Habari za Punde

Masheha, Madiwani Waahidi Kubadilika

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                              27.6.2012
  

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

MADIWANI, Masheha na viongozi wa Halmashauri za Unguja,  wameahidi kubadilika katika utendaji wa kazi zao ikiwa ni kufuata kauli mbiu ya semina waliotayarishiwa juu ya  kuimarisha uhusiano kati ya viongozi wa kisiasa na kiutendaji katika serikali za Mitaa huku wakiwataka wananchi nao kubadilika hasa katika suala la usafi wa mji na mazingira.
 
Viongozi hao waliyasema hayo katika maelezo yao ya michango waliyokuwa wakiitoa kutokana na mada kadhaa zilizowasilishwa katika semina ya siku mbili iliyofanyika  huko katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya mji wa Zanzibar yenye kauli mbiu isemayo ‘viongozi lazima tubadilike’.
 
Katika maelezo yao viongozi hao walieleza kuwa umefika wakati wa kubadilika na kwenda sambamba na kaulimbiu ya semina hiyo huku wakitoa pongezi zao kwa elimu waliyoipata kutokana na semina hiyo iliyotayarishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Aidha, viongozi hao walieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo mashirikiano ya pamoja kati yao na wananchi katika suala zima la usafi wa mji pamoja na uhifadhi wa mazingira.
 
Viongozi hao walieleza kuwa licha ya changamoto kadhaa wanazozipata katika kazi zao lakini bado wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
 
Walieleza kuwa kutokana na hali hiyo wanaomba mashirikiano zaidi na taasisi husika zikiwemo Idara za Serikali ikwa ni pamoja na kutatua migogoro kadhaa inayojitokeza katika maeneo yao.
 
Viongozi hao walieleza kuwa kupatiwa elimu hiyo imedhihirisha wazi kuwa wao wamekuwa ni sehemu umuhimu katika jamii hali ambayo itawahamasisha katika utendaji wao wa kazi.
 
Viongozi hao walieleza haja ya taasisi za Serikali, ikiwemo Idara ya Misitu kuwafanyia semina ndogo ndogo ili waweze kuwapatia elimu zaidi wananchi wakiwemo Madiwani na Masheha  juu ya uhifadhi wa misitu pamoja na mambo mengineyo.
 
Pamoja na hayo, viongozi hao walieleza jinsi wanavyochukua juhudi katika kupambana na matumizi ya misumeno ya moto katika maeneo yao kutokana na kutumika kukata miti ovyo kwa kutumia misumeno hiyo.
 
Kutokana na hali hiyo, viongozi hao wamesisitiza kuwa wananchi nao wana wajibu wa kubadilika katika suala zima la usafi.
 
Pia, viongozi hao walieleza haja ya kuzipitia sheria juu ya ukusanyaji wa mapato kati ya Manispaa na taasisi nyengine kwani kumekuwepo muingiliano kwa mujibu wa maelezo ya viongozi hao katika ukusanyaji wa mapato ya Manispaa ya Mji.
 
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein alisisitiza haja ya viongozi hao kupewa elimu ambayo itawasaidia katika kuimarisha utendaji wa kazi zao.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa semina kama hiyo inatarajiwa kufanyika huko kisiwani Pemba mara baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili viongozi kama hao walioko huko waweze kupata elimu itakayowasaidia katika kutekeleza shughuli zao.
 
Dk. Shein abaye ndie Mwenyekiti wa Semina hiyo, alisisitiza kutofanya kazi kwa mazoea na kueleza matumaini yake makubwa ya kufanyiwa kazi elimu itakayotolewa katika semina hiyo kwa viongozi hao.
 
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa elimu ni suala la lazima hasa katika ukusanyaji wa mapato na kueleza kuwa taasisi zote za ukusanyaji wa mapato hapa nchini zimekuwa zikifanya kazi nzuri katika ukusanyaji wa mapato na kuwataka viongozi hao kutoa ushirikiano wao juu ya hilo.
 
Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa mchango wake katika semina hiyo aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa ardhi inatumiwa vizuri hasa ikizingatiwa kuwa ardhi yenyewe ni ndogo tena ni ardhi ya visiwa.
 
Alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia ardhi bila ya mpangilio mzuri na wamekuwa wakivamia maeneo ya kilimo na kusisitiza kuwa elimu na udhibiti juu ya hali hiyo hairidhishi.
 
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame alisema kuwa semina hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika kutambua Sheria saba za usimamizi wa ardhi na kufahamu kuwa ardhi yote ni mali ya Serikali na usimamizi wake uko chini ya Serikali kwa uangalizi wa Wizara husika.
 
Mapema, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, aliwaeleza viongozi hao kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha malengo ya Dira ya 2020 yanafikiwa kwa mashirikiano ya viongozi hao.
 
Alisema kuwa viongozi ni lazima wawaeleze wananchi juu ya maendeleo ya serikali yao sanjari na hatua zilizofikiwa na kusisitiza haja ya mawasiliano kwa wananchi.
 
Pamoja na hayo, Dk. Abdulhamid aliwataka viongozi hao kutojiingiza katika migogoro ya ardhi na iwapo kutatokea masuala na sheria za  ardhi wawaombe wahusika wa sekta hiyo kulifanyia kazi na sio wao kwa lengola kuepusha matatizo ama migogoro hiyo.
 
Nao watoa mada waliowasilisha mada za katika semina hiyo waliwasisitiza na kuwahamasisha viongozi hao wa Serikali za Mitaa kuhakikisha katika utekelezaji wa kazi zao wanafuata sheria, taratibu, mipango ya maendeleo ya nchi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
 
Mada kumi zinatarajiwa kutolewa katika semina hiyo ikiwemo Hali ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, Umuhimu wa Kufuata Taratibu za Ununuzi na Sheria za Fedha katika Serikali za Mitaa,Wajibu wa Serikali za Mitaa katika Kusimamia Taratibu na Sheria za Ardhi
 
Nyengine ni Wajibu wa Serikali za Mitaa katika Uhifadhi na Uendelezaji wa Maliasili na Utunzaji Mazingira, Wajibu wa Meya, Wenyeviti na Makatibu wa Halmashauri, Madiwani na Masheha katika Uendeshaji wa Serikali, Wajibu wa Serikali za Mitaa katika Kusimamia Utawala Bora, Mawasiliano na Maendeleo katika Serikali za Mitaa na mada nyenginezo.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.