Habari za Punde

Sheria Mabadiliko ya Katiba Kuwasilishwa Baraza la Wawakilishi. Bunge Kupokea Bajeti leo

Na Mwantanga Ame
KIKAO Cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar kinatarajiwa kuanza kesho ambapo wajumbe wa Baraza hilo wataipokea Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary akitarajiwa kuiwasilisha sheria ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao hicho ni mkutano wa nane wa Baraza la nane, kinatarajiwa kuzipokea bajeti za wizara 16 za Serikali ya Zanzibar, ambapo wajumbe wa Baraza hilo watapata fursa ya kuzijadili na hatimaye kuzipitisha.

Akizungumza na waandishi wa Habari Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahya Khamis Hamad, alisema kikao hicho kinatarajiwa kuchukua zaidi ya mwezi mmoja na masuali 197 wataulizwa mawaziri wa wizara mbali mbali.

Aidha, Katibu huyo alisema kikao hicho, kinatarajiwa kuipokea sheria ya mabadiliko ya Katiba sura ya 83, Toleo la mwaka 2012, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha sheria hiyo.

Alisema sheria hiyo inakuja ikiwa ni sehemu ya matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, chini ya kifungu cha 132 (2), kinachoelezea sheria kama hiyo baada ya kupitishwa na Bunge lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na waziri anayehusika.

Kifungu hicho kinakuja baada ya kifungu cha 132 (1) kueleza kuwa hakuna sheria yoyote itayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe kwa ajili ya mambo ya Muungano tu ipitishwe kulingana na maelekezo yaliochini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Kutokana na vifungu hivyo Katibu huyo alisema sheria hiyo itawasilishwa kwa wajumbe hao na kuipitisha bila ya kuwapo mjadala kutokana na kuwa tayari ilishapitishwa na wajumbe wa pande mbili za Muungano.

Alisema utaratibu huo unafanyika ni kwa mujibu wa Katiba ya Muungano ambayo kuja kwa sheria hiyo hairuhusu kujadiliwa upya ila utaratibu ni lazima iwasilishwe mbele ya Baraza la Wawakilishi.

Aidha alisema mjadala juu ya Bajeti ya Zanzibar unatarajiwa kuanza kusikilizwa kuanzia Jumatatu ijayo baada ya wajumbe hao kuipokea ikiwa ni hatua ya kuwapa muda ya kuitafakari kwa kina.

Aidha, Katibu huyo alisema katika kikao hicho pia Wajumbe hao wanatarajia kuupokea mswada wa sheria wa kuidhinisha Matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 (Appropriation Bill) na mswada wa Fedha (Finance Bill).

Wakati kikao kikitarajiwa kuanza, tayari serikali ya Zanzibar imeshatangaza mwelekeo wa bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ambapo itatumia shilingi bilioni 648.9 kwa fedha za maendeleo na kazi za kawaida.

Wakati huo huo, Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwasilishwa lengo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.

2 comments:

  1. Kumbe inawezakana! Ni vema basi sheria nyingine zilizotungwa na bunge la Muungano au lile la Afrika Mashariki ziwasilishwe barazania ili matumizi yale hapa Zanzibar yakubalike, kisheria. Sheria ya Income Tax ya mwaka 2004 and ile ya Forodha ya mwaka 2004 ni baadhi ya sheria kama hizo.

    ReplyDelete
  2. Na sielewi hizo sheria zikipelekwa BLW kama zitajadiliwa au zitapitishwa tu manake Z'bar tumeamua Wawakilishi wetu wawe wale wenye elimu ndogo.

    Sidhani kama Jussa peke yake ataweza kujadili na kuchambua kila kitu.
    Waliobaki wawe wanapiga meza tu kuonesha kukubali.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.