Habari za Punde

Dk Shein azungumza na watendaji Wizara ya Kazi, uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika

 Watendaji wa Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi,Kiuchumi na Ushirika, wa Idara mbali mbali wakiwa katika Mkutano na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, katika utekelezaji wa Mpango wa kazi za Wizara hiyo,wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi,Kiuchumi na Ushirika,katika utekelezaji wa
Mpango wa kazi za Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano Ikulu Mjini Zanzibar. [ Picha na Ramadhan Othman,IKULU.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika imepongeza juhudi za maendeleo zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinudizi Dk. Ali Mohamed Shein huku ikieleza hatua ilizozichukua katika kupunguza migogoro kazini kwa kuweka kitengo maalum kinachoshughulikia migogoro ya wafanyakazi nchini.
Maelezo hayo yametolewa leo na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee walishiriki kikamilifu, Wizarav hiyo ilieleza kuwa hatua hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro kadhaa katika sehemu za kazi nchini.
Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Haroun Ali Suleiman alisema kuwa Wizara hiyo ina jukumu la kusimamia na kuratibu program zinazolenga katika kukuza ajira na kunyanyua kipato cha wananchi hasa wale wenye kipato cha chini.
Waziri Haroun aliyataja malengo makuu ya Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza kutanua program za kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuongeza ufanisi katika kuzimamia utekeleza wa sheria za kazi, kuongeza upatikanaji wa fursa za ajira zenye heshima kwa wananchi.
Malengo mengine ni pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Kazini, Sheria Namba 8 ya mwaka 2005, kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa pamoja na utekelezaji na uratibu wa Sera, Mipango na Programu na Kuimarisha uwezo wa Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake.
Sambamba na hayo, Wizara hiyo ilieleza kuwa tayari imeshakutana na uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kujadili juu ya suala la kuanzisha soko la Jumaapili huko kisiwani Pemba.
Aidha, Wizara hiyo imeeleza kuwa imeshafuatilia suala la kuwatafutia shughuli mbadala wananchi wanaojihusisha na kazi ya uchimbaji mawe katika kijiji cha Vitongozi ili kuzuia uharibifu wa mazingira katika eneo hilo ambapo wananchi hao wamehamasishwa kuunda vikundi vya ushirika ambapo jumla ya vyama vya ushirika 29 vimesajiliwa.
Vikundi hivyo vimesajiliwa na vimebuni miradi mbali mbali ikiwemo ya kilimo, uvuvi na biashara.
Wizara hiyo pia, ilieleza kuwa imeshafanya utafiti katika maeneo muhimu ya kiuchumi ili kubaini fursa za uwezeshaji katika maeneo ya sekta za utalii na kilimo. Pia, Wizara hiyo ilieleza azma yake ya kufanya mikutano na Mawizara hasa yenye majengo mapya kwa ajili ya ushauri wa kiusalama katika majengo hayo huku ikienedelea kutoa ushauri huo kwa taasisi nyengine za umma na zile za binafsi.
Pamoja na changamoto zilizojitokeza ikiwemo uhaba wa vitendea kazi, Wizara hiyo imeweza kufanikisha kwa kiasi kikubwa malengo iliyojiwekea kwa kiasi kikubwa na kueleza kuwa Mpango Kazi wa mwaka 2011/2012 umetoa fursa ya kujifunza, kubaini changamoto
Ambapo pia, umeweza kutafakari mbinu mbali mbali za kukabiliana na changamoto zinazohusiana na utekelezaji wa sheria za kazi, ajira, uwezeshaji wananchi kiuchumi na maendeleo ya sekta ya ushirika.
Nae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipongeza juhudi za Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kuwa na Sera ya Uwezeshaji ili iweze kusaidia katika sekta ya uwezeshaji na kuweza kuifaidisha jamii.
Pamoja na mambo mengine Dk. Shein ameitaka Wizara hiyo kueleza mafanikio iliyoyapata hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo imeshafanya mambo mengi ambayo mengine ni muhimu wananchi wayajue na wayafuate kwa ajili ya manufaa yao na maisha yao kwa jumla.
Alisema kuwa elimu juu ya usalama kazini na hata majumbani ni muhimu kutolewa kwa jamii hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo inayo Idara yake ya Usalama na Afya Kazini ambayo imedhamiria kwa makusudi kutoa huduma kwa jamii juu ya usalama wao.
Alieleza kuwa suala la usalama maofisini linatakiwa kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa ipo haja ya Idara hiyo kutoa elimu na pia, kusaidiwa ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa zaidi kutokana na umuhimu wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.