Habari za Punde

Kitabu cha mwaka cha Sheria Zanzibar (Zanzibar yearbook of Law) chazinduliwa

 Mmoja miongoni mwa Wanafamilia ya Gwiji wa fani ya Sheria Kitaifa na Kimataifa Marehemu Profesa Haroub Othman, Bwana Abdulla Miraji akiushukuru Uongozi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kwa kuendeleza malengo la Muasisi wa Kituo hicho kwenye uzinduzi wa Kitabu cha Zanzibar yearbook of Law uliofanyika Eacrotanal Mjini Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikizindua rasmi Kitabu cha Zanzibar Yearbook of Law kusherehekea maisha ya muasisi wa kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Marehemu Profesa Haroub Othman hapo katika ukumbi wa Eacrotanal Mjini Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikionyesha rasmi Kitabu cha Zanzibar yearbook of Law kwa wanataaluma wa fani ya sheria mara baada ya kukizindua rasmi hapo Eacrotanal.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari na kushoto yake ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi.
 
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.


 Na Othman Khamis Ame OMPR

Uongozi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar umekumbushwa kuendelea kubakia kuwa  urithi wa mchango mkubwa kwa jamii ulioachwa na Mwanafalsafa mahiri aliyebobea katika  fani  ya Sheria Zanzibar, Tanzania na Kimataifa  Marehemu Profesa Haroub Othman.
 
Urithi huo aliouacha Profesa Haroub ulilenga zaidi katika kuwasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria kupata msaada na haki za  kisheria pamoja na utaalamu wa haki za binaadamu.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akikizindua kitabu cha Mwaka cha Sheria Zanzibar  { Zanzibar yearbook  of Law } katika kuendeleza  kumbukumbu ya Maisha ya Marehemu Profesa Haruob Othman uliofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Simulizi  Asili na Lugha za Kiafrika                       { Eacrotanal } kiliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 
Balozi Seif alisema urithi huo unaoendelezwa na Kituo hicho cha sheria Zanzibar umekuwa ukitoa fursa ya msaada kwa wananchi wanyonge kupata haki zao wengi zaidi wakiwa ni akina mama, watoto, watu wenye ulemavu pamoja na wazee.
 
