Habari za Punde

Waathirika wa maafa ya moto Pemba waaswa kuwa na subira

Na Bakar Mussa, Pemba
Shirika la Biashara la Taifa ( ZSTC) Zanzibar, limekabidhi msaada wa Bidhaa mbali mbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mheshimiwa , Dadi Faki Dadi, wenye thamani ya Tshs, 5,325,000/=, kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi waliofikwa na maafa ya kuunguliwa na Moto wa Shehia za Shumba Mjini na Maziwa Ng’ombe katika Wilaya ya Micheweni .
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa MKoa wa Kaskazini Pemba, MKurugenzi Mwendeshaji wa Shirika hilo, Mwanahija Almas Ali,aliwataka Wananchi hao kuwa na subra katika kipindi hichi kwani yaliotokezea yote ni maandiko kutoka kwa Mwenyeezi Mungu na kila Mmoja ameguswa na Mtihani huo ambao unaweza kutokezea kwa mtu yoyote.
Akizungumza na Wananchi hao huko katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba, Mkurugenzi huyo alisema kuwa Mtihani wowote unatokezea basi huwa umepangwa na Allah hivyo aliwasisitiza kuwa na subra na wapokee msaada huo ambao umetolewa na ZSTC, na iko pamoja nao na itaendelea kusaidiana nao kwa kadri ya Uwezo wao utaporuhusu.

“ Shirika letu linaguswa na Mtihani huu na liko pamoja nanyi na halitosita kuwasaidia kwa kadri Uwezo wetu utaporuhusu”, alisema, Mwanahija.
Mkurugenzi huyo , alieleza kufurahishwa kwao na juhudi zilizo chukuliwa na Wananchi wa Shehia ya Maziwang’ombe katika Wilaya hiyo ya kuamuwa kuwajengea Wananchi Nyumba za kuishi kwa haraka sana na kuahidi kuchangia Tshs, 400,000/= kwa ajili ya kuongezea Matufali kwa ajili ya kuendeleza Ujenzi huo ambapo Nyumba nne tayari zimeshajengwa kwa kutumia Matufali ya kuchongwa kwa wale walaiofikwa na mtihani wa kuunguliwa na moto Majumba yao.
Akipokea Msaada huo wa Bidhaa mbalimbali ikiwemo Mchele, Unga wa Ngano, Sukari , Mafuta ya kula na Maharage, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mh, Dadi Faki Dadi,alilipongeza Shirika la ZSTC, kwa  kujali maisha ya Watu wengine hasa wenye matatizo kama hayo na kwamba Msaada huo ameupokea kwa furaha kubwa na utawafikia Wahanga wa tukio hilo kama ulivyokusudiwa.
Alisema kuwa Utamaduni wa kusaidiana kwa Watu ambao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo kama hayo ulikuwepo miaka mingi iliopita na kwamba ni Vyema Wananchi kuendeleza Utamaduni huo , na kuyataka Mashirika na Watu wengine wenye Uwezo kuiga mfano wa Shirika hilo la ZSTC.
Masheha wa Shehia hizo, Rahma Moh’d Shaame wa Shehia ya Shumba ya Mjini, na Asha Yussuf Hassan, wa Shehia ya Maziwa Ng’ombe, alieleza kuwa ni jambo la faraja kuona kuwa Serikali iliposikia Wananchi wake wamefikwa na Mitihani kama hiyo haikukaa kimya na badala yake wakafuata moja kwa moja kuja kuwafariji hiyo inwapa myo Wananchi hao kuona kuwa Serikali na Viongozi wao inawajali.
Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi huko katika Viwanja vya Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba, kwa pamoja walieleza kwamba wamefurahishwa namna ya Viongozi wa Serikali na wale wa Vyama vya Siasa na Mashirika na Watu binafsi kwa walivyoguswa na Mtihani huo uliotokezea kwa Wananchi wao na kuonesha moyo wa kutowa misaada mbali mbali ya kiutu kwa Wahanga hao.
“ Mtihani uliopita kwa Wananchi wa Shehia zetu ni mkubwa lakini yote ni maandiko kutoka kwa Mwenyeezi Mungu , lakini kwa vile Wananchi kutoka mbali mbali kuona wanaguswa na mtihani huu tuliopewa na wakaamuwa kutusaidia tumefurahi ijapo tuna machungu, “alisema , Sheha wa Shehia ya Maziwang’ombe , Asha Yussuf.
Haji Ali Kombo (70) Mkaazi wa Shehia ya Maziwang’ombe ni mmoja wa Wahanga hao, ambae aliunguliwa na Nyumba yake, alisema kuwa anaipongeza Serikali ya Mapinduzi kwa kuona kuwa lilotokezea na Mtihani wa Allah, na kuwafika kwa haraka Wananchi kuwafariji na kuwasaidia jambo ambalo limewatia moyo na kuona kuwa Viongozi wao wanawajali Wananchi wao.
Kombo Shineni Ali (25) mkaazi wa Maziwa Ng’ombe, ni miongoni mwa Wahanga hao , ambae alimueleza Mwandishi wa habari hizi kwamba ni wazi kwamba Serikali inawajali Wananchi wake hasa wanapokuwa na Mitihani kama hiyo na kuwa karibu nao kwa hali na mali ili kukabiliana na matatizo yao.
Alisema kuwa ” tunayashukuru Mashirika mbali mbali ikiwemo ZSTC, na wale watu binafsi ambao wamekuwa wakitusaidia kwa hali na mali na kwamba tunawaomba wasisite kufanya hivyo na mola atawalipa lao fungu”.
Kombo Faki Kombo (70) mkaazi wa Shumba ya Mjini ni miongoni mwa Wahanga hao, ambae alisema kuwa Wananchi wa Zanzibar hawana budi kurejesha Utamaduni wa Kusaidiana hasa pale wanapofikwa na mitihani kama hiyo iliotokezea ni jambo la kutia moyo kuwaona Wananchi mbali mbali wamekuwa karibu sana na wale waliofikwa na mtihani huo.
Massoud Ali Khamis (48)mkaazi wa Shumba ya Mjini, ni miongoni mwa Wahanga hao, ambae alilipongeza shirika la ZSTC ,kwa kuonesha moyo wa kuguswa na Mtihani huo na kuamuwa kuwasaidia Binaadamu wenzao  waliofikwa na maafa kama hayo.
Misaada mbali mbali ya Kibinadamu imekuwa ikitolewa na Serikali , Mashirika, Taasisi na Watu mbali mbali kwa ajili ya Wahanga hao , ikiwemo Chakula , Nguo, Fedha Taslim, Vyombo vya matumizi nk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.