Habari za Punde

Sarhan aahidi kuinua michezo Chambani

 
Na Haji Nassor, Pemba
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Chambani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Matar Sarhan Said, amewahakikishia vijana na wapenda michezo kuwa, atawajengea uwanja wa michezo iwapo atachaguliwa.
Pamoja na mambo mengine, Sarhan amesema ana dhamira ya dhati kuimarisha michezo katika jimbo hilo, na ujenzi wa uwanja huo utakuwa hatua muhimu kuwawezesha vijana kuibua na kuendeleza vipaji vyao.
Aidha alisema, atahakikisha anaondoa kasoro zilizopo kwa upande wa sekta ya michezo kwa kuwanunulia vijana vifaa mbalimbali.
Alikuwa akizungumza juzi katika uzinduzi wa kampeni za CCM kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa ubunge kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha mbunge wa zamani marehemu Hemed Salum Khamis, uliofanywa na Mjumbe wa NEC CCM Balozi Seif Ali Iddi katika uwanja wa skuli ya Ukutini.
Aidha alisema, atahakikisha klabu zote za mpira wa miguu na michezo mingine, anazinunulia vifaa, vikiwemo viatu, mipira, jezi, na pia magoli ya kisasa kwa viwanja vya mpira wa miguu.
"Nakuahidini vijana, kama nitakuwa mbunge wenu, mtang’ara kwa vifaa vya michezo, pamoja na kuviimarisha viwanja vyetu michezo", alijigamba Matar.
Alieleza kuwa, jimbo hilo limejaaliwa kuwa na vipaji vizuri lakini vimekuwa vikififia kutokana na kukosa vifaa vya kisasa vya michezo, ikiwa ni pamoja na viwanja.
Hivyo amewaomba wazee, vijana na wananchi wote wa Chambani kumpa ridhaa ili apate wasaa mzuri wa kuimarisha michezo, ambayo alisema imeanza kupotea taratibu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.