Mheshimiwa Spika, kamati inaishauri Serikali, ili kuitafutia ufumbuzi changamoto hii, kuweka mipango ya kuhakikisha kuwa Ofisi za Mikoa na Wilaya zinakuwa na watumishi wa kutosha kutoka kila taasisi inayohitajika.

MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

Baraza la Manispa,
Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazochukuliwa na Baraza la Manispaa katika kutekeleza majukumu yake yakiwemo majukumu ya kusimamia na kuimarisha usafi katika Manispaa ya Zanzibar. Kamati inalitaka Baraza hili kuendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa Rwanda ya pili katika masuala ya usafi. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ili Baraza hili liweze kufikia lengo la kuhakikisha kuwa Manispaa yetu inakuwa katika mazingira ya usafi tunayoyataka, kunahitajika mashirikiano ya dhati kati ya Baraza la Manispaa na wadau wengine kama vile Serikali kuu, vikundi mbali mbali vinavyotunza mazingira na masuala ya usafi, viongozi pamoja na wananchi kwa ujumla. Mheshimiwa Spika, tunalianisha hili kwa sababu wengi wetu tuna fikra suala la kusafisha Manispaa na kuimarisha mazingira ni la Baraza la Manispaa pekee na kushau kuwa wadau wengine mbali mbali nao wanahitajika kuhakikisha kuwa wanachangi nguvu zao kwa kuhakikisha kuwa wanasafisha maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira. Serikali kwa upande wake inahitajika kulisaidia Baraza hili kwa kulipatia vitendea kazi vya kutosha na maslahi bora kwa watumishi ili Baraza liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, Serikali inahitajika kulisaidia Baraza la Manispaa kwa kuliachia vianzo vya mapato ambavyo vitaliwezesha Baraza kujiendesha. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa kwa Baraza la Manispaa kujielewa kuwa mapato ya Serikali si mali ya mtu bali ni mali ya Serikali. Hivyo lihakikishe kuwa kodi zinazokusanywa ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi wetu

Mheshimiwa spika, katika kazi zake, mwezi wa Mei mwaka huu. Kamati yetu ilipata fursa ya kukutana kwa pamoja na Uongozi wa Baraza la Manispaa na vikundi vinavyojihusisha na masuala ya utunzaji mazingira na masuala ya usafi kwa lengo la kubadilishana mawazo na kuhamasisha utekeleza wa dhana ya Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya Sekta ya Umma, na Binafsi (PPP). Kamati kwa ujumla imefarajishwa na matokeo ya kikao kile kwa sababu kimepelekea washiriki wa kikao hicho sio tu kuilewa dhana hiyo bali pia kujenga mashirikiano katika shughuli zao za utunzaji mazingira na masuala ya usafi.

Mheshimiwa spika, ili kufanikisha kwa pamoja shughuli za Serikali kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali na Jamii kuhamasisha utekeleza wa dhana ya Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya Sekta ya Umma, na Binafsi (PPP). Hivyo, kamati yetu inatoa wito kwa Serikali na jamii kutoa elimu kwa viongozi, watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla ili kuweza kuielewa dhana hii mpya. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna haja kwa Serikali kuijengea uwezo sekta binafsi ili iwe nayo iwe na uwezo wa kuitekeleza kwa ufanisi dhana hii.

Mheshimiwa spika, kamati inalitaka Baraza la Manispaa kuwa na utaratibu mzuri katika utekelezaji wa miradi kati wadi mbali mbali zilizopo katika Manispaa ya Zanzibar. Kamati inalianisha hili kwa sababu imekuwa na mashaka kuwa Baraza limekuwa likitoa fedha za miradi hiyo lakini utekelezaji wa miradi hiyo huwa hauonekani.

Mheshimiwa Spika, kuna haja kuwashirikisha madiwani na masheha katika Utekelezaji wa Miradi katika wadi ili kuhakikisha ufanikishaji wa miradi   hiyo.

Mheshimiwa Spika, kamati inapongeza jitihada zinazofanywa na Halamashauri na Mabaraza ya Miji mbali mbali Unguja na Pemba. Hata hivyo, mbali na jitihada zinazofanywa na taasisi hizi, Halmashauri na Mabaraza mengi ya Miji yanakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa wataalamu hususani wanasheria na watoza kodi, ukosefu wa vitendea kazi, kuchelewa kukamilika kwa Mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Miji, kukosekana kwa mashirikiano kati yao na taasisi nyengine za Serikali katika suala zima la ukusanyaji mapato na udhibiti wa mazingira. Hali hii kwa ujumla inazipelekea tasisi hizi kutofanya kazi zao kwa ufanisi hususani katika suala la ukusanyaji wa kodi.

