Habari za Punde

Wasudan Wakaribishwa Zanzibar Kuwekeza


Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } Bibi Mwatum Khamis Othman akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Bibi Mwatum aliambatana na Viongozi Waandamizi wa Chama hicho kufikisha baadhi ya Kero zinazowakwaza Wafanayakazi wa Chama hicho katika maeneo yao ya Kazi.

Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Nchini Jamuhuri ya Sudan { Giad Industrial Group } ukifuatilia maelezo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi walipokutana Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Ujumbe huo uliongozwa na Balozi wa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed Ali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Viwanda ya Jamuhuri ya Sudan { Giad Industrial Group } Ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar. Kulia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ni Balozi wa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed Ali.

Na Othman Khamis Ame

Wawekezaji wa Jamuhuri ya Sudan wameombwa kuangalia vyema mazingira ya Zanzibar katika dhana nzima ya kuwekeza Vitega Uchumi vyao vinakavyosaidia kushajiisha Uchumi wa Pande hizo mbili. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo hapo Ofisini kwake Vuga wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Jumuiya inayojishughulisha na Viwanda Nchini Sudan ya { Giad Industrial Group } ukiongozwa na Balozi was Sudan Nchini Tanzania Dr.Yassir Mohammed Ali. 

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuimarisha Uchumi wake kupitia Sekta Tofauti ikiwemo ile yaViwanda kwa kukaribisha Makampuni, Mashirika na Taasisi hisani. 


Aliiomba Jumuiya hiyo ya Giad Industrial Group ya Sudan ambayo imeshiriki na kupata ushindi katika maonyesho ya saba saba Mjini Dar es salaam kujipanga vyema kuleta maombi yake ili ipate fursa ya kuwekeza hapa Zanzibar. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali itakuwa tayari kuipa mashirikiano Taasisi hiyo muhimu ambayo uzalishaji wa bidhaa zake ambazo ni pamoja na fanicha unahitajika sana Nchini. “ Zanzibar inahitaji takriban Madeski 25,000 katika Skuli zake Unguja na Pemba ili kuondosha tatizo la vikalio kwa Wanafunzi wake. Hivyo kitendo cha Jumuiya hiyo kuanzisha Tawi lake kunaweza kutatua kadhia hiyo”.

 Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi. Mapema Balozi waa Jamuhuri ya Sudan Nchini Tanzania Dr. Yassir Mohammed Ali alisema Ujumbe wa Jumuiya hiyo upo Zanzibar kuangalia uwezekano wa kuja kuwekeza Vitega Uchumi vyao Nchini. Balozi Yassir alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Uhusiano uliopo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Sudan ikiwemo Zanzibar kwa ujumla utaendelea kuimarishwa kwa ustawi wa Jamii za pande zote mbili. 

Ujumbe huo tayari umeshaahidi kufanya maandalizi ya kuandaa maombi ya namna ya kuja kuwekeza Miradi yao hapa Zanzibar ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja. Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi amekutana na Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Habari na Utafiti { RAAWUZ } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 

Katika Mazunguimzo yao Katibu Mkuu wa Chama hicho cha Raawuz Bibi Mwatum Khamis Othman alisema suala la ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika Bodi na Kamati za Uongozi ndani ya Taasisi za Kazi umesahauliwa kwa kipindi kirefu sasa. 

Bibi Mwatum alifahamisha kwamba endapo Uongozi katika sehemu za Kazi ungekuwa ukiitumia vyema ile sheria nambari 10 ya Kamati za Uongozi Makazini kusingekuwa na malalamiko mengi katika sehemu za Kazi. Katibu mikuu huyo wa Chama cha RAAWUZ alivitaja vyuo viwili tu vya Maendeleo ya Utalii Maruhubi na Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka ndivyo pekee vyenye uwakilishi wa Wafanyakazi katika Kamati za Uongozi wao. 

Bibi Mwatum na Ujumbe wake pia walizungumzia masuala kadhaa yanayowakabili watendaji wa Taasisi za Kazi ikiwemo ukosefu wa uangalizi wa afya wakiwa kazini,mishahara duni kwa wafanyakazi wazoefu pamoja na bakaa ya fedha za Mishahara kwa wafanayakazi waliokatwa mishahara yao wakati wa zoezi la mabadiliko ya mishahara. 

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja hizo Makamu wa Pili wa Raisn wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliahidi kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Wafanyakazi katika Taasisi za kazi ili kuimarisha ufanisi wa Kazi. 

Balozi Seif alisema atahakikisha anaziandikia Taasisi zote katika kuona ushiriki wa Wafanyakazi unapatikana vyema . Aliueleza Ujumbe huo kwamba suala la Wafanyakazi wazoefu litaangaliwa kutokana na mchango wao wa muda mrefu katika Taifa hili pamoja na kusisitiza kuandaliwa utaratibu kwa wafanyakazi kupimwa afya zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.