Habari za Punde

Balozi Seif Aongoza Kikao cha Kamati ya Maafa Zanzibar.

Kikao cha kwanza cha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chakutana chini ya mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif akikiongoza Kikao cha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar akisaidiwa na Makamu Mwenyekiti wake kulia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad  aliyesimama akitoa Muhtasari wa Sheria ya Kamisheni hiyo kwenye Kikao cha kwanza Wajumbe wa Kamaisheni hiyo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Nd. Moh’d  Khamis Ngwali akitoa ufafanuzi wa muelekeo wa mvuza zinazonyesha  za mwezi januari na febuari 2016 kwenye kikao cha kwanza cha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Kikao cha kwanza cha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kimeanza rasmi ambapo Wajumbe  wa Kamisheni hiyo wamekutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Kufutwa  kwa Sheria nambari 2 ya mwaka 2003 na kuanzishwa kwa sheria nambari 1 ya mwaka 2015 ya kukabiliana na maafa Zanzibar ndio iliyotoa mamlaka kwa kamisheni hiyo kutekela majukumu yake hapa Nchini.

Akiwasilisha Muhtasari wa sheria ya kukabiliana na maafa Zanzibar kwenye Kikao hicho, Mkurugenzi  Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema mabadiliko ya sheria hiyo yamekuja kutokana na mapunugu kadhaa yaliyokuwa yakikwamisha utekelezaji wa shughuli za kujikinga na kukabiliana na maafa hapa Zanzibar.

Nd. Juma alisema kukosekana kwa muundo wa usimamizi, mfumo madhubuti wa utoaji wa Taarifa, ushiriki wa sekta binafsi pamoja na mbinu za kujiandaa, kujikinga na kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa ni  baadhi ya masuala  yaliyokuwa yakileta usumbufu katika kipindi kilichopita nyuma.

Alisema kwa mujibu wa sheria nambari 1 ya mwaka 2015, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa itakuwa ni chombo cha juu kitakachotoa maamuzi yanayohusu masuala ya kukabiliana na maafa Zanzibar.

Alifahamisha kwamba  katika kukabiliana na maafa , kifungu cha 6 cha sheria hiyo kinaipa uwezo Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kumshtaki mtu ye yote ambae atakataa kutoa au kupokea huduma wakati wa dharura au maafa.

“ Kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika, kufanya ukaguzi kwa mtu ye yote, jengo, eneo au chombo kwa lengo la kukinga, kupunguza na kukabiliana na maafa na hali za dharura ”. Alisisitiza Nd. Juma.

Akitoa ufafanuzi wa Taarifa ya muelekeo wa Mvua mkubwa kwa mwezi wa Januari na Febuari  mwaka  2016  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya  Zanzibar  Nd. Moh’d  Khamis Ngwali alisema changamoto za mvua zinazonyesha ni kiashirio kinachoweza kusababisha Mvua za Alninyo.

Nd. Ngwali alisema kwa mujibu wa miongo ya mvua miezi ya Januari na Febuari ni misimu ya vimbunga ambavyo vinaweza kuleta athari wakati wowote na mamlaka hulazimika kutoa tahadhari  pale mvua inapoendelea kunyesha wakati ikipindukia zaidi ya milimita arubaini.

Alisema  baadhi ya wakati mvua zinazoripotiwa kunyesha hapa Zanzibar  hufikia hadi milimita 83.5 kiwango kinachosababisha kutokea mafuriko na hatimae kuleta maafa hasa katika maeneo ya mabonde.

Naye Waziri wa Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee  alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaandaa mfuko maalum wa Miundo mbinu        { Infrustructure Fund } ambao huchangiwa  na Kila Mgeni anayeingia Nchini  kwa Dola Moja ya Kimarekani.

Mh. Omar alisema matarajio ya makusanyo ya mkufo huo imekadiriwa kufikia shilingi Bilioni 25 ambapo asilimia 25% ya makusanyo hayo yamelengwa kwa Mifuko saba  iliyosajiliwa akatolea mfano kama ile ya Maafa pamoja na  ukimwi.

Wakichangia katika Mkutano huo  baadhi ya wajumbe wa Kikao walisema bado ipo haja ya kuandaliwa njia mbadala kwa watu wanaoishi katika maeneo hatarishi itakayokuwa ya kudumu katika kudhibiti maafa wakati yanapotokea.

Walisema mipango ya muda mrefu na mfupi inahitajika kufanywa licha ya juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali Kuu katika uchimbaji wa mitaro katika baadhi ya maeneo  kwa kudhibiti maji yanayotuwama pamoja na wale  waathirika kuhifadhiwa kwenye majengo ya Skuli.

Kuhusu Kikosi cha Zima moto na Uokozi  Zanzibar  Wajumbe hao waliiomba Serikali Kuu kwa kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa kukijengea uwezo zaidi wa Vifaa Kikosi hicho ili kiwe na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Walisema yapo mapungufu mengi ya ufinyu wa vifaa vinavyoweza kukisaidia kikosi hicho katika kukabiliana na maafa hasa yale ya moto kwenye baadhi ya maeneo kama  Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Umoja wa Mataifa tayari umeshatoa onyo la kuziasa Nchi wanachama kuwa tayari kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi wakati wowote yanapotokea.

Balozi Seif alisema  utafiti wa Wataalamu wa Umoja huo umethibitisha na kutoa tahadhari kwamba zipo nchi nchi zenye uwezekano wa kukumbwa na vimbunga ikiwemo Tanzania kutokana na mabadiliko makubwa ya mzunguuko wa hali ya hewa Duniani.

Kikao hicho cha kwanza cha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kilijumuisha wajumbe  mbali mbali wakiwemo Mawaziri, wakuu wa Mikoa na Vikosi vya ulinzi pamoja na watendaji wa taasisi zinazohusiana na maafa hapa Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.