Na Othman Khamis, OMPR
SERIKALI ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Wizara ya Afya ya
Nchi hiyo imethibitisha kuendelea kushirikiana na Mataifa rafiki ya Bara la
Afrika katika mikakati yake ya kuwapatia huduma bora za Afya Wananchi wa
Mataifa hayo Rafiki.
Kauli hiyo imetolewa na na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa
wa Jamhuri ya Watu wa China, Feng Yong wakati akizungumza na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
Feng Yong aliyeambatana na
Ujumbe wa madaktari na wafanyakazi 14 wa Wizara ya Afya ya China ambao wapo nchini
kurikodi filamu Maalum ya Miaka 50 ya Maendeleo ya Ushirikiano wa pamoja
wa Sekta ya Afya kati ya China na Afrika, amesema bado jamii ya walio wengi barani
Afrika wanaendelea kukosa huduma za afya hasa vijijini.
Alisema mpango wa nchi hiyo kutoa madaktari bingwa kufanya kazi za
huduma ya Afya katika Mataifa ya afrika ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
utadumishwa na kuzingatiwa zaidi.
Aidha Feng Yong ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi
wake kutokana na ushirikiano wao kwa madaktari Mabingwa wa China wanaofanya
kazi Zanzibar.
“ Tumeshuhudia ushirikiano huo wa karibu uliopo kati ya wananchi
wa Zanzibar na madaktari wetu, hali inayopelekea wengine kuamua kutaka kubakia
nchini kuendelea kutoa huduma”, alisema Fenga Yong.
Akitoa shukrani zake Balozi Seif alisema China imesaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza uhaba wa Madaktari uliopo hapa Zanzibar.
Balozi Seif alisema inapendeza kuona Taifa la China linaendelea
kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika kuwapatia huduma za afya wananchi wake
ukiwemo mpango ulioanzishwa miaka ya nyuma wa Nchi hiyo kutoa fursa za
upendeleo kwa Madaktari bingwa wa Zanzibar kupata taaluma zaidi ya juu nchini China.
“Bahati nzuri mimi mwenyewe binafsi wakati nikiwa Balozi wa
Tanzania Nchini China nimeshuhudia madaktari kadhaa wa Zanzibar niliwapokea nchini
humo walipokwenda kupata mafunzo ya Juu ya Udaktari Bingwa Nchini China”, alifafanua
Balozi Seif.
Balozi Seif aliomba utaratibu huo kama umesita au kupungua ni
vyema ukaendelezwa zaidi ili kutoa fursa ya kuwa na watendaji wa kutosha wa
sekta ya Afya kwa lengo la kuufanikisha mpango wa Zanzibar wa kuwa na Vituo cha
Afya kila baada ya kilomita tano.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tayari imejipanga kuzingatia mpango wa kuwapatia mafunzo ya Afya Wanafunzi
wanaomaliza Elimu ya vyuo vikuu na Diploma utakaokidhi mahitaji ya Sekta hiyo
muhimu kwa ustawi wa jamii nchini.
Aliuhakikishia ujumbe huo wa Madaktari na Watendaji wa Wizara ya
Afya ya Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kuchukuwa jitihada zaidi za kuwapatia huduma nzuri Madaktari
Mabingwa wa China wanaotoa huduma hapa Zanzibar.
Alisema Wananchi walio wengi hapa Zanzibar wameonesha kuendelea
kuridhika pamoja na kufurahia huduma mbali mbali bora za Afya zinazotolewa na Madaktari
bingwa kutoka China.
Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar, Chen
Qiiman ambae aliambatana na Ujumbe huo alieleza kwamba mpango maalum
utaandaliwa kwa baadhi ya Madaktari wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na ile ya
Abdulla Mzee Kisiwani Pemba wa kuwapatia mafunzo nchini China katika dhana ya
kuzijengea uwezo zaidi wa kutoa huduma Hospitali hizo kubwa mbili hapa
Zanzibar.
Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba iko katika hatua za mwisho
za kufanyiwa matengenezo makubwa ya majengo na Vifaa muhimu vya uchunguzi wa
Afya pamoja na vitanda 60 vya kulaza Wagonjwa chini ya ufadhili wa Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China.
No comments:
Post a Comment