IDARA YA URATIBU WA IDARA MAALUM ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inavipongeza vikosi vyote vya SMZ kwa kazi kubwa wanazofanya kwa kusaidia ulinzi katika Nchi yetu, lakini pia kushiriki katika kujenga uchumi wa Nchi yetu. Hata hivyo, kamati yetu inaikumbusha Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa suala la nyongeza za mishahara katika Vikosi vya SMZ bado ni tatizo kwa maana wapo walioongezwa lakini nyongeza hiyo ni ndogo lakini nyongeza hizo hazikuzingatia muda wa mtu kuwepo kazini kwa maana mpiganaji mwenye cheo cha koplo ambaye amekipata cheo hicho leo hii, mshahara wake utakuwa sawa na koplo aliyedumu katika cheo hicho kwa miaka mingi. Mheshimiwa Spika, hili ni tatizo ambalo ukweli limechangiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutekeleza majukumu ya kurekebisha mishahara ya vikosi na taasisi nyenginezo bila ya kuzishirikisha Tume za Utumishi za taasisi husika. Mheshimiwa Spika, kamati yetu bado inaisisitiza Serikali kufanya marekebisho hayo kwa kuwapatia wapiganaji wetu haki zao za msingi wanazozidai. Aidha, kamati inaishauri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwapatia “salary sleeps” mara baada ya kulipwa mishahara yao ili kuepusha malalamiko miongoni mwa wapiganaji.

Kikosi cha Zima Moto na Uokozi
Mheshimiwa Spika, kamati inazipongeza kwa dhati kazi zinazotekelezwa na kikosi hiki. Aidha, kamati inakipongeza kikosi hiki kwa kupatiwa eneo la Mwanakwerekwe ili kiweze kutanua shughuli zake. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla kikosi hiki kinafanya kazi kubwa usiku na mchana kwa lengo la kufanya uokozi wa aina mbali mbali. Hata hivyo, kikosi hiki kinakabiliwa na changamoto kadhaa na miongoni mwa hizo ni ukosefu wa vitendea kazi, kutoshirikishwa na Idara ya Ardhi pamoja na jamii katika masuala ya ujenzi wa nyumba ili kiweze kutoa ushauri wake, kupewa mawasilano ya uongo na baadhi ya wananchi, hali ambayo inapelekea kupoteza mafuta ambayo nayo hayatoshelezi kwa matumizi ya kikosi. Changamoto nyengine kwa kikosi hiki ni kutokuwa na majengo katika maeneo ya Viwanja vya ndege na kupelekea kufanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, kamati yetu kwanza inaipongeza Serikali kwa kukiongezea kikosi hiki fungu la pesa kwa mwaka 2012/2013. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kukifikiria kikosi hiki kadri inavyowezekana kwa kukipatia pesa zaidi ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kamati inaiomba Serikali kukiwezesha kikosi hiki kwa kukipatia majengo ya kudumu katika maeneo ya uwanja wa ndege ili kiondokane na usumbufu uliopo.


Jeshi la Kujenga Uchumi (J. K.U)
Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza jitihada zinazofanywa na kikosi hichi kwa kuendeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Lakini pia kikosi kinapongezwa kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana wanaojitolea kupitia kikosi hichi ambao ni nguvu kazi ya taifa letu.Mbali na hayo kikosi kinakabiliwa na changamoto ikiwemo madeni wanayodaiwa na wafanyabiashara binafsi, ukosefu wa hati miliki katika maeneo yao, ukosefu wa umeme kwa baadhi ya kambi pamoja na vitendea kazi, huduma duni kwa vijana wanaojitolea katika kikosi na uhaba wa bajeti hali ambayo inapelekea kukwama kwa baadhi ya malengo waliojipangia.

Mheshimiwa Spika, kamati yangu kupitia Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inaomba Serikali kukiangalia kikosi hichi kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba ya kamanda huko Pemba, kuimarisha mashamba yao kwa kuchimba visima kwa ajili ya umwagiliaji maji,pamoja na kuwafikiria vijana wanaojitolea kwa kuwaajiri inapotokezea nafasi za ajira ili kuwatia moyo na wengine kuweza kujitolea.

Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (K.M.K.M)
Mheshimiwa Spika, tunatoa pongezi kwa kikosi Kikosi cha KMKM kwa kujiimarisha kwa kukipatia wataalam waliokuja kutoa mafunzo kwa ajili ya uokozi pamoja na kuongeza vifaa vya kuzamia jambo ambalo litasaidia kuwa na nyenzo za kuokolea pale maafa yatakapotokea. Pia kikosi hiki kinakabiliwa na uchakavu wa majengo yake ambayo huwafanya baadhi ya Askari wake kuishi katika mazingira magumu kwenye majengo ambayo hayastahiki kuishi Askari. Changamoto nyingine tulioiona ni kuwepo kwa rasilimali ya chelezo hapo Kibweni. Kamati yangu inaitaka Serikali kukitengeneza chelezo hichi ili kuongeza mapato na pia kurahisisha matengenezo ya vyombo vyao. Kamati yangu bado inakitaka kikosi kuwa na kitengo cha kuzamia katika kisiwa cha Pemba ili kusaidia uokozi pindipo itakapo tokea maafa. Changamoto nyingine ni upungufu wa mafuta ya kufanyia Doria kwani maumbile ya kazi yao ni kulinda baharini.

