Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi.Maswali na Michango - Wajumbe

Serikali Iwafikirie Watendaji Gazeti la Zanzibar Leo


Na Husna Mohammed
MWAKILISHI wa kuteuliwa, katika baraza la Wawakilishi Zanzibar, Asha Bakar Makame, aliitaka Serikali kuwafikiria watendaji wa Gazeti la Zanzibar Leo, kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Mwakilishi huyo, alisema hayo wakati akichangia bajeti ya ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2012/2013, katika kikao kinachoendelea mjini hapa.

Alisema kuwa ni vyema Serikali ikawafikiria kwa kina watendaji wa gazeti hilo kwa kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.

"Mimi mwenyewe nilikwenda nikaona utendaji wao, Serikali ipo haja ya kuwaona hawa kwa kuwa kazi zao ni ngumu hivyo zinahitaji kutizamwa kwa jicho la huruma," alisema.

Alisema gazeti hilo, ni la mwanzo kulipata waheshimiwa, lakini utendaji wa kazi zake ni mgumu sana mpaka kufanikisha kutoka gazeti hilo.

Sambamba na hilo, lakini Mwakilishi huyo aliitaka Serikali kufikiria kulichapisha gazeti hilo hapa Zanzibar kwa kuwa linatumia gharama kubwa kuchapisha gazeti hilo huko.

"Jamani tuangalie na hili kwa sababu gazeti hili ni moja tu tena la Serikali, hivyo ipo haja ya kuchaopishwa hapa, na hasa ikizingatiwa sisi ni wa mwanzo kulipata gazeti hili", alisema.


Tutawasaidia Wanaoachana na Dawa za Kulevya- SMZ



Na Oscar Samba, AJTC

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, inakusudia kuwasaidia vijana walioamua kucha madawa ya kulevya, ili waweze kujiendesha wenyewe.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza Rais, Fatma Abdul-habib Fereji, alisema kwa kuwa vijana wameachana na dawa za kulevya kwa hiari yao, hakuna budi Serikali kuwasaidia.

Waziri huyo, alisema Serikali ina kusudia kuwapeleka vijana hao katika vyuo vya amali sambamba na kuwapa mitaji ili waweze kujiendeleza.

"Tutawasaidia wanaocha matumizi ya dawa za kulevya kwakuwawezesha kiuchumi na kuwapeleka kwenye skuli za amali ili waweze kujitegemea na wasirudi tena kwenye matumizi ya dawa hizo haramu," alisema.

Alifahamisha kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga nyumba ya kurekebisha tabia (sober house) kwa watu walioathirika na matumizi ya dawa hizo kwa lengo la kupunguza msongamano kwenye nyumba za kurekebisha tabia wanazoishi sasa ambazo ni za watu binafsi.

Hata hivyo, Fatma aliitaka jamii kutowatenga watumiaji wa dawa hizo hasa kwa wale walioamua kucha kwani kufanya hivyo kunawavunja moyo vijana hao.

"Ni lazima wazazi na walezi kuwa pamoja nao wale walioamua kucha matumizi ya dawa hizo na kuwaona ni sehemu katika jamii hasa ikitiliwa manani kuwa hawakutaka kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo," alisema.

Sambamba na hilo lakini pia aliwataka wazazi kuwaangalia vyema watoto wao ikiwa ni pamoja na kurejesha maadili ya kizanzibari yanayoonekana kutoweka baada ya kuvamiwa na utandawazi unaopelekea watoto kujiingiza katika vitendo viovu ikiwa na hilo la utumiaji wa dawa za kulevya.

Akizungumza kwa niaba ya vijana walioachana na dawa za kulevya, Amina Salum, aliiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa kuwa wao ndio chanzo cha vijana kujitumbulkiza katika matumizi ya dawa hizo.

Aidha alisema ni vyema kwa Serikali, ikabuni mpango maalumu wa kuwachukua vijana wanaotumia na walioachana na dawa hizo kuweka pamoja kwa lengo la kuwapa ushauri nasaha na kuwa tiba ya kuachana na dawa hizo.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika ukumbi wa EACROTANAL, ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ' tujenge jamii yenye afya bila matumizi ya dawa za kulevya'.

Fumba Watakiwa Kushirikiana na Wawekezaji



Na Asya Hassan
WANAKIJIJI wa shehia ya Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja, wametakiwa kushirikiana na wawekezaji waliowekeza kijijini hapo kwa lengo la kuimarisha polisi jamii ili kuondokana na vitendo vya uhalifu.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa polisi jamii Mkoa wa Mjini Magharibi, SP Hamad Nassor Mselem, alipokuwa akizungumza na wananchi, wawekezaji na vikundi vya maendeleo na polisi jamii vya shehia hiyo.

