Na Tatu Makame
WANAFUNZI 30 wa Almadrasatu Nurul-huda ya
Matetema Kitope wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja, wamenusurika kufa baada ya kula
mbegu za mbono.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 10:00 za jioni
wakati watoto hao walipochuma mbegu za mti huo na kula wakati wakicheza nje ya
madrasa yao.
Sheha wa shehia ya Matetema, Mohammed
Bakari,alisema watoto hao awali walikuwa wametolewa kwa ajili ya kwenda kusali pamoja
na mapumziko ndipo walipokwenda kwenye miti hiyo na kuchuma mbegu zake na kula.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini
Unguja, Salma Khamis, alisema ni kweli
alipata taarifa ya watoto wa kijiji hicho kula mbegu za mti huo, lakini
walikuwa 24 tu.
Alisema watoto hao walikimbizwa hospitali ya
KMKM Kibweni na 22 kati ya hao walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani na
wawili bado wanaendelea na matibabu.
Aliwataja wanaoendelea na matibabu hospitalini
hapo kuwa ni Mulhati Foum Khamis (3) na Amina Haji Khamis (6) wote
wakaazi wa kijiji cha Matetema.
Alitoa wito kwa wazazi na walimu wa madrasa
kuwaelimisha watoto kuhusu madhara ya mbegu za mti huo.
No comments:
Post a Comment