Habari za Punde

Maalim Seif aendelea na ziara zake kuwatembelea wazee na wagonjwa

Bi Fatma bint Baraka maarufu Bi Kidude akisisitiza kwamba yeye ni mzima hasa kwa wale waliojaribu kumzushia kwamba amefariki ila miguu ndiyo inamsumbua kwa sasa.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akimfariji msanii mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Bi. Fatma Baraka Khamis maarufu Bi. Kidude wakati alipomtembelea nyumbani kwa mwanae anakojiuguza maradhi ya miguu, huko Kihinani, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Makamu wea Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiomba dua pamoja na msaniii mkongwe wa muziki wa Taarab nchini Bi Fatma bint Baraka alipomtembelea. (Picha na Salmin Said OMKR

Khamis Haji, OMKR             


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefanya ziara ya kuwatembelea wagonjwa na wazee kwa ajili ya kuwapa pole na kuwafariji katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Miongoni mwa wagonjwa waliotembelea na Maalim Seif ni msanii maarufu hapa Zanzibar, Bi. Fatma binti Baraka maarufu Bi. Kidude ambaye anasumbuliwa na maradhi ya miguu kwa wiki kadhaa sasa.

Bi. Kidude akizungumza na Maalim Seif huko nyumbani kwa mwanawe Kihinani, Wilaya ya Magharibi Unguja, alimueleza kuwa anasumbuliwa na maradhi ya miguu, lakini amekuwa akifanya shughuli zake nyingi za kawaida.

Hata hivyo, Bi. Kidude alisema amesikitishwa sana na kitendo cha baadhi ya watu kueneza uvumi kwamba amefariki wakati bado ni mzima na anafanya shughuli zake kama kawaida.

Alimueleza Maalim Seif kuwa kitendo cha watu hao licha ya kumsikitisha yeye binafsi, pia kimesababisha usumbufu na hofu kubwa miongoni mwa jamii na baadhi ya watu ambao walilazimika kufunga safari kuja Zanzibar kutoka nchi mbali mbali. “Kuna watu wameeneza taarifa za uongo kwamba nimekufa, wapo watu waliofunga safari kutoka nchi tafauti kuja Zanzibar, lakini walipofika walishangaa kuniona nipo hai”, alisema Msanii huyo maarufu wa muziki wa taarab hapa Zanzibar na Afrika Mashariki.

Katika ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuwatembelea wagonjwa na watu wazima iliyoanza juzi, pia aliwafariji, Mzee Khamis Makungu wa kijiji cha Ndijani, Mzee Abdulrazak Mukri wa Mkunazini, Mzee Ali Haji Pandu wa Mpendae na Sheikh Habib Ali Kombo wa Kiembesamaki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.