Alisema kuwepo kwa kikundi hicho ni njia mojawapo ya kupunguza na kuondosha vitendo mbalimbali vya uhalifu ambavyo vinapelekea uvunjifu wa amani na kurudisha nyuma maendeleo ya kijiji hicho na serikali kwa ujumla.

Mratibu huyo wa polisi alisema kuwa kijiji cha Fumba kinarasilimali nyingi ambazo zinahitaji ulizi, hivyo kama hawajawa tayari kulinda rasilimali hizo ni wazi kuwa zitatoweka kutokana na baadhi ya wananchi kuharibu na kuziiba rasilimali hizo.

"Kijiji chenu kinarasilimali nyingi ambazo mukizitunza na kuzilinda zitawaongezea kipato cha juu, hivyo kama mkiwa hamutaki kushirikiana katika ulinzi watakuja wenzenu kutoka sehemu nyengine ya mbali kuja kuziharibu na badala yake muendelee kuwa katika hali ya chini ya kipato," alisema.

Hamad, alifahamisha kuwa kijiji hicho pia kinavitega uchumi kama mahoteli ya kitalii ambayo huingia watalii mbalimbali na mali zao hivyo ni vyema kuimarisha ulinzi huo ikiwa ni sehemu mojawapo ya ajira zao na kuweza kuendeleza maendeleo ya maisha yao.

Nae Mkufunzi wa mafunzo ya polisi jamii, Mussa Ayoub Mussa, alisema endepo wananchi hao wataimarisha kikundi cha polisi jamii katika shehia yao wataweza kufanikiwa kama walivyofanikiwa wenzao wa shehia nyengine.

Alisema shehia mbalimbali zimepiga hatua kutokana na kudhibiti vitendo hivyo, jambo ambalo linapelekea kuwa na amani na utulivu katika sehemu hizo.

Mkufunzi huyo aliwataka wananchi hao kushirikiana na wawekezaji hao ili kuweza kutatua baadhi ya matatizo ambayo ni kero kwao.

Kwa upande wa muwekezaji wa hoteli ya Safaribluu, Elena Griplas, alisema kuwa yeye ameweza kusaidia mambo mbalimbali ya kijiji hicho na ataendelea kufanya hivyo wakati uwezo utakaporuhusu.

Alivitaja baadhi ya vitu alivyovisaidia katia kijiji hicho ni umeme, kusomesha baadhi ya vijana, kuwapatia ajira wananchi wa eneo hilo na huduma nyengine za kijamii.

Kwa upande wa sheha wa shehia hiyo, Issa Hassan Shoka, aliwataka wananchi hao kuondoa kasoro zao na badala yake kuwa pamoja katika kuimarisha ulinzi huo kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya shehia yao.

Nae Katibu wa jumuiya ya maendeleo ya Fumba, Khamis Kombo Mahmoud, alisema kijiji hicho kimeweza kupiga hatua kwa baadhi ya maendeleo kutokana na muwekezaji huyo kuwaunga mkono katika baadhi ya huduma za kijamii.

Walimu 60 Kisauni wapigwa msasa ya elimu mjumuisho



Na Madina Issa
WALIMU nchini wametakiwa kuitumia vyema fursa ya mafunzo wanayoyapata kwa lengo la kuwaweka katika mstakabali mzuri wa elimu.

Mkurugenzi wa Idara Elimu ya Maandalizi na Msingi, Uledi Juma Wadi, alisema hayo alipokuwa akifunga mafunzo yaliyowashirikisha walimu 60 wa skuli ya Kisauni Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alisema hivi sasa walimu wamekuwa wakipatiwa mafunzo mbalimbali yanayohusu elimu mjumuisho kwa lengo la kumjenga wanafunzi wenye mahitaji maalum kuwa sawa na wenzake.

Aidha, alisema kuwa elimu inayotolewa kwa walimu pia inaweza hata kumjenga mwalimu kakabiliana na mwanafunzi yoyote kwa kuwa hivi sasa kumekuwa na wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa majumbani bila ya kupelekwa skuli ambapo baadhi ya wazazi na walezi wanahofu ya kudhalilishwa watoto wao.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo, aliitaka jamii kuacha kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum kwani serikali hivi sasa imejipanga kuwakomboa watoto wenye matatizo hayo kupata elimu kama watoto wengine.

Akisoma risala katika hafla hiyo, Mwanaasha Khamis Juma, ambae ni miongoni mwa walimu waliopata mafunzo hayo alisema wamefurahishwa na mafunzo waliyopatiwa kwani hivi sasa wataweza kuwamudu wanafunzi wa aina yoyote wakati wakiwa madarasani.

Aidha, aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iendelee na utaratibu wa kuwapatia mafunzo walimu mbalimbali kwani kufanya hivyo, kutaweza kusaidia kuondokana na usumbufu watoto wenye mahitaji maalum.

