Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakifungua pazia kuashiria makabidhiano ya skuli mpya ya urafiki kati ya nchi hizo mbili iliyopo mtaa wa mwanakwerekwe
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf Balozi Seif Ali Iddi akiangalia moja ya darasa liliomo ndani ya skuli mpya rafiki kati ya china na Zanzibar iliyopo mwanakwerekwe.
Viwanja vya michezo mbali mbali vilivyomo ndani ya eneo la skuli mpya rafiki kati ya china na Zanzibar iliyopo mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna wakitia saini mkataba wa makabidhiano ya skuli mpya rafiki kati ya China na Zanzibar hapo ilipo skuli hiyo mwanakwerekwe
Baadhi ya Maafisa wa Ubalozi Mdogo wa China na familia zao wakishuhudia hafla ya makabidhiano ya skuli mpya rafiki kati ya china na Zanzibar iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya China hapo Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbali mbali waliohudhuria hafla maalum ya makabidhiano ya skuli mpya ya urafiki kati ya China na Zanzibar mara baada ya makabidhiano hayo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ .
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa hatua yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kujiletea maendeleo ya Kiuchumi pamoja na Ustawi wa Jamii.
Shukrani hizo alizitoa wakati wa hafla maalum ya Makabidhiano ya Skuli Mpya ya Kisasa ya Msingi ya Mwanakwerekwe C iliyopewa jina la Skuli Rafiki kati ya China na Zanzibar baada kukamilika ujenzi wake ndani ya kipindi cha miezi saba.
Balozi Seif akifungua rasmi pazia kuashiria makabidhiano hayo kati yake na Balozi Mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar Bibi Chen Qiiman ilikwenda samba na utiaji saini hati na makabidhiano hayo kati ya Balozi Mdogo huyo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar hasa katika sekta ya Elimu ambayo inatoa fursa nzuri kwa wanafunzi wa Zanzibar kujipatia elimu katika mazingira ya kisasa ya sayansi na teknolojia.
Aliwahimiza Wanafunzi kujitahidi kusoma katika viwango vya juu vitakavyokidhi mahitaji hayo ya mabadiliko ya sayansi kwa vile Serikali tayari kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi inaendelea kuwawekea mazingira bora.
“ Ukweli Dunia hivi sasa inaelekea katika sayansi na teknolojia. Hivyo kinachohitajika kwenu ni juhudi zaidi itakayokuwezesheni kuwa na nguvu za ziara za kuingia katika soko la ajira hasa lile la Afrika mashariki “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi kwamba Serikali itaendelea kujenga Skuli nyengine mpya zenye hadhi ya ghorofa ikiwa ni miongoni mwa sera zake ilizoziandaa katika mpango maalum wa matumizi sahihi ya ardhi ndogo iliyopo Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika hotuba yake hiyo alitoa Mkono wa pole kwa Wananchi wa Jimbo la Sichuan Nchini China Kupitia Balozi huyo Mdogo wa China hapa Zanzibar Bibi Chen Qiiman kufuatia kukumbwa na Tetemeko la ardhi lililoleta maafa.
Balozi Seif alisema maafa hayo yaliyosababisha vifo vya wananchi kadhaa wa Jimbo hilo yamefanana na yale yaliyotokea katika Mji wa Shengdu Jimboni humo mwaka 2009 yamewagusa wananchi wa Zanzibar hasa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliopo katika ya China na Zanzibar na hasa Jimbo la Sichuan.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Skuli hiyo mpya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Mwanaidi Saleh alisema ujenzi huo uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya China ya Fujian Engineering Construction umegharimu jumla ya shilingi Bilioni 3.3 ikiwa ni msaada uliotolewa na China.
Bibi Mwanaidi alisema Skuli hiyo mpya ina madarasa 12, Ofisi saba za Walimu, maabara, chumba cha kompyuta, vyumba viwili kwa walimu wanaopatwa na dharura ya maradhi pamoja na viwanja vya michezo.
Naye kwa upande wake Balozi Mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar Bibi Chen Qiiman alisema hatua ya ujenzi huo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo katika ya China na Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla.
Balozi Chen alishukuru ushirikiano walioupata wajenzi wa Skuli hiyo Kampuni ya Fujiani ambao umewawezesha kukamilisha ujenzi wa huo katika kipindi kifupi cha miezi saba tokea kuanza kwa ujenzi wake tarehe 2 mwezi agosti mwaka 2012.
Akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alieleza kwamba misaada ya China kwa Zanzibar itaendelea kuwa kielelezo cha uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili.
Waziri Shamhuna akisisitiza msimamo wa Wizara hiyo kujizatiti katika kuitunza vyema skuli hiyo yenye uwezo wa kutumika katika kipindi cha miaka 50 ijayo alisema kukamilika kwa ujenzi wake kumetoa ishara njema ya kupunguza ufinyu wa madarasa unayoyakumba maskuli mengi Nchini.
Skuli mpya ya Msingi ya Urafiki kati ya China na Zanzibar iliyopo mwanakwerekwe ikitanguliwa na kama hiyo iliyopo Kijichi Wilaya ya Magharibi ina samani kamili katika madarasa yote 12 pamoja na uwezo wa kujitegemea yenyewe kwa huduma za maji safi na salama ikiwa na kisima chake.
No comments:
Post a Comment