Na Mwajuma Juma
WANAWAKE wa Kizanzibari wametakiwa kusimama imara kwa kujiendeleza kielimu na kiuchumi na kujaribu kusoma mazingira kwa lengo la kuiletea mabadiliko nchi yao.
Akizungumza katika kongamano la Baraza la Wanawake la Chadema (BAVICHA), Mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA Josephin Slaa amesema kuwa elimu sio lazima uende darasani bali hata kusoma mazingira ya wapi unatoka na unapokwenda na sio kukaa na kubakia kubebeshana lawama jambo ambalo halitawasaidia katika mapambano yao.
Alisema kuwa kitu chochote ambacho kitafanyiwa mabadiliko ni lazima kwamba uandae mikakati vyenginevyo hutoweza kusonga mbele.
Hata hivyo alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na matokeo mengi ya uvunjifu wa amani ambayo yanafanyika kwa lengo la kuichafua Zanzibar huku wanawake kama wanawake ambao ndio tegemeo la watu wengi wakiwa wamekaa kimya.
Hivyo aliwataka kujifunza kujadili masuala ya msingi ili wafikie katika maamuzi magumu hasa kwa vile wanawake wakithubutu wataweza.
Aidha alisema kuwa watanzania wengi wanakuwa nyuma katika masuala ya maendeleo, hali ambayo inatokana na kuchoka mapema.
Hivyo aliwataka kutofanya mzaha kwani watakapokuwa na uchungu wan chi yao ndipo watakapoweza kuikomboa nchi yao.