Na Mwajuma Juma
TIMU ya Soka ya Wizara ya Utumishi Ikulu imeondolewa katika mashindano ya kombe la Mapinduzi ya Mawizara kwa kuvunja taratibu za mashindano hayo.
Timu hiyo ambayo ilipaswa kucheza mechi yake na Wizara ya Fedha juzi lakini mchezo huo haukuchezwa baada ya wachezaji wake wengi kutokuwa na vitambulisho vya ZSSF na NSSF.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo Mohammed Azan amesema kuwa katika mashindano yao kuna vigezo na masharti ambavyo vinatumika ikiwemo washiriki wawe waajiriwa wa wizara husika ambao vitambulisho vyao vitakuwa aidha ni kitambulisho cha ZSSF na NSSF jambo ambalo halikutendeka kwa timu hiyo.
Hivyo alisema kuwa kutokana na hali hiyo ni dhahiri timu hiyo imejitowa kwenye mashindano kwa vile timu ikikosa kucheza mechi moja itakuwa imetoka kutokana na michuano yao imeanza kwa mtoano.
“Kimsingi Ikulu imetoka katika mashindano na sisi kamati tumebariki kwani haikuweza kucheza na sababu ikiwa wachezaji wake hawana vitambulisho hivyo”, alisema.
Hata hivyo alisema kuwa hadi sasa wakiwa wanaaza hatua ya makundi mashindani hayo yanaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote lilijitokeza ukitoa hilo la timu ya Ikulu.
Michuano hiyo ilianza kwa mtoano ambapo timu zilizoingia katika hatua ya makundi ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Wizara ya Fedha, PBZ, IPA, Miundombinu na Mnazimmoja.