Na Aboud Mahmoud
ZAKA ni nguzo ya tatu katika nguzo tano za Kiislamu,ambazo kila muislamu hana budi kuifuata nguzo hiyo muhimu katika hizo nguzo tano ikianziwa na kutoa shahada,ya pili kuswali swala tano,ya tatu kutoa zaka ya nne kufunga Ramadhan na ya tano kwenda Makka kuhijji.
Kila muislamu anahitajika kutoa zaka kwa muda maalum hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan ambapo zaka hiyo hutolewa kwa mwaka mara moja.
Zaka husaidia kumsaidia mwanaadamu kujikimu na maisha magumu yanayomkabili kila siku ambao hawana mahitaji na kupunguza watu wanaoomba omba majiani.
Lakini mbali na zaka,sadaka nayo ni muhimu sana kwa kila muislamu kutoa ambapo sadaka hupewa mtu mwenye uwezo na hata asiekuwa na uwezo kwa lengo la kusaidia waislamu.
Katika hadithi mbali mbali za mitume zimeelezea umuhimu wa sadaka ikiwemo kuwa sadaka husaidia kuponyesha maradhi kama utainuilia sadaka yake.
Pia husaidia siku ya mwisho ‘Yaumul Kiyama’ itamfaa katika hesabu na kumsaidia muislamu katika kujiwekea mazingira mazuri hapa duniani na kesho Akhera.
Katika visiwa vya Zanzibar kumejitokeza kikundi maalum ambacho kimejipanga kutoa msaada wao kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kusaidia wanawake masikini na watoto mayatima.
Kikundi hicho kinachojulikana kwa jina la As salaam Womens Group kinachoundwa na wanawake 15 kwa lengo la kuwasaidia wanawake wa Kizanzibari wenye hali ngumu.
Mwandishi wa makala haya alibahatika kukutana na mmoja wa viongozi wa kikundi hicho Ummulkulthum Abdul-Aziz na kumuelea walipoanzia,walipofikia na malengo ya baadae ya kikundi hicho.
Alisea kuwa kikundi hicho kinaundwa na akina mama 15 wa Kizanzibari akiwemo yeye mwenyewe,Nadrat Jeff,Luna Seif Salim,Yasub Seif Salim,Sabra Abdallah Suleiman,Latifa Hugo,Ajba Abdullah,Salma Batash,Sada Mhoma,Sophy Batash,Zakia Abass,Moza Salum,Wahida Nadir na Liza Abass.
Alisema kuwa wanawake hao walijiunganisha kwa pamoja kwa lengo la kuwasaidia akina mama wa Zanzibar ambao wana hali ngumu ya kimaisha ambao wanahitaji msadaa hasa katika kipindi cha Ramadhan.
“Mimi na wenzangu tuliamua kwa pamoja kuanzisha kikundi ambacho kitasaidia kuaondoshea hali ngumu ya kimaisha wanawake wa Zanzibar hasa katika kipindi hichi cha Ramadhan,”alisema.
Bi Ummi alisema kuwa mara baada ya kuanzisha kikundi hicho waliamua kuandaa chakula maalum cha usiku kilichofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort kwa lengo la kutunisha mfuko huo.
Alisema kuwamara baada ya kufanyika kwa tukio hilo waislamu mbali mbali wa ndani na nje ya Zanzibar walifanikiwa kujitolea katika kuwasaidia waislamu hao katika mambo mbali mbali ikiwemo chakula na pesa.
Alifahamisha kuwa michango mingi ilitolewa usiku huo ambayo inatumika kwa mambo mbali mbali ya kuwasaidia waislamu wa Zanzibar.
“Nashkuru siku tulioandaa chakula cha usiku,tulifanikiwa sana kupata michango kutoka kwa watu mbali mbali waliohudhuria na hata wale ambao hawajahudhuria kwa lengo la kuwasaidia akina mama na watoto wa kiislamu,”alisema.
Alisema kuwa mara baada ya kufanikiwa kupata michango hiyo,kikundi hicho tayari kimeshaaanza kufikisha sadaka hizo kwa waislamu mbali mbali wa Zanzibar kwa mwezi huu wa Ramadhan.
Aidha pia alifahamisha kuwa lengo la kikundi hicho sio kuishia kwa Ramadhani bali kuendelea katika miezi mengine pamoja na Ramadhani zijazo.
“Lengo la kikundi chetu ni kuwasaidia akina mama na mayatima sio kwa Rmadhani hii tu bali kila mwezi na hata Ramadhani nyengine ili waondokane na hali ngumu za kimaisha zinazowakabili,”alifahamisha.
Alifahamisha kuwa kikundi chao hushirikiana na viongozi wa dini ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa sadaka na zaka kwa misngi ya dini ya Kiislamu na kufikia walengwa.
Aidha alisema kuwa matarajio yao ya bade ya kikundi hicho ni kuona kwamba kimefikia malengo makubwa ya kuwaondoa akina mama katika hali ngumu za kimaisha.
“Matarajio ya kikundi chetu ni kuhakikishya kuwa tunafikia malengo ya kuwasaidia wanawake wenzetu katika kuwaondosha katika hali ngumu za kimaisha hasa katika kipindi hichi cha Ramadhan.
Hata hivyo pia walisema kuwa malengo ya kikundi hicho ni kuanisha tovuti ambayo itasaidia kwa watu walionje ya nchi kufahamu malengo yao na kutoa msaada wao.
Hata hivyo Ummulkulthum aliwaomba wafanyabiashara,wananchi mbali mbali wa ndani na nje ya Zanzibar kujitokeza katika kuwasaidia akina mama wenye hali ngumu kimaisha.
Alisema kuwa msaada wao utasaidia kuwaondolea matatizo akina mama hao na kujikwamua kimaisha kupitia kikundi hicho.
Ni faraja iliyoje kwa akina mama wa Kizanzibari ambao sio viongozi wa Kiserikali kuamua kwa moyo mmoja kuwasaidia akina mama wenzao kutokana na hali ngumu walizonazo.
Ni jambo la kuwapongeza wana As-salaam Women Group kutokana na kuandaa na kubuni mpango ambao umesaida kwa kiasi kikubwa kuwaokoa na kuwassaidia mayatima.
Lakini kwa upande wa Serikali msichoke na wala msione tabu kusaidiana kikundi hichi ambacho kinahitaji kuwaletea maendeleo na kuwatoa katika shida zinazowakabili wanawake wenye hali ngumu kimaisha wa Zanzibar.
Lengo na nia mlionayo wana As-Salaam inaonekana wazi kuwa mmo katika kujitolea na kuwasaidia wanawake wenzenu hasa katika Mwezi mtukufu wa Ramadhan
Kwa niaba ya mwandishi wa makala haya na uongozi mzima wa gazeti la Zanzibar Leo unatoa pongezi za dhati kwa kikundi hicho cha akina mama na kuwaombea kwa Mwenyezi mungu Inshaallah awajalie kuwa na moyo huo huo na malipo ya kheri mtakayakuta kesho kwa Allah (S.W).
No comments:
Post a Comment