Na Salum Vuai, Maelezo
KAMATI Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeridhia uteuzi uliofanywa na Rais wa chama hicho Amani Ibrahim Makungu, kuteua wajumbe wanne kuingia kwenye kamati hiyo kwa uwezo aliopewa katika kifungu namba 31 (l) cha katiba.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, mjumbe wajke Hafidh Ali Tahir, amewataja wajumbe hao wapya kuwa ni Suleiman Mahmoud Jabir, Juma Abdallah Mohammed kwa upande wa Unguja, Salum Msabah na Omar Ahmed Awadh kwa Pemba.
Tahir amesema katiba ya ZFA inampa uwezo Rais kuteua wajumbe wanne kuingia kwenye kamati tendaji ya chama hicho wakati akiwa madarakani akiona iko haja ya kufanya hivyo.
Akimkariri Rais wa chama hicho, Tahir aliwashukuru baadhi ya wajumbe waliokuwemo kwenye kamati hiyo kwa uteuzi kama huo ambao ulifanywa na Rais aliyejiuzulu Ali Ferej Tamim.
Katika hatua nyengine, Tahir alieleza kuwa, nafasi ya Katibu Mkuu wa ZFA taifa Kassim Haji Salum, sasa inakaimiwa na Suleiman Mahmoud Jabir, baada ya Katibu huyo kuomba ruhusa ya kwenda kusoma.
Alieleza kuwa, Haji ameamua kuongeza taaluma ya kompyuta ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli za kiofisi zinahitaji upeo mkubwa wa kompyuta kwa ajili ya Mawasiliano na taasisi na washirika mbalimbali wa chama hicho.
“Wapo watu wanaodai kuwa Katibu wa ZFA amefukuzwa, hilo si kweli, ndugu Kassim ameomba ruhusa ya kuhudhuria mafunzo ili kuongeza ujuzi, na chama kimemruhusu na ndicho kinachomlipia, wakati wowote akiwa tayari nafasi yake ipo, ila kwa sasa inakaimiwa na ndugu Suleiman”, alifafanua Tahir.
No comments:
Post a Comment