Na
Mwandishi wetu,
ZANZIBAR inajivunia uhusiano wa muda
mrefu uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya watu wa
Norway katika kusaidia maendeleo ya wananchi wa Zanzibaar.
Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi Makaazi Maji na Nishati, Ali Khalil Mirza ameyazungumza
hayo wakati wa mkutano wa pamoja baina ya ujumbe wa Kamati ya Nishati na
Mazingira kutoka nchi ya Norway ulipofika ofisini kwake Forodhani kuangalia
utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na nchi hiyo.
Katibu
Mkuu amesema kuwa uhusiano wa muda mrefu uliopo wa kuwapa mafunzo watendaji
mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na uwekezaji katika
sekta ya Nishati ya umeme ni jambo la kupigiwa mfano.
Ujumbe
huo wa kamati ya Nishati na Mazingira kutoka Bunge la Serikali ya Norway
ukiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Bwana Ola Elvestuen umefika Zanzibar
kuangalia utekelezaji wa miradi mbali mbali inayofadhiliwa kupitia Shirika la
Maendeleo la nchi ya Norway (NORAD).
Mbali
na ujumbe huo kufanya mazungumzo na watendaji wa ofisi mbali mbali ulipata
fursa ya kutembelea kazi mbali mbali za ujasiriamali huko vijijini
zinazoendeshwa kwa kutumia nishati ya umeme.
Meneja
Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi: Hassan Ali Mbarouk akiukaribisha
ujumbe huo kuzungumza na wananchi wa shehia sita (6) za Mkoa wa Kaskazini hapo
Chuo cha Amali Mkokotoni amesema kuwa Shirika la Umeme linajivunia mafanikio
makubwa ya utekelezaji wa mradi huo wa usambazaji umeme vijijini ulitekelezwa
kwa awamu nne (4) tofauti zenye mafanikio makubwa tokea mashirikiano hayo
yalipoanza mnamo miaka ya 1980s.
Amefahamisha
kuwa mradi wa usambazaji umeme vijijini umepelekea upatikanaji wa umeme katika
maeneo mengi ya Unguja na Pemba ikiwemo uwekaji na ulazaji waya wa umeme
baharini kutoka Tanga hadi Pemba, uwekaji na ulazaji waya wa umeme bahirini
kutoka Mkokotoni hadi Tumbatu, uimarishaji wa miundo mbinu ya umeme na
usambazaji umeme vijijini.
Ujumbe
huo ulitembelea na kuangalia kazi mbali mbali za mikono kama vile kiwanda cha mbao
na kusaga nafaka kilichopo Mkwajuni na kuangalia kazi mbali mbali zinazofanywa
na Chuo cha Amali Mkokotoni zikiwemo ushoni na ufundi wa umeme.
Aidha,
ujumbe huo ulihitimisha ziara yake kwa upande wa Unguja kwa kufanya mkutano na
kuzungumza na wananchi wa shehia sita (6) za Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwemo shehia
ya Mkokotoni, Pita na Zako, Mto wa Pwani, Kibeni, Pale na Mkwajuni.
Wananchi
hao wametoa shukrani zao kwa Serikali ya Norway juu ya miradi ya usambazaji
umeme katika mkoa huo na kusema kuwa imewakomboa kiuchumi hususan katika
shughuli zao za uvuvi na kuuomba ujumbe huo kuweka nguvu zao zaidi kuwasaidia
katika sekta ya kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji maji.
Wakiwa
ni wafadhili wa karibu wa huduma ya umeme kupitia Shirika la Umeme ZECO na
ushirikiano uliopo tokea miaka ya 1980s Serikali ya Norway kupitia Shirika lake
la Maendeleo (NORAD) wameweza kusaidia sekta ya umeme nchini kwa awamu nne tofauti
zenye mafanikio ikiwa Shirika la Umeme (ZECO) kwa sasa linajiandaa na mpango
mwengine wa utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na NORAD.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Nishati na Mazingira kutoka Norway Bwana Ola
Elvestuen kwa niaba ya Serikali ya Norway wamewashukuru wananchi hao kwa
mwitikio wao na kuzungumzia changamoto mbali mbali zinazowakabili na kuahidi
kuzifikisha sehemu husika ili kuweza kufanyiwa kazi.
Ujumbe
huo utaendelea na ziara yake wiki hii kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment