Habari za Punde

Zanzibar Heroes yarejea kishujaa leo. Waziri Mbarouk kuongoza mapokezi. Kurdistan bingwa 'VIVA World Cup'

Na Salum Vuai, Maelezo
KIKOSI cha timu ya Taifa ya soka ya Zanzibar, 'The Zanzibar Heroes', kinatarajiwa kuwasili nchini leo alasiri, huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk akiongoza wananchi mbalimbali kuwalaki katika bandari ya Zanzibar.

Msafara wa timu hiyo iliyoshika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizokuwa wanachama wa Shirikisho la Kimataifa (Fifa), umeondoka jana jioni huko Arbil, kwa ndege ya Shirika la Qatar Airways kupitia Doha, Qatar, na utarajiwa kutua Dar es Salaam asubuhi hii na baadae kupanda boti ya Kilimanjaro saa tatu asubuhi na kuwasili bandarini Zanzibar wakati wa saa tano.

Ofisa Habari wa Chama cha Soka Zanzibar Munir Zakaria, amesema chama chake kilikuwa katika jitihada za kupata kibali cha jeshi la polisi ili baada ya msafara wa timu hiyo kupokelewa, utembee katika manispaa ya mji wa Zanzibar kuwapungia mikono Wazanzibari katika kujipongeza, huku wakishindikizwa na beni maarufu ya mbwakachoka.

Zanzibar Heroes iliichabanga Provence mabao 7-2 katika mchezo wa kutafuta nafasi ya tatu, ambapo kwenye kundi lake B iliongoza kwa kushinda mechi mbili dhidi ya Raetia (6-0) na Tamil Eelam (3-0), kabla kufungwa 2-0 na Cyprus ya Kaskazini katika mchezo wa nusu fainali.

Wakati huo huo, waandaaji wa michuano hiyo Kurdistan, wamefanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuichapa Cyprus ya Kaskazini kwa mabao 2-1 juzi.

Mchezo huo wa fainali ulirindima katika uwanja wa Franso Hariri na kuhudhuriwa na watazamaji 22,000, ambapo wachezaji wa timu zote mbili walionesha ushindani mkubwa na dhamira ya kutoka na ushindi.

Mabao ya washindi katika mchezo huo yakifubngwa na Halgurd katika dakika ya tisa kwa mkwaju wa penelti, pamoja na Siamund aliyezifuania nyavu katika dakika ya 32.

Dakika kumi baadae, makosa yaliyofanywa na walinzi wa Kurdistan, yaliiwezesha Cyprus ya Kaskazini kujipatia bao la kufutia machozi, kutokana na beki mmoja kujifunga

Huo ni ubingwa wa kwanza kwa Kurdistan kwenye michuano hiyo, baada ya mwaka 2009 na 2010, kushika nafasi ya pili mtawalia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.