Habari za Punde

Dk Shein : Tumieni fursa za huduma za jamii vizuri

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                    04 Januari, 2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wananchi wametakiwa kuzitumia vyema fursa za huduma za jamii zinazopatikana hivi sasa katika maeneo yao zikiwa ni matunda ya utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
 

Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiongwe, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja mara baada ya kufungua Kituo cha Afya cha Kijiji hicho.
 

Aliwaeleza wananchi wa kijiji hicho kuwa kuzinduziliwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa ahadi ya Chama cha Afro Shirazi iliyoitoa kwenye mkutano wake wa mwisho wa kampeni za Uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Julai, 1963 kuwa endapo itashika dola itatoa huduma za jamii ikiwemo afya na elimu bila malipo wala ubaguzi.
 

Aliwakumbusha wananchi hao kuwa wakati wa ukoloni wengi wao katika kijiji hicho kama ilivyokuwa kwa wananchi wengi wa sehemu za mashamba hawakuweza kupata huduma za matibabu kutokana na sera ya utawala wa kikoloni kutoa huduma hizo kwa ubaguzi na zaidi kutozingatia huduma hizo kwa watu wa mashamba.


Kwa hiyo alibainisha kuwa dhamira  hiyo ya chama za ASP ambayo iliweka mkazo katika kutoa huduma za matibabu na dawa bure, kuondoa ubaguzi na unyonge katika hospitali zote na kuongeza utibabu katika sehemu za mashamba na kuwezesha madaktari kutembelea vituo vya afya vya mashamba imekuwa ikitekelezwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi sasa hatua kwa hatua.

DK. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa dhamira ya Serikali wakati wote ni kupeleka huduma za jamii karibu na wananchi kama ilivyofanya kwa kijiji hicho kwa hiyo aliwataka wananchi hao kujenga uhusiano wa karibu na ushirikiano mzuri kati yao na watumishi wa afya kituo hicho.

Alisema wataalamu wa afya ni watu wazuri wanaofanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma yao hivyo makosa madogo madogo ya yanayoweza kutokea ni ya kibinadamu kama anavyofanya binadamu mwingine ye yote katika jamii.
 

Akijibu risala ya wananchi hao Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia kuwa ahadi ya kujenga barabara ya lami Bumbwini hadi Kiongwe itakamilishwa kwa kipande kilichobaki kati ya Bumbwini Makoba hadi kijijini hapo si muda mrefu.
 

Kuhusu huduma ya maji alisema utekelezaji wa ahadi hiyo unaendelea kwa kuongeza visima zaidi kwa msaada wa Serikali ya Ras Al Khaimah na kuhusu umeme aliahidi kuliagiza Shirika la Umeme Zanzibar- ZECO kushughulkia ombi hilo.
 

Wakati huo huo Serikali imesema kuanzia sasa haitaruhusu tena ujenzi wa vituo vipya vya afya isipokuwa katika mazingira maalum kwa kuwa vituo vilivyopo vinatosheleza mahitaji kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 1964.  
 

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha Afya cha Kiongwe jana Waziri wa Afya Juma Duni Haji alisema Sera hiyo ya afya iliweka utaratibu wa kuwapatia wananchi huduma za afya si zaidi ya kilomita 5 ambapo hivi huduma hizo zinapatikana kutoka umbali wa kilomita tatu tu.
 

Alibainisha kuwa hivi sasa humu nchini kuna vituo vya afya 135 vya Serikali mbali ya binafsi na vinavyomilikiwa na taasisi za Serikali hivyo ametoa wito kwa wananchi ambao wanahisi wanahitaji kituo cha afya kuwasiliana kwanza na uongozi wa Wizara kabla ya kuchukua hatua ya ujenzi.
 

Waziri Duni alisema hivi sasa Wizara yake inaweka mkazo zaidi kwa kushirikiana na wananchi kuimarisha vituo vilivyopo kwa kuvipatia vifaa na wataalamu na kwa upande mwingine ujenzi wa nyumba za watumishi wa vituo hivyo.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz

1 comment:

 1. ziko wapi hizo huduma?
  afya ? kama kweli ni nzuri mbona mnaenda kutibiwa nchi za nje mkiumwa kidole tu!
  elimu? kama kweli ni nzuri mbona watoto wenu mnapeleka praiveti au nje!
  maji? mpaka leo tunatembea na madoo na maplastiki kutafuta maji , usiku kucha tunawanga kuvizia
  maji
  umeme? uko wapi mara upo mara haupo hauna msimamo kama kakakuona

  ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.