STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 10.2.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka watumiaji wote wa mitandao ya kijamii na wale
wenye dhamana ya kusimamia na kufanya
tahariri wawe makini zaidi ili kulinda hali ya amani ya nchi na kujiepusha na
matatizo yanayoweza kuwakumba kwa uvunjaji wa sheria.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika
maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar zilizofanyika katika viwanja vya
Victoria Garden, Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman
na wengineo.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema
kuwa inasikitisha kuona kwamba baadhi ya viongozi na wahariri wa mitandao hiyo
wanaishi hapa Zanzibar na wanausahau utu wao pamoja na utu wa wenzao kwani
heshima ya wananchi wa Zanzibar inayoambatana na utamaduni na desturi zao
zinajulikana vizuri sana.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, ina imani kwamba kuwepo kwa mitandao ya kijamii
iliyobora na inayotumainiwa na kuongozwa kwa kuzingatia sheria ni jambo la
lazima kwa maendeleo na kuimarisha uhuru wa wananchi wa kutoa maoni kama
ilivyoelezwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika Ibara ya 18.
Dk. Shein alisema Serikali inaendelea
kuhakikisha kuwa uhuru wa wananchi wa kuwa na maoni yao pamoja na uwezo na
kutafuta na kutoa taarifa unatumiwa vizuri na kwa kuzingatia sheria, ili
kulinda haki za wananchi na maslahi ya nchi.
“Kwa upande mwengine, ni wajibu wa kila
mwananchi kuelewa kwamba Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inatulinda na inatuhakikishia
kuwa katika utumiaji wa taarifa na utoaji wa maoni, utu wa mtu unaheshimika na
hakuna aliye na haki kisheria ya kuweza kumdhalilisha mwenzake”,alisema Dk.
Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Sheria ya
Mitandao ya mwaka 2015, iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, inazidi kulinda heshima, hifadhi na faragha za wananchi katika suala
zima la mawasiliano kupitia mitandao na simu kama ilivyokusudiwa na sheria
hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa ipo baadhi ya
mitandao ya kijamii ambayo inatumiwa kurusha habari za uchoshezi na habari za
uongo dhidi ya Serikali ambapo baadhi ya wakati mitandao hiyo inaruhusu
wanachama kutumia taarifa huku wakificha majina yao.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema
kuwa ni wazi kwamba kauli mbiu ya mwa ka huu isemayo ‘ Matumizi Mabaya ya
Mitandao ya Kijamii Yanaweza kuwa Chanzo cha Uvunjaji wa Sheria na Amani ya
Nchi” imekuja wakati mzuri ambapo matumizi ya simu na mitandao yameongezeka na
kukua kwa kiasi kikubwa hapa Zanzibar.
Alisema kuwa hivi sasa mwananchi wa Zanzibar, takriban popote alipo katika
kisiwa cha Unguja na Pemba anaweza kupata huduma za inteneti na kujiunga na
mitandao ya kijamii yote muhimu duniani kwa haraka na wepesi kwa kupitia
mashirik mbali mbali ya simu yaliopo Zanzibar.
“Mitandao yote hii sasa imekuwa ni nyenzo
muhimu ya kurahisisha utoaji wa huduma na ya kupeana taarifa mbali mbali
zikiwemo zile zinazoitwa ‘dripu’...ni taarifa zinazotolewa kwa lengo la kutiana
moyo juu ya jambo fulani japo kuwa taarifa hizo baadhi ya wakati huwa hazina
ukweli wala mantiki yoyote”,alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kuwa faida
zinazopatikana kwa kuwepo na kuimarika kwa huduma za intaneti, mitandao ya
kijamii na huduma za simu zimegusa sekta zote za kiuchumi na kijamii kwani
teknolojia ya habari imerahisisha sana maisha na kufungua fursa nyingi ambazo
zinahitaji kulindwa kwa sehria ili faida zinazopatikana ziwe endelevu.
Hata hivyo Dk. Shein alieleza kuwa iko
haja kuanza kufikiria namna bora itakayowezesha kutumia simu na mitandao wakati
wa kazi bila ya kuathiri utekelezaji wa majukumu, hasa katika taasisi zinazotoa
huduma kwa wananchi.
Pia, alisisitiza umakini katika kuhakikisha
kuwa matumizi ya simu makazini hayaathiri utekelezaji wa majukumu yaliopangwa.
Wakati huo huo, Dk. Shein ameeleza azma
ya Serikali katika bajeti ijayo ya kujenga jengo jipya la Mahakama Kuu huko
Tunguu pamoja na kupokea ombi la kuongezwa kwa Majaji na kusisitiza kuwa
Serikali itatekeleza wajibu wake.
Aidha, ameueleza uongozi wa Mahakama kuu
kuwa fedha zilizoombombwa hