Habari za Punde

Mgodi wa Buzwagi Wapongezwa kwa Kuzingatia Sheria za Mazingira.

Meneja wa kinu cha kuchenjua dhahabu wa Mgodi wa Buzwagi Festo Shayo (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Naibu waziri ofisi ya makamu wa rais anaeshughulikia mazingira na Muungano, Luhaga Mpina namna mgodi wake unavyohifadhi maji yaliyotumika kusafishia dhahabu.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano Luaga Mpina (wa kwanza kushoto), akisikiliza maelezo ya Afisa Mazingira wa Mgodi wa Buzwagi bwana Frank Ngoroma (wa kwanza mkono wa kulia), aliyesimama katikati ni meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo.
Mh Luhaga Mpina akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo katika eneo la kituo cha Uthibiti wa taka mbalimbali mgodini hapo.

Naibu Waziri pamoja na wataalamu wake wakikagua moja ya maeneo ambayo NEMC yalitoa ushauri kuwa yafanyiwe kazi katika ziara zao, ambapo wakati wa ziara hii utekelezwaji wake ulikutwa umeisha kamilika kama walivyokuwa wameelekezwa.
Mmoja wa maafisa wa mazingira aliyekuwa ameandamana na naibu Waziri akiuliza jambo wakati wa ziara hiyo.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akifafanua jambo wakati wa ugeni wa naibu Waziri wa mazingira.
Baadhi ya maofisa wa Mgodi wa Buzwagi wakitoa maelezo mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano Luaga Mpina
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Shinyanga.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, ameupongeza Uongozi na wafanyakazi wa Mgodi wa Buzwagi kwa kuzingatia sheria za mazingira Mgodini hapo.
Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika Mgodi huo kwa lengo la kujionea namna mwekezaji huyo anavyozingatia maelekezo ya wataalamu wa wizara yake juu ya utunzaji wa mazingira.
Akiwa katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alitembelea bwawa maalumu kwa ajili ya kuhifadhia maji yalitumika kuchenjulia dhahabu na kujionea namna ambavyo mgodi huo unavyochukua tahadhari ya hali ya juu katika kuhakikisha maji yanayohifadhiwa ndani ya bwawa hilo hayawezi kuwa na madhara kwa Jamii, pia naibu Waziri huyo alitembelea  kituo cha udhibiti taka, Uwanda wa kuvuna maji ya mvua mgodini hapo pamoja na karakana ya mgodi huo.

“Bwawa hili kama unavyoliona usanifu wake, umezingatia tahadhari zote kuhakikisha hakuna maji yoyote yanatoka nje na hasa ukizingatia maji yanayopatikana hapa ni yenye mchanganyiko wa madawa yanayotumika kuchenjua dhahabu” Alisema Meneja wa Kituo cha Uchenjuaji dhahabu bwana Festo Shayo, wakati alipokuwa akitoa maelezo juu bwawa hilo.
Kwa upande wake naibu Waziri Mpina amesema licha ya kufanya ziara katika Migodi mingi bwawa la kuhifadhia maji yanayotoka katika kinu cha kuchenjulia dhahabu la Buzwagi ni la kiwango cha juu na ameitaka Migodi mingine pia kutembelea kwa lengo la kujifunza usanifu wake.
“Ni seme tumepita maeneo mengi ila hapa mmejitahidi kuhakikisha wananchi wanaowazunguka wako salama, nafikiri kuna haja ya migodi mingine kuja kujifunza hapa, karakana yenu pia ni nzuri na inazingatia utunzaji wa mazingira. Alisema mh Mpina.
Aidha akiwa katika kituo maalumu cha udhibiti taka Mgodini hapo Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi kujenga paa kwenye eneo la udhibiti wa taka za vyuma ili kuzuia maji ya mvua kugusa taka hizo.

“Mmejitahidi kuhakikisha taka zinawekwa katika utaratibu mzuri, ila kukosekana kwa paa hapa ni tatizo, hivyo nawaagiza ndani ya siku therathini eneo hili liwe na paa” alisema Naibu Waziri Mpina.

Awali akiukaribisha ugeni wa naibu Waziri huyo Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo alimueleza naibu Waziri huyo kuwa sekta ya madini kwa sasa duniani imekumbwa na changamoto ya kuporomoka kwa bei ya dhahabu, hali ambayo imepelekea wawekezaji wengi kujikuta wakijiendesha kwa hasara.

“Mheshimiwa naibu Waziri, Mgodi wa Buzwagi toka uanze shughuli zake umekuwa ukishirikiana na Jamii katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo na tunaendelea kufanya hivyo, Hata hivyo changamoto ni kubwa kwani kila siku bei ya dhahabu inashuka na hii inatufanya tushindwe kujiendesha kwa faida”alisema Mwaipopo.

“Tumeanza mchakato wa maandalizi ya kusitisha shughuli za uchimbali maana gharama zinazidi kuwa kubwa hata hivyo kama bei ya soko itabadilika tutafikiria vinginevyo” aliongeza Mwaipopo.

Akizungumzia hatua ya mgodi huo kutaka kusitisha shughuli za uchimbaji naibu Waziri Waziri ofisi ya makamu wa rais anaeshughulikia mazingira na muungano Luaga Mpina, amewaomba wawekezaji hao kuangalia namna ingine itakayowawezesha kuchimba kwa gharama ndogo inayoendana na bei ya dhahabu.

“kwa kweli serikali inawahitaji sana wawekezaji na tunaposikia mnaondoka kwetu sisi ni hasara kwa sababu kodi mbalimbali ambazo mmekuwa mkilipa kwa halmashauri ya mji wa Kahama hazitakuwepo tena na hii itafanya miradi mingi ya Maendeleo isitekelezeke baada ya ninyi kuondoka, tunawaombea bei ya dhahabu ipande ili muendelee kuwepo” Alisema Mpina.

Ziara hiyo ya kushitukiza ili lenga kujionea namna ambavyo mgodi wa Buzwagi unazingatia maelekezo mbalimbali ya wataalamu wa wizara yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.