Habari za Punde

Vyandarua 315,465 vyenye dawa kugawiwa

 Waziri wa Afya Zanzibar Juma Duni Haji akisoma Taarifa ya Uzinduzi wa Mpango mpya wa Ugawaji wa Vyandarua vyenye dawa ya Muda mrefu ikiwa ni mkakati wa kutokomeza Ugonjwa wa Maleria Zanzibar katika Ukumbi wa Kitengo cha kupambana na Maleria MwanaKwerekwe Zanzibar.
Mfano wa Chandarua kinachotarajiwa kugawiwa Wananchi chenye dawa ya muda mrefu ili kujikinga na Ugonjwa wa Maleria. Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar.
 
Na Faki Mjaka-Maelezo
 
Wizara ya Afya Zanzibar imezindua Ugawaji wa Vyandarua Vyenye dawa ya muda mrefu ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha Ugonjwa wa Malaria unatokomezwa Zanzibar.
 
Akizindua Mpango huo Waziri wa Wizara hiyo Juma Duni Haji amesema kukamilika kwa ugawaji wa vyandarua hivyo kunaweza kutokomeza moja kwa moja Ugonjwa wa Maleria ambao kwa sasa upo chini ya Asilimia moja.
 
Amesema licha ya maambukizi kuwa chini ya Asilimia moja lakini Mikakati ya Wizara ni kuhakikisha ugonjwa huo unabaki historia katika Visiwa vya Zanzibar.
 
“Kwa kweli hadi sasa maambukizi yapo Chini ya Asilimia 1 lakini mipango yetu ni kuhakikisha Maleria yanabaki kuwa historia Nchi hii ndio maana tunaandaa kila mkakati kufikia lengo hilo” Alisema Duni.

Waziri Duni amefahamisha kuwa Jumla ya Vyandarua  315,465 vinatarajiwa kugawiwa kwa Wakazi wa Unguja na Pemba ambapo Unguja Watagawiwa Vyandarua 221,803 ambapo kwa Pemba watapata 78,637.
 
Amewataja watakaonufaika na Vyandarua hivyo kuwa ni kinamama Wajawazito,Walemavu, Wajane na Waliofikwa na Majanga yanayopelekea kukosa Uwezo wa kununua Vyandarua.
 
Kwa upande wake Msaidizi Meneja wa Kitengo cha kupambana na Malaria Zanzibar Mwinyi Mselem amesema pamoja na Kutoa Vyandarua hivyo Kitengo chake pia kinaendelea na Upigaji dawa kwa ajili ya kuulia mazalio ya Mmbu wa Maleria.
 
Mkakati mwingine wanaoutumia kutokomeza Maleria ni kufuatilia hali ya Ugonjwa inavyoendelea ambapo amewaomba Wananchi kuchukua tahadhari ya kuweka Mazingira safi na kuripoti Vituo vya afya pindi wanapojiskia Vibaya.
 
Kuhusu Ugawaji wa Vyandarua Mwinyi amesema Masheha wa Shehia ndio watakaohusika kutoa Kuponi kwa wale wanaostahiki kupewa Vyandarua ambapo amesisitiza kuwa Watajitahidi ili kila mwenye sifa za kupewa apate Vyandarua hivyo.
 
“Ndugu waandishi tumewaelekeza vizuri Masheha wetu tunaamini watatenda haki lakini kama kuna Sheha ambaye ataenda kinyume na mkapata ushahidi basi musisite kumpripoti ila haki ipatikane kwa Walengwa” Alibainisha Mwinyi.
 
Mradi huo Uliofadhiliwa na Mfuko wa Dunia(Global Fund),Mfuko wa Rais Bush wa kupambana na Maleria kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utaanza siku ya Jumatatu ambapo Walengwa watapa Vyandarua hviyo Unguja na Pemba.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR 06/06/2014.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.