Habari za Punde

Korea kuigeuza Kibokwa kijiji cha mfano kimaendeleo

Hassan Hamad,OMKR
KOREA ya Kusini inakusudia kukifanya kijiji cha Kibokwa kuwa cha mfano wa maendeleo Tanzania.

Balozi wa Korea Kusini nchini,Jeong Il alieleza hayo katika sherehe za ufunguzi wa jengo la kijiji cha Kibokwa, litakalotumika kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za mikutano, ufundi, kilimo na mifugo.

Balozi Jeong Il alisema inawezekana kwa kijiji hicho kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa mfano wa kuigwa na vijiji vyengine vya Tanzania.

Alifahamisha kuwa Korea ya Kusini ilikuwa nchi maskini kama ilivyo Tanzania, lakini imeinuka kiuchumi baada ya kuamua kuanzisha vijiji vipya na kuviendeleza kama ilivyo kwa kijiji cha Kibokwa.

Alisema maendeleo ya kijiji hicho yatachochea maendeleo ya vijiji vyengine vya Zanzibar, na kuahidi kuanzisha mradi kama huo kisiwani Pemba iwapo mradi huo wa Kibokwa utaonesha mafanikio.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, alisema Korea ya Kusini ni marafiki wa kweli, na kwamba serikali inathamini mchango unaotolewa na Korea kupitia miradi mbali ya maendeleo.

Aliwataka wananchi wa Kibokwa kuuenzi na kuundeleza mradi huo, sambamba na kuendelea kuwapa mashirikiano wataalamu wa Korea walioko nchini, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Alisema kijiji hicho kimepata bahati ya kuanzishiwa mradi huo ambao ni muhimu kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla, na kutaka uhifadhiwe vizuri ili uwe endelevu.

Alisema mradi huo ambao pia unahusisha kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Kibokwa, utasaidia utekelezaji wa kaulimbiu ya serikali katika Mapinduzi ya kilimo, na hatimaye kupunguza utegemezi wa chakula.

Katika risala yao wananchi wa Kibokwa wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao tayari matunda yake yameanza kuonekana.

Risala hiyo imetaja baadhi ya mafanikio yaliyoanza kupatikana kuwa ni pamoja na kupatikana fursa za ajira kwa vijana wa kijiji hicho hasa katika masuala ya ufugaji.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Jimbo la Kyongsang la Korea ya Kusini,Song Pil Kak.

Mradi huo wa miaka mitano unatekelezwa kwa mashirikiano kati ya Mkoa wa Kaskazini wa Korea ya Kusini na Mkoa wa Kaskazini Unguja, unatarajiwa kukamilika mwaka 2015.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Affan Othman Maalim alisema tayari dola milioni 50 zimeshatengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa aina yake kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.