Meneja Mwendeshaji Masoko wa New Spitalfields Market, Nigel Shepherd akitoa maelezo kwa Mh. Waziri Mkuu. Kando ni Juma Bozdogan
Mh Waziri Mkuu akiangalia bidhaa mbalimbali ambazo ziko tayari kuuzwa
Mh. Waziri Mkuu akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi wa SACOMA, Sam Ochieng aliyeshika kiazi kikuu toka Ghana
Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na msafara wake wakiondoka eneo la ghala la soko kuelekea mkutanoni. Kulia kwake ni Balozi Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa SACOMA, Sam Ochieng
Perez Ochieng wa SACOMA (aliyeshika matunda ya Cherry) akiwa na Mh Waziri MkuuWaziri Mkuu , Mizengo Pinda akitoa shukrani zake na kuahidi uwezekano wa Tanzania kujitayarisha ipasavyo
Imeandikwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
Ijumaa iliyopita itajulikana kama siku mlango mdogo ila muhimu sana ulipofungua kitasa chake kwa baadhi ya wananchi wanaojituma kikazi na kibiashara Tanzania. Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitembelea soko la mboga na matunda lililoko Leytonstone, mashariki ya London. Matembezi yalidhihirisha mahusiano ya ujirani mwema kati yetu Watanzania na Kenya yenye kampuni iliyoshajijenga ndani ya soko hili maarufu na kubwa sana.
Soko hilo linaloitwa Spitalfields si sehemu inayofahamika na wengi wanaoishi Uingereza licha ya kwamba jina hilo si rahisi kutamka au kuandikwa. Lakini Spitalfields (tamka “Spitol-fildz”), itakua eneo muhimu sana kwa vijana, wakulima na wafanyabiashara Tanzania, miaka ijayo.
Hapa ndipo mboga na matunda toka sehemu mbalimbali duniani huletwa halafu zikasambazwa maduka makubwa ya vyakula Uingereza. Hivyo basi mlango kufunguliwa ni “uwanja muafaka” kwa wote wanaojituma na kutaka maendeleo kiuchumi.
Spitalfields ina zaidi ya miaka mia tatu. Ingawa ilipoanzishwa makao yake yalikuwa mtaa wa Brick Lane karibu na Liverpool Street, leo tawi jipya, New Spitalfields Market limehamishwa karibu uwanja yalipofanyika mashindano ya Olimpiki mwaka jana. Tawi hili lilifunguliwa rasmi 1991 na linaongoza Ulaya nzima kwa usambazaji wa matunda na mboga toka nchi zenye joto duniani.
Kati ya nchi hizo ni ndugu zetu wa Kenya kupitia kampuni ya SACOMA(“Sahara Communities Abroad”) iliyoanzishwa mwaka 2000 kuendeleza wananchi wasiojiweza kiuchumi na kielimu walioko jimbo la kusini ya jangwa la Sahara wanaozungumza Kiswahili. Licha ya kusafirisha bidhaa na kuziuza New Spitalfields, SACOMA , anasema msemaji wake Bi Perez Ochieng hutoa ajira kwa takriban watu 30,000 Ulaya na Kenya.
Perez Ochieng, mumewe Sam Ochieng (mkurugenzi SACOMA) na meneja mwendeshaji New Spitalfields, Bw. Nigel Shepherd walimtembeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiongozana na Balozi wetu Ungereza , Mhe Peter Kallaghe, mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania, London, Yusufu Kashangwa na maofisa wengine. Ubalozi wa Tanzania Uingereza ndiyo ulioratibu na kuandaa tukio zima.
Waziri Mkuu na wenzake walikuja London kuhudhuria mkutano wa kimataifa unaoangalia namna ya kuondoa njaa na umuhimu wa lishe bora kwa kina mama na watoto ulimwenguni. Mkutano umeandaliwa na asasi za serikali na zisizo za kiserikali kukutanisha mataifa makubwa (yaani G8), wachangiaji, wadhamini na watoaji misaada kwa lengo la kutokomeza njaa na kusaidia kuwapatia kina mama na watoto lishe bora.
Baada ya matembezi ndani ya ghala, SACOMA iliandaa kikao kifupi kuonyesha namna na pia mazao gani huuzwa. Baadhi ya mazao yaliyowekwa mezani kilipofanyika kikao ni pamoja na mahindi ya kuchemsha, ndizi kisukari, juisi za matunda, viazi vitamu, maembe sindano na mboga maarufu ya Sukumawiki ambayo hutumiwa zaidi Kenya. Sukuma Wiki (iliyo ndani ya familia ya mboga za kabeji) huuzwa tayari imefungwa kwenye mifuko na SACOMA.
Wakati wa kikao hicho wazungumzaji wahusika walieleza namna ambavyo soko litawafaidi wakulima , vijana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale wanaojituma.
Meneja Mwangalizi wa soko, Nigel Shepherd na Wana
SACOMA walifafanua baadhi ya masharti yanayotakiwa kufikiwa kuleta bidhaa hizi sokoni. Mojawapo ni kuzingatia taratibu za uuzaji wa mazao uliowekwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU). Taratibu hizo ni mathalan upandaji mazao unavyofanywa kusudi umudu safari ya muda mrefu, hifadhi yake katika makasha ya baridi, usafi wa jumla, ufungaji na utangazaji (branding).
Perez Ochieng alitoa mfano namna SACOMA ilivyojitahidi kuwahusisha vijana wa Kenya katika kilimo ambacho kimewaletea ajira na kuboresha maisha yao. Akifafanua Perez alisema kawaida vijana waishio mijini huwa hawavutiwi na kazi za kilimo lakini kuna “mengi ya kuzingatiwa ikiwemo kazi za kupakia bidhaa, kuzifunga katika mifuko, uendeshaji magari, uandishi wa makasha, nk.”
Akiendeleza hoja zaidi Waziri Mkuu ambaye kazaliwa mazingira ya kilimo alisema shughuli hii imedunishwa na mtazamo kuwa ni kazi ngumu na chafu ya jembe tu. “Inabidi tuweke mazingira yatakayowafanya vijana waone kazi zao zinaweza kupata soko. Kazi kubwa inahitajika kufanywa kuwafanya vijana wapende kilimo.”
Akitoa mfano wa kampuni ndogo ya vijana wa Gongo Seke walioamua kufanya biashara ya kilimo cha bustani aliyotembelea karibuni mkoa wa Mwanza, Waziri Mkuu alisema hiyo inathibitisha wapo wanaoweza kufuata fani hii.
Mheshimiwa Pinda aliwahakikishia wenyeji kwamba si tatizo hata kidogo kwa Tanzania kuuza bidhaa zake. Akithibitisha uzoefu wake kama mkulima, Waziri Mkuu aliwachekesha wasikilizaji aliposhika moja ya ndizi kisukari zilizokua mezani akasema Watanzania wanaweza kuleta ndizi zilizovimba zaidi na maembe dodo makubwa kuliko yale sindano yaliyoonyeshwa.
Kufuatana na takwimu zilizotolewa na idara ya habari ya CNN mwaka jana, ingawa uchumi wa Afrika unatazamiwa kukua kwa asilimia 4.5 idadi ya vijana inatazamiwa kuongezeka mara mbili barani mwaka 2045. Leo asilimia 30 ya vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 29 hawana ajira katika jamii nyingi za Afrika.
No comments:
Post a Comment