Habari za Punde

Mikarafuu yaungua bonde la Mkanyageni, Pemba

Na Masanja Mabula –Pemba 

Zaidi ya mikarafuu 151 umeungua  katika tukio la moto lililotokea Janauri 22 mwaka huu katika bonde la Mkanyageni Shehia ya Mzambarauni Wilaya ya Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba .

Jumla ya eka tisa  (9)  za mashamba ya mikarafuu yameathiriwa  zimehujumiwa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha hasara kuwa kwa wamiliki ya mashamba hayo .

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa  Wilaya ya Wete  Rashid Khadidi Rashid amevitaka vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika wa kitendo hicho .

Amesema kuwa kitendo cha kuchoma moto mashamba hayo ni kuhujumu uchumi wa nchi pamoja na wananchi wake na kwamba serikali itahakikisha wanahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani .

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho ambacho kinarudisha nyuma juhudi za serikali za kuliimarisha zao la karafuu ambalo ndio uti wa mgogo wa uchumi wa Nchi.

“Serikali haiwezi kuvifumbia macho vitendo vya kuhujumu uchumi wake , hivyo naviomba vyombo vya sheria kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika waweze kupatikana na kufikishwa mahakamani ”alisisitiza.

Aidha amefahamisha kwamba kuchomwa moto mashamba hayo ni hujuma za makusudi zilizofanyika  , kwani moto huo umetokea katika  maeneo na mashamba tofauti .

“Ukiangalia jinsi moto ulivyotokea utabaini kwamba kuna hujuma  za makusudi , moto umetokea katika sehemu na maeneo tofauti , kitend hichi ni kudhoofisha maendeleo ya nchi  na wananchi wake ”alifahamisha.

Mmoja wa wananchi wakaazi wa shehia hiyo  Hamad Bakari Makame  akizungumza na mwandishi  wa habari hizi amesema kwamba kitendo hicho kimesababisha athari kubwa ya kiuchumi na kimazingira .

Alifahamisha kwamba kutokana na bei za sasa ya zao la karafuu mkarafuu mmoja unauwezo wa kuzalisha zaidi ya pishi ishirini sawa na zaidi ya shilingi laki nne , na kuna zaidi ya mikarafuu 151 iliyoungua moto .

“Ni hasara kubwa za kiuchumi na kimazingira , kwa kweli hali ya umaskini kwa waliokuwa wakimiliki mikarafuu hii wimbi la umaskini linawanyemelea , tunataka uchunguzi ufanyike ”aliomba .

Aidha amefahamisha kwamba katika Shamba la Mohammed Abdalla Chande mikaraafu hamsini na nane (58) imeungua wakati katika shamba la Mani Abdalla Chande (70) imeungua na mikaraafu 23 imeungua katika shamba la Serikali .
mwisho

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.