Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
amezifariji na kuzipa mkono wa pole familia za wananchi waliokumbwa na maafa
kutokana na ajali ya boti ya Kilimanjaro II na wale nyumba zao zilizoteketezwa
na moto kisiwani Pemba mapema mwaka huu.
Akizifariji katika maeneo tafauti, amezitaka kuwa na subira kutokana
na maafa yaliyowakuta kwa sababu matukio kama hayo yanaweza kumkuta binadamu
yoyote bila ya kutarajia.
Akizungumza na familia ya Nd.
Khamis Issa Mohammed katika mtaa wa Mbuyu Mnne Unguja, ambayo imepoteza
watoto watatu katika ajali ya boti iliyotokea Januari 5 katika eneo la mkondo
wa Nungwi, alisema serikali na jamii nzima iko pamoja nao katika wakati huu
mgumu wa maombolezi.
Familia ya Khamis Issa ilipoteza watoto watatu ambapo mmoja, Nasba
Khamis Issa aliweza kuokolewa.
Wakati huo huo, alipongeza mshikamano uliooneshwa na wananchi wa
Shumba Mjini na Maziwa Ng’ombe baada ya kutokea maafa ya moto mapema mwezi huu.
Alisema mshikamano na umoja uliooneshwa na wananchi hao kwa kusahau
tafauti zao zote wakati wa maafa hayo ni mkubwa na hauna budi kuendelezwa
katika maeneo mengine yanapotokea maafa.
Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi na watu walioathiriwa na
maafa ya nyumba zao kuteketea kwa moto katika vijiji vya Shumba Mjini na Maziwa
Ng’ombe.
Alisema mshikamano wa aina yake uliooneshwa na wananchi hao katika
kuzima moto pamoja na kuepusha usisambae na kusababisha maafa zaidi ni wa
kupigiwa mfano na wananchi wa maeneo mengine waige mfano wa watu wa Shumba na
Maziwa Ng’ombe.
Moto mkubwa uliozuka Januari 3 na 4 katika vijiji hivyo ulisababisha
hasara kubwa kwa baadhi ya nyumba kuteketea kabisa na vitu vyote vilivyokuwemo
na zaidi ya familia 50 zimeathirika.
“Nimekuja kuwapa mkono wa pole wote waliokutwa na maafa haya, lakini pia
kuwapongezeni wananchi wa maeneo haya kwa mshikamano wa aina yake mliouonesha
baada ya kutokea maafa yale,” alisema alipokuwa akiwahutubia wananchi wa maeneo
hayo.
Alisema wananchi wote wa maeneo hayo walisahau tafauti zao na
kuhakikisha moto huo hauendelei kusababisha maafa zaidi, baada ya kuwepo hatari
ya kuteketea sehemu kubwa zaidi ya maeneo hayo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Dadi Faki Dadi, amempongeza
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kutokana na moyo wake wa kuwafariji na
kuwapa mkono wa pole wananchi hao, ambao hivi sasa wanakabiliwa na wakati mgumu
kutokana na maafa hayo.
Alisema Serikali kwa jumla imekuwa karibu na wananchi hao na imeonesha
moyo wa imani na huruma kutokana kutoa misaada mbali mbali kwa wananchi hao,
tokea yalipotokea maafa hayo.
No comments:
Post a Comment