Na Husna Mohammed
UJENZI wa kiwanja cha mchezo wa judo kisiwani Pemba, unatarajiwa kuanza wakati wowote mwezi ujao. Kiongozi wa mchezo huo nchini, Tsuyoshi Shimaoka, amesema fedha kwa ajili ya ujenzi huo zinatarajiwa kupatikana katikati ya mwezi huu kutoka Ubalozi wa Japan nchini.
Alisema ujenzi huo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 185, na kuongeza kuwa, michoro ya ujenzi tayari imekamilika, na hati ya ardhi ya kiwanja kitakachotumika kwa ujenzi huo imeshakabidhiwa kwa Chama cha Judo Zanzibar (ZJA)..Shimaoka ameitaja kampuni itakayojenga kiwanja hicho kuwa ni Pambo Professional ya Zanzibar.
Hata hivyo, amefahamisha kuwa, zabuni kwa ajili ya kupata msimamizi wa kazi hiyo itatangazwa baadae. Shimaoka alieleza kuwa, Julai 8, mwaka huu, wanatarajia kwenda kisiwani Pemba pamoja na Balozi mdogo wa Japan kwa ajili ya kukiangalia kiwanja hicho.
Akizungumzia kuhusu vifaa vya ujenzi huo, alisema tatani 232 zitakazotandikwa katika kiwanja hicho zimeagizwa kutoka nchini Japan na zinatarajiwa kuwasili kati ya mwezi ujao na Septemba mwaka huu.
Alisema tatani 90 kati ya hizo, ni msaada kutoka kwa chama rafiki cha 'All Japan Judo Federation', wakati nyengine 100, wamepewa na chama cha 'All Judogi Tatani, ambazo zote zitawasili kutoka Japan mwishoni mwa mwaka huu. Alihitimisha kuwa kusema, kiwanja hicho kinatarajiwa kufunguliwa wakati wa sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi mwakani.
No comments:
Post a Comment