Habari za Punde

Vita dawa za kulevya endelevu – Waziri


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Fatma Abdulhabib Ferej amesema serikali haitarudi nyuma katika juhudi za kupambana na tatizo la dawa za kulevya.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akijibu suali la Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, aliyetaka kujua sababu za serikali kurudi nyuma katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Waziri huyo alisema serikali haitorudi nyuma kwenye vita hivyo hasa ikizingatiwa kuwa dawa za kulevya ni janga lisilo na mipaka na linaathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.


“Juhudi zinaendelea na zipo kesi kadhaa zimekamatwa katika kipindi hichi. Katika mwaka 2010 kuanzia Novemba hadi Disemba ni kesi 67 zilizokamatwa na Januari 2011 hadi Juni 2011 ni kesi 168 na kuanzia Julai 2011hadi Juni 2012 ni kesi 104”,alisema waziri huyo.

Waziri huyo alibainisha kuwa katika kupambana na ndawa za kulevya visiwani hapa, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alikutana na wadau mbali mbali wanaohusika katika kudhibiti dawa za kulevya ili kupata maoni yao juu ya namna ua udhibiti wa dawa hizo.

Waziri Fatma alisema wizara yake iliandaa kikosi kazi kulichojumuisha taasisi mbali mbali za dola zenye kuhusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kuandaa ‘road map’ ya utekelezaji wa sheria za dawa za kulevya.

“Naomba mjumbe pamoja na wawakilishi kwa ujumla wa Baraza lako tukufu kuwa na subira kwa kipindi ambacho mchakato wa ukamilishaji wa ‘road map’ hiyo ukiendelea”, alisema waziri huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.