Alifahamisha kwamba kazi hizo zinazofanywa na Kituo hicho zilikuwa ni moja ya azma ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo ifikapo Januari 12 mwaka 2014 yanatimiza umri wa miaka 50 aikiwa  ni jambo la kujivunia kwa Wananchi wote.
“ Tunaadhimisha kumbu kumbu ya  maisha ya Prof. Haroub Othman, mwanzilishi wa Kituo hichi cha Huduma za Sheria Zanzibar. Angekuwepo leo Prof. Haroub Othman, uzinduzi huu wa Kitabu cha Zanzibar Yearbook of Law ungeweza kufanywa ndani ya mikono yake”. Alifahamisha Balozi Seif.
Balozi Seif alieleza kwamba usomi wa Profesa Haroub Othman ulisaidia sana kutoa na kuzalisha wataalamu mbali mbali katika taaluma ya sheria, sayansi ya jamii na hata masuala ya Haki za Binadamu ambao kwa sasa wamekuwa walimu wa Taifa hili.
“ Profesa Haroub hakuwa mchoyo katika jambo lolote alilokuwa akiliamini. Alikuwa mpenda watu, mcheshi hana makuu wala dharau. Sisi lazima tuzienzi juhudi zake, kazi zake ili tuwe sehemu ya Profesa Haroub ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba Marehemu Profesa Haroub Othman alikuwa akihimiza suala zima la kudumishwa kwa amani ya Nchi ambalo ipo haja kwa wananchi wote kuliheshimu suala hilo kwa kuwacha kushabikia makundi yenye lengo la kubomoa amani iliyopo Nchini.
Akizungumzika suala la uzinduzi wa kitabu cha Zanzibar Yearbook of Law,  Balozi Seif alisema hiyo ni hatua kubwa katika kazi za Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar wanayopasa  kujivunia kwa vile Zanzibar inaingia katika ramani ya dunia kuwa ni nchi yenye wataalam waliobobea katika fani ya sheria.
Aliwaomba watendaji wa  Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar waendelee na moyo wa kumuenzi Profesa Haroub, kufikiria changamoto zinazolikabili Taifa na Wananchi wa Zanzibar katika masuala ya Sheria pamoja na kuandika sambamba na  kuweka vizuri kumbukumbu za sheria kwa faida ya vizazi vya sasa na vya baadae.
Akitoa salamu za wanafamilia ya Marehemu Profesa Haroub Othman Mmoja wa wanafamilia hao Bwana Abdulla Miraji alisema familia hiyo imefarajika na kazi zinazoendelea kufanywa na kituo hicho kwa kuchapishwa vitabu vinavyosaidia wananchi katika kuelewa haki zao kisheria.
Hata hivyo Bwana Miraji alitoa wito kwa Uongozi wa Kituo hicho kuongeza nguvu zaidi vijijini ili kusaidia kupunguza matatizo mengi yanayoikumba jamii kwenye Vijiji mbali mbali Nchini.
Alisema yapo matatizo ya muda mrefu yanayoendelea kusumbua jamii akatolea mfano wa masuala ya udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba zaidi watoto, wanawake, Wazee pamoja na suala sugu la matumizi ya ardhi.
“ Haya yote yanaendelea kutokea na kuwakumba wananchi hasa wale wenye maisha duni kutokana na kasoro kubwa ya ukosefu wa taaluma ya sheria “ Alisisitiza Mwanafamilia huyo wa Marehemu Profesa Haroub Othman.
Akizungumzia mchakato wa Taifa kuelekea kwenye bunge la Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Abdulla Miraji aliwaasa wananchi watakaoingia kwenye Bunge hilo kuhakikisha kwamba wanaleta Katiba bora itakayokidhi mahitaji ya Wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Aliomba kuangaliwa kwa mtazamo wa pekee kundi kubwa la Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara wanaokadiriwa kufikia zaidi ya Watu Laki 750,000 ambao wamekosa fursa ya kusemewa kwenye mchakato mzima wa maoni ya katiba katika kujua hatma ya maisha yao ya baadaye.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wahariri wa Kitabu hicho cha Zanzibar Yearbook of Law ambae pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman alisema kitabu hicho ni kielelezo kikubwa kwa Zanzibar kutoa mchango wa Taaluma katika Nyanja ya Kimataifa Kisheria.
Mh. Othman alisema Zanzibar imekuwa na Historia ndefu katika fani ya sheria kwa kuanzisha Gazeti rasmi la Serikali, Mahkama rasmi ya Kadhi pamoja na Ripoti ya Sheria tokea karne ya 18.
“ Zanzibar ilianzisha Law Report mwaka 1866 hadi mwaka 1986, ikaanzisha Gazeti la mwanzo rasmi la Serikali mwaka 1894 pamoja na kuanzisha Mahkama rasmi ya kadhi mwaka 1897 ”. Alifafanua Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif Ali Iddi kuzindua kitabu hicho cha Zanzibar Yearbook of Law Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari alisema Kitabu hicho kimejikita zaidi katika kutoa elimu itakayowasaidia wananchi wasiokuwa na sauti katika jamii kuwa na nguvu za kutetea haki zao.
Waziri Aboubakari aliiomba jamii kuwa na wajibu wa kuendeleza malengo la Profesa Haroub Othman ambayo  katika uhai wake aliyasimamia kuona haki ya kila raia inapatikana wakati na mahali popote pale.
Kitabu cha Zanzibar Yearbook of Law kimeandikwa takriban na waandishi wapatao 15 kikitoa taaluma ya masuala ya Kisheria  Kimataifa, Afrika, Kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania na Zanzibar kwa ujumla


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.