Na Ramadhan Makame
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, amekiri kuwepo kwa tatizo kubwa la mikataba ya ovyo kwa wafanyakazi wa sekta binafsi hasa kwenye hoteli za kitalii na kampuni.
Waziri Haroun alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa ajibu hoja za wajumbe wa Baraza hilo, kabla ya kupitisha vifungu vya matumizi vya bajeti yake kwa mwaka 2012/2013.
Alisema anasikitishwa sana kuwepo tatizo hilo, na kumtia uchungu kuona vijana wa Kizanzibari wanaofanya kazi katika hoteli na baadhi ya kampuni kuwa hawatendewi haki.
“Nakubali suali la mikataba mibovu lipo na limekuwa tatizo kubwa, lakini nakuombeni nipeni muda zaidi kulitatua”,alisema waziri huyo.
Waziri huyo alisema kama wapo wafanyakazi ambao wanahisi haki zao zinavunjwa na wanapigwa danadana na watendaji, wasisite kufika ofisini kwake na kuonana naye ili juhudi za kupatiwa haki zao zifanyike.
Akizungumzia juu ya mkataba na nchi ya Qatar ambao unaonekana kuvamiwa na upande wa pili wa muungano, waziri huyo, alisema Zanzibar inahitaji mkataba na sio ule ulioletwa na wizara ya Mambo ya Nchi za Nje unaotaka maoni ya Zanzibar.
Alisema suala la kazi si la muungano na kwamba Zanzibar inahitaji kusimama yenyewe pamoja na kwamba ingependa kufanya mambo yake kwa mashirikiano na upande wa pili wa muungano.
“Nina uchungu na nchi hii, tusionekane juhudi hazifanyiki hayo ndiyo tunayoyafanya kuhakikisha wazanzibari wanapata haki zao”,alisema waziri huyo.
Akizungumzia suala la harufu ya rushwa ambalo lilihusishwa wizarani kwake, alisema katika maisha yake hajawahi kuomba kitu hicho na kama yupo mtendaji mteuliwa wa Rais apewe jina ili amuandikie barua Rais kumuomba kumuondoa mtendaji huyo.
Alisema kama yupo mfanyakazi ambaye yuko chini ya mamlaka ya wizara, apelekewe jina ili kesho ampumzishe kazi kwani mla rushwa hafai na hana nafasi katika wizara yake.
Akizungumzia nafasi za ajira za Wazanzibari katika hoteli za kitalii alisema kwa kiasi fulani tatizo hilo limepungua, lakini bado kuna tatizo kubwa la wafanyakazi wa Kizanzibari kuomba dharura.
Awali akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake (CCM), Asha Bakari Makame alimtaka waziri wa wizara hiyo kusimamia vyema mikataba ya ajira katika hoteli za kitalii kwani kuna malalamiko kadhaa juu ya mikataba.
Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani (CCM), Ali Salum Haji, alisema kuwa kama kuna tatizo la sheria lirekebishwe ili wawekezaji katika sekta binafsi waweze kutoa nafasi zaidi za ajira kwa vijana wa Kizanzibari.
Mwakilishi huyo alipendekeza kuwa wananchi wanaopatiwa mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi yao wapatiwe elimu kwanza ili miradi ya wananchi hao endelevu hali itakayowawezesha kumudu kulipa deni la mkopo.
Naye Panya Ali Abdalla, aliwataka akinamama wanaopatiwa mikopo kuifanyia biashara ili waondokane na umasikini kuliko kuendekeza maandalizi ya chai za harusi, kwani sio malengo ya mikopo hiyo.
Naye Kazija Khamis Kona, alisema fedha za mikopo zinazotolewa kwenye vikundi vya ujasiriamali bado hazijatosheleza, huku tatizo jengine linaloviandama vikundi hivyo ni kutokuwa na elimu ya kutosha.
Alisema vikundi vya uzalishaji hasa wafugaji wa kuku wamekumbwa na tatizo la soko hasa kuwepo kwa kuku wa biashara wanaoingizwa kutoka nje.
No comments:
Post a Comment