JOHANNESBURG, Afrika Kusini
AFRIKA Kusini imemtaja mchezaji anayekipiga nchini Uholanzi, Thulani Serero, kwenye kikosi kitakachocheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, licha ya kiungo huyo kutocheza tokea Septemba.
Mchezaji huyo ni miongoni mwa nyota saba wanaocheza nje katika kikosi cha wachezaji 23 ambacho kocha Gordon Igesund, alikielezea cha mchanganyiko wa vijana.
Igesund, alisema, alikuwa akifuatilia uzima wa Serero kwa sababu ya uwezo wa kushinda mechi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 anayekipiga na Ajax Amsterdam.
Serero alishiriki katika mechi tatu za kujipima nguvu wiki iliyomalizika jana na kumshawishi kocha kwamba alikuwa yupo fiti kufuatia majeraha ya goti yaliyomuweka nje kwa miezi mitatu.
Wenyeji Afrika Kusini watacheza mechi ya kujipima ubavu dhidi ya Norway Januari 8, na kuivaa Algeria siku nne baadaye kabla ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Cape Verde kwenye dimba la Soccer City mjini Johannesburg Januari 19.
Kikosi kamili cha Bafana Bafana kinaundwa na walinda milango, Itumeleng Khune (Kaizer Chiefs), Senzo Meyiwa (Orlando Pirates) na Wayne Sandilands (Mamelodi Sundowns).
Walinzi ni Siboniso Gaxa (Kaizer Chiefs), Bongani Khumalo (PAOK Salonika, Ugiriki), Tsepo Masilela (Kaizer Chiefs), Thabo Matlaba (Orlando Pirates), Anele Ngcongca (Racing Genk, Ubelgiji), Thabo Nthethe (Bloemfontein Celtic), Siyabonga Sangweni (Orlando Pirates).
Viungo ni Lerato Chabangu (Moroka Swallows), Kagisho Dikgacoi (Crystal Palace, England), Dean Furman (Oldham Athletic, England), Reneilwe Letsholonyane (Kaizer Chiefs), May Mahlangu (Helsingborg, Sweden), Oupa Manyisa (Orlando Pirates), Thuso Phala (Platinum Stars), Thulani Serero (Ajax Amsterdam, Uholanzi), Siphiwe Tshabalala (Kaizer Chiefs) .
Washambuliaji ni pamoja na Lehlohonolo Majoro (Kaizer Chiefs), Katlego Mphela (Mamelodi Sundowns), Tokelo Rantie (Malmo FF, Sweden), Bernard Parker (Kaizer Chiefs). (Reuters).
No comments:
Post a Comment