Idara ya Chuo Cha Mafunzo
Mheshimiwa Spika, Kamati inathamini kazi zinazofanywa na Chuo cha Mafunzo. Hata hivyo, pamoja na kazi kubwa zinazotekelezwa na Chuo hiki, Chuo cha Mafunzo kinakabiliwa na changamoto kama vile kuwa na uhaba wa pesa zinazoingiziwa kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa. Hali hii husababisha Chuo kupata mzigo mkubwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mahabusu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi (wafungwa). Hivyo, tunaitaka Serikali kuongeza fungu hili ili kuweza kukidhi mahitaji ya chakula kwa wafungwa na na mahabusu. Pia kamati yangu inaitaka Serikali kupitia Kikosi cha mafunzo kujenga magereza yanayokwenda na wakati kwani haya yaliyopo yamepitwa na wakati na mazingira yake hayaridhishi kiafya. Pia tunaomba kujengwa majengo maalum ya watoto ili wasichanganywe na wanafunzi watu wazima,

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kupitia Chuo cha Mafunzo kuyafanyia ukarabati mkubwa majengo wanayoishi Askari, Unguja na Pemba kwani mengi yao yamezeeka na kuchakaa sana. Pamoja na hayo kamati yangu imepata malalamiko kutoka kwa baadhi ya Askari kuwa kuna baadhi yao wamepewa barua za uhamisho kutoka Pemba kuja Unguja lakini wanaambiwa wajitegemee kwa kuwa hakuna pesa za uhamisho.  Sasa Mhe Waziri, ukija hapa kutujibu tunaomba jawabu katika hilo. Pia Kamati yangu inaitaka Serikali kupitia ushauri wa kamati kuwa Askari wote wa Vikosi vya SMZ wasilazimishwe kukatwa pesa katika mishahara yao bila ya kushauriwa kwani mshahara ni haki ya muajiriwa na inabidi kila atakachokatwa basi iwe ni lazima kwa mashauriano na muajiri wake, Mheshimiwa Spika, kamati yangu pia inaitaka Serikali kupitia chuo cha mafunzo, kuwapeleka mawakili ili kwenda vyuo vya Mafunzo kuwasaidia wanafunzi kukata rufaa kwa wale wanaohitaji.

Kikosi cha Valantia, Zanzibar (KVZ)
Mheshimiwa Spika, kamati vile vile inakipongeza kikosi hichi kwa kazi kubwa wanazozifanya hasa katika suala la kuimarisha ulinzi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini, lakini tunaomba uongozi wa kikosi hicho kwanza wao wenyewe viongozi wakuu, wawe na maelewano makubwa kwani bila ya mashirikiano yao basi, kikosi kitayumba. Kamati yetu pia inaitaka Serikali kumtafutia makaazi yanayostahiki Mkuu wa kikosi hiki kwa upande wa Pemba kwani kumpatia chumba kimoja yeye na familia yake ni kumdhalilisha kwa hiyo tunaomba suala hili lifanyiwe kazi mara moja. Pia kamati yangu inakitaka kikosi kutafuta hati miliki za maeneo yao yote ya kambi zao kwani tumegundua kuwa maeneo mengi ya kikosi hayana hati miliki. Pia kamati inakiomba kikosi hiki kupatiwa vitanda na magodoro kwa Unguja na Pemba kwani katika baadhi ya kambi mfano mzuri Pemba maofisa na askari wanalala chini. Hili ni jambo la kusikitisha Mheshimiwa Spika, nani kati yetu sisi anataka alale chini bila ya godoro? Kamati yetu pia inaishauri Serikali kukisaidia kikosi hiki kwa upande wa Pemba kwa kukipatia pesa ili kilipe madeni mengi inayodaiwa.

Mheshimiwa spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kwa mara nyengine na nawashukuru Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza kwa makini.

Mheshimiwa spika, baada ya maelezo hayo, naomba nitamke kwamba, kwa niaba ya Kamati yetu naunga mkono hoja mia kwa mia.

Mheshimiwa spika, naomba kuwasilisha.

                                    …………………………..
                                    Mhe Ali Salum Haji
Kny: Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa
                             Baraza la Wawakilishi

  



















No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.