Sambamba na hilo, walimu hao waliiomba wizara hiyo kuwapatia vifaa ambavyo watakabiliana na wanafunzi wanaohitaji mahitaji maalum katika skuli zenye watoto hao..

Mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuwasomesha watoto wenye mahitaji maalum yalikuwa ya siku nne ambapo yamewashirikisha walimu 60 kutoka skuli ya Kisauni.


NGOs Kufanyiwa Marekebisho ya Kisera



Na Mwanajuma Mmanga
WIZARA ya Katiba na Sheria Zanzibar, kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (AU) inakusudia kufanya marekebisho ya sera za taasisi za serikali na zisizo za serikali ya mwaka 2009.

Akizungumza katika kikao cha kujadili Rasimu ya pili ya msaada wa sheria ya NGO Mtaalamu mwelekezi wa sheria kutoka Arusha Francis Kiwanga alisema NGOs yoyote itakayojisajili ni lazima ifuate sheria iliyopo hivi sasa na ihakikishe kuwa inaendana na mabadiliko ya sera ya NGOs iliyopo.

Alisema NGOs yoyote ihakikishe inapata barua ya usajili kutoka kwa Mrajisi mkuu wa Serikali kwa lengo la kutambulika kisheria.

Alifahamisha kuwa ni vyema kwa NGOs zote kutoka katika mfumo wa Analojia na kuingia mfumo wa Dijital ili kuhifadhi taarifa zao wenye kompyuta kwa kufuata utaratibu wa kisasa unaokwenda na wakati wa Sayansi na Teknologia.

Aidha akifafanua kuhusu NGOs hizo, mtaalamu huyo, alisema zitaangaliwa kwa ukamilifu katika kusimamia, kutathmini taarifa ya utendaji wa kazi zao kwa mwaka ikiwa ni pamoja na vianzio vyake vya mapato.

Alisema pia umoja huo utaanzisha mtandao kwa ajili ya mawasiliano utakaotumia lugha ya Kiswahili na kiengereza kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata taarifa kwa njia moja ama nyengine.

Katika mjadala huo pia ilijadiliwa sheria ya NGOs,uundwaji wa Taasisi pamoja na utaratibu wa usajili wa NGOs mbali mbali ambazo zinafanya kazi chini ya usimamizi wa sheria maalum.

Nae Mtaalamum wa jumuiya za kiraia kutoka Asasi za kiraia ya nchi za Ulaya DR. Adam Novak alisema kwamba hatua iliyofikia hivi sasa ni kwamba tayari rasimu ya pili yga sheria na mpango wa utekelezaji wa sera umeshatayarishwa baada ya kuzingatiwa michango iliyotolewa na wadau mbali mbali hapo awali.

Alisema ni lazima kuwepo na muandalizi maalum ambayo yatatathmini kazi zote na atashughulikia shughuli zote za mashirika ya kijamii.

Kwa upande wa Afisa wa Jumuiya zisizo za kiserikali kutoka katiba na sheria alisema lengo la mkutano huo ni kujadili sheria mpya ya jumuiya hizo juu ya utekelezaji wa sera ya mwaka 2009.

Alisema kutokana na jumuiya nyingi haziunganishwi na kuziratibiwa NGO'S zote ziweze kufanya kazi kwani inaonesha jumuiya hizo zinaonesha hazina maendeleo yoyote yanayopatikana.

Hata hivyo, Wizara ya Katiba na sheria imombioni katika mchakato wa kuziunda sheria mpya pamoja na kuziunganisha njia madhubuti ili ziweze kurekebishika kasoro zinazojitokeza kwa wananchi.


TCRA Yatakiwa Kukemea Kampuni za Simu Zisizofuata Sheria

Na Raya Khatib
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inatakiwa kuhakikisha huduma inazozitoa zinafuata kanuni na sheria.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Abdalla Mwinyi Khamis, alisema hayo wakati akifungua semina juu ya haki na wajibu na watumiaji wa huduma za mawasiliano, huko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kuna kero za muda mrefu zinazotokana na huduma za mawasiliano ikiwemo kutumiwa mijumbe isiyofaa , kukosekana kwa kwa huduma kwa baadhi ya maeneo pamoja na matatizo mengin

"Kampuni nyingi za mawasiliano hasa za simu zimekuwa zikilalamikiwa na wateja wao kutokana na kutojali huduma wanazozitoa," alisema.

.Hivyo, alisema imefika wakati kuona kila mwananchi anafaidika na huduma hizo katika sekta za mawasiliano nchini.

Naye Mkurugenzi wa huduma za Mawasiliano kutoka TCRA, Richard Kayombo, alisema ni kweli watumiaji wa huduma hizo wanapaswa kuelewa usalama wa huduma zao pamoja na kujua haki zao.

