Habari za Punde

CAG Abaini Ubadhilifu Masharika ya Umma. SMZ Haikushirishwa Tozo la Simu.

Hafsa Golo na Asya Hassan
MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini udharifu katika masuala ya ufungaji na uwasilishwaji wa hesabu katika baadhi ya mashirika, halmashauri za wilaya na kusababisha malimbikizo makubwa ya madeni wanayodai au kudaiwa na taasisi za serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu kwa wizara, mashirika na taasisi za serikali mwaka 2011/2012 katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi jana.

Alisema sababu kubwa ni kutofuatwa sheria za manunuzi ya umma ya mwaka 2005 na kanuni zake na kukosekana vielelezo muhimu katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mashirika na taasisi hizo.

Akizungumzia kuzorota miradi ya ujenzi wa majengo ya serikali, alisema kumesababishwa na kuchelewa kupatikana fedha, kutokuwepo usimamizi mzuri na ukiukwaji wa sheria na taratibu za manunuzi pale fedha zinapopatikana hali inayoisababisha hasara kubwa serikali.

Hata hivyo, alisema kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya kawaida ya mwaka wa fedha 2011/2012, hali ilikuwa nzuri ambapo shilingi 262,824,308,000 ikiwa sawa na ongezeko la shilingi 43,739,308,000 sawa na asilimia 16.7 zilikusanywa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2010/2011 ambapo makusanyo yalikuwa shilingi 219,085,000,000.

Alisema kuna fursa nzuri ya kukusanya mapato zaidi kama jitihada za makusudi zitachukuliwa.

Pamoja na kujitokeza changamoto mbali mbali, alisema ofisi ya CAG inaendelea kutekeleza mpango mkakati ulioanza 2011 na unatarajiwa kukamilika 2014 ambapo umejikita kuimarisha ofisi kiutendaji sambamba na kuongeza idadi ya wafanyakazi wenye ujuzi wa fani mbali mbali kwa lengo la kusaidia kuimarisha kazi za ukaguzi.

Mwenyekiti wa PAC, Omar Ali Shehe, alisema iwapo serikali itashindwa kuwajibika kuwakemea na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kijinai watendaji wanaofuja fedha za wananchi bado lengo la udhibiti halitofikiwa.

Alisema Zanzibar ina vianzio vingi vya mapato lakini kutokana na uzembe na kutowajibika kwa baadhi ya watendaji waliopewa dhamana ndio sababu wawekezaji mbali mbali wa mahoteli wanaendelea kuitafuna Zanzibar kiuchumi huku faida ya uwekezaji huo ikiwanufaisha wageni.

Mapema akijibu hoja za Wawakilishi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema serikali inaandaa mikakati madhubuti ya kukuza mapato na kudhibiti mianya ya uvujaji wa fedha.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha mtandao utakaoshughulikia ukusanyaji kodi.

Pia alisema serikali imo katika hatua za kufunga mitambo itakayodhibiti mapato ya viza.

Alisema ZIPA itahakikisha kila muwekazaji anapata mahitaji yote ikiwemo ardhi na vitendea kazi.

Aidha alisema jumla ya taasisi15 zimekwepa kulipia kodi ZRB ambapo 13 zimefikishwa katika vyombo vya sheria na mbili zimeahidi kulipa.

Akizungumzia mkonga wa taifa alisema hauna haja ya kuondoshwa kwani hakuna athari itakayojitokeza na kwamba bado upo katika eneo zuri na linalofaa.



Aidha Waziri huyo alisema anasikitishwa na ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wanaoiba fedha za umma.

Hata hivyo, alisema tayari wameanza uchunguzi wa malipo ya wafanyakazi hewa baada ya kumruhusu CAG kufanya uchunguzi juu ya malipo ya mishahara hewa.

Alisema kazi hiyo itafanywa katika wizara zote ambapo wafanyakazi watatakiwa kuchukua mishahara yao katika ofisi wanazozifanyia kazi badala ya benki.

Alisema uchunguzi huo pia utafanywa kwa wastaafu wanaolipwa viinua mgongo na pencheni.

Wakati huo huo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha mswada wa sheria ya kuidhinisha makisio ya matumizi ya serikali ambapo makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 658,526,528 kutoka mfuko mkuu wa serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14, yameidhinishwa.

Waziri Mzee alisema kupitishwa kwa mswada huo kutawezesha pia serikali kukopa ndani na nje kiasi cha fedha zilizotajwa kwenye kifungu cha 5(1) cha mswada huo pamoja na masharti yake kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30.

Aidha alisema mswada huo una vifungu tisa ambavyo vinatoa muelekeo mzima wa utumiaji wa fedha hizo.

Katika hatua nyengine Mwantanga Ame anaripoti kwamba serikali imesema haijashirikishwa katika mchakato wa kupanga viwango vipya vya kodi ya tozo la simu, vinavyokusudiwa kutozwa watumiaji wa simu za mkononi nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alisema hayo jana wakati akijibu hoja za wajumbe wa baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Bunge lilipitisha sheria inayowataka kila mtumiaji wa laini ya simu kutozwa kodi ya shilingi 1,000, kitendo ambacho kinapingwa vikali na wadau mbali mbali.

Alisema tangu kuanza mchakato huo, hajawahi kushirikishwa katika maamuzi yoyote juu ya suala hilo na analisikia linaendeshwa na upande mmoja wa Muungano, wakati Zanzibar pia ina watumiaji wa simu za mkononi.

“Penye ukweli napenda niseme kweli kwa hili mimi sijashirikishwa tangu limeanza hadi limemalizika ila sasa nasubiri hatma kutoka bungeni,” alisema.

Alisema serikali ya Zanzibar, baada ya kukamilika mchakato wa bunge itakaa na kuliangalia suala hilo litakavyomalizikia pamoja na utekelezaji wake.

Alisema kama serikali ya Muungano itaamua kuondoa kodi hiyo na serikali ya Zanzibar haitaona umuhimu wa kuendelea kuwatoza kodi wananchi.

Aidha alisema miradi mingi haikuweza kufikiwa lengo lilikosudiwa kutokana na fedha zilizoingizwa kutumika kinyume na makusudio.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.