Na Haji Mtumwa
MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Awena Seif Sharif, amewahimiza wazazi na walezi wa wanafunzi kuhakikisha wanawapatia elimu yenye manufaa watoto jambo ambalo litawanufaisha duniani na akhera.
Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kuwanasua wanafunzi hao katika hali ya kuondokana na mambo ya wigo yakiwemo ya kujiingiza katika vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya.
Mama Awema aliyasema hayo baada ya kukabidhi zawadi kwa wanafunzi walioshinda katika mashindano ya kuhifadhi kur-ann, yaliyofanyika katika Itiqaf ya kimataifa inayoendelea katika msikiti wa Amani kwa Saidi washoto.
Aliwataka wazazi hao kutambua kuwa wana dhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu katika kuhakikisha kuwa thamani ya watoto wao inakuwa kwa hali ya juu kutokana na watoto hao ndio tegemeo kubwa katika familia zao pamoja na taifa kwa ujumla.
"Ni vyema wazazi mkajitahidi katika kuwalea watoto wenu katika misingi imara ili watoto hao wasijepoteza silka na utamaduni wa dini yao, huku mkitambua kutofanya hivyo mtakuwa na dhima kubwa juu yenu", alisema Awema.
Alifahamisha kuwa kukosena kwa silka na utamaduni wa kiislamu hasa kwa watoto ndio changamoto kubwa kwa watoto hao kujiingiza katika madimbwi ya vitendo viovu.
Alisema aliwashauri walimu wa wanafunzi hao na wengine kudumu kufanya kazi yao hiyo ya ufundishaji ili kuwawezesha kuondokana na dhana mbaya ya kujiingiza katika makundi maovu pamoja na kujijengea sifa katika dini.
Kwa upande wake Naibu Mwenyeki wa Itiqaf hiyo ya kimataifa, Tahir Khatib Tahiri aliwaomba waislamu popote walipo kujitokeza kwa wingi katika kuchangia harakati za Ibada hiyo.
Alisema kuna kasoro ndogo ndogo ambazo bado hazikukamilka ikiwemo ukosefu wa fedha, maji, sukari pamoja na vyakula vyengine mbali mbali ambavyo hutumika katika kufutarishia.
Hivyo alisema kuwa kwa yoyote yule alikuwa yuko tayari kusaidi Ibada hiyo afike katika Msikiti wao uliopo Amani kwa Saidi washoto Wilaya ya Magharibi Unguja na kuonana na uongozi wa Itiqaf hiyo kwa hatua zaidi.
Katika mashindano hayo kwa upande wa wanafunzi wanawake kwa juzuu 15 mshindi kwa kwanza alikuwa ni Siti Simai, kutoka Pemba aliyepata alama 95, na kuzawadiwa Televisheni ya rangi nchi 16.
Mshindi wa pili alikuwa ni Maryam Saidi kutoka Uganda aliyepata alama 94, na kuzawadiwa televisheni ya rangi ya nchi 14, ambapo mshindi wa tatu alikuwa ni Safia Nassor kutoka Burundi aliyepata alama 90, na kuzawadiwa pasi ya umeme.
Nafasi ya nne alikuwa ni Fatma Kombo kutoka Tanzania bara aliyepata alama 89.5 na kuzawadiwa jiko la umeme aina ya Rice cooker, na mshindi wa tano alikuwa Maryam Hamad kutoka Unguja, aliyepata alama 88, na kuzawadiwa seti ya sahani za vigae.
Kwa upande wa wanaume Maudhi Ahmada alikuwa mshindi kwa kwanza kwa kupata alama 96, na kuzawadiwa televisheni ya rangi ya nchi 21, ambapo Hamza Siraji kutoka Uganda alikuwa mshindi wa pili kwa kupata alama 88.5, na kuzawadiwa televisheni ya rangi ya nchi 20.
Mshindi wa tatu alikuwa ni Ayoub Muhammed kutoka Tanzania bara aliyepata alama 88,na kuzawadiwa pasi ya umeme, Babib Hussein kutoka Kenya likuwa ni mshindi wa nne kwa kupata alama 84.5, na kuzawadiwa Blender na Nshimi Yamana kutoka Burundi alikuwa ni mshindi wa tano na kuzwadiwa seti ya vikombe vya chai.
Itiqaf hiyo ya kimataifa hufanyika kila ifikapo mwezi ishirini wa mfungo wa Ramadhan, katika Msikiti wa Saidi washoto wilaya ya Magharibi Unguja na humalizika asubuhi ya Sikukuu ya Idd el Fitri.
No comments:
Post a Comment