Sambamba na hilo, Mkurugenzi huyo aliahidi kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka husika kwa lengo la kufanyiwa kazi malalamiko yanayotoka kwa wateja wa simu za mikononi.

Semina hiyo iliyoandaliwa na mamlaka ya mawasiliano Tanzania, ambayo iliwashirikisha wakuu wa Wilaya, watendaji wakuu wa mkoa wa kusini, masheha na madiwani wa mkoa huo.


'Wafichuliwe wanaowatumikisha watoto wadogo'



Na Laylat Khalfan

WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuwafundisha watoto wao haki na sheria zinazohusu masuala ya utumikishwaji mbaya wa watoto ikiwa ni hatua ya kufikia malengo ya kupiga vita tatizo hilo katika jamii.

Akizungumza katika mafunzo ya haki na sheria, Afisa Wanawake na Watoto Aza Yussuf Ameir, Mwera Wilaya ya Magharibi Unguja, juu ya suala zima la udhalilishaji wa watoto kutoka Mikoa na Wilaya za Unguja.

Alisema kuwa endapo wazazi na walezi wataonesha ari juu ya suala zima la kuwadhibiti watoto majumbani kwa kiasi kikubwa kutapelekea kutozurura ovyo mitaani.

Alifahamisha kuwa hali hiyo itapelekea watoto hao kuwa na muamko mzuri wa kielimu na kuachana na tabia ya kutumikishwa ovyo mitaani.

Afisa huyo, alisema kuwa watoto ndio tegemeo kubwa la maendeleo ya taifa la baadae, hivyo wazazi wana wajibu wa kuwatunza na kuwatetea kunapotokea vitendo vya kudhalilishwa na kunyanyaswa ndani ya jamii.

"Wazazi muwe na muamko wa kuwatunza watoto pamoja na kuwalinda zaidi ili kutokomeza kabisa tabia mbaya ya kuwatuma watoto kiholela jambo ambalo ni kinyume na sheria kwa watoto wetu," alisema Aza.

Nae Afisa wa Wilaya hiyo, Zuhura Abdalla Aliy, aliitaka jamii hasa wazazi kuacha kuwatumikisha watoto kwani kufanya hivyo kunawakosesha haki zao za kielimu jambo ambalo linapelekea ongezeko la watoto wa mitaani.

Zuhura alitoa wito kwa watoto hao kuwa na ujasiri wa kuwabainisha wazazi na walezi wanaowafanyia vitendo viovu ili kuchukuliwa hatua za kisheria.


Watendaji Serikalini watakiwa kutathmini kazi zao



Na Fatma Omar Wkuu
WIZARA ya kazi, Uwezeshaji, Wananchi, Kiuchumi na ushirika, imewataka watendaji wa serikali kutumia mfumo maalum wa ufatiliaji na tathmini katika kazi zao ili waweze kutambua utendaji wao.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Ali Abdalla, alisema hayo alipokuwa akifungua warsha ya kuandaa mfumo wa ufatiliaji unaohusiana na tathmini, katika ukumbi wa umoja wa Watu wenye Ulemavu Kikwajuni mjini Zanzibar.

Alisema endapo mfumo wa ufatiliaji utatekelezwa ipasavyo wataweza kujipima na kujuwa utendaji wao wa kazi unavyoendea katika harakati zao za kila siku.

Katibu mkuu huyo, alifahamisha kuwa ni umuhimu kuangalia maswala mtambuka kwani yanachangia kuleta maendeleo katika shughuli mbali mbali ambazo zinaweza kuwakomboa wananchi.

Aidha wizara yake imo katika mpango wa kuwaandaa sera na rasimu ambazo zitashughulikia masuala tofauti ya wizara yake.

Mapema Mkurugenzi Mipango sera na utafiti, Radhiya Rashid, alisema lengo la kutaarisha mafunzo hayo ni kuona mfumo wa ufatiliaji na tathmini utawezesha wizara yake kufatilia utekelezaji wa shughuli zake.

Sambamba na hilo lakini alitoa wito kwa washiriki kuwa makini katika kutoa michango madhubuti na kuangalia mafanikio na changamoto zitakazojitokeza ili zifanyiwe kazi kwa lengo la kuleta mafanikio katika kutekeleza majukumu ya wizara.

Nao washiriki wa warsha hiyo walisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu katika kuleta maendeleo ya kazi zao pamoja na kuwa ni balozi wazuri kwa wenzao.

Walisema kuwa wanatarajia kupanga mipango ya baadae ambapo kwa kila idara imeweza kuweka viashiria vyake ambavyo vitakuwa na uwezo wa kufanyiwa kazi .

Warsha hiyo imewashirikisha watendaji kutoka sehemu tofauti za serikali na zisizo za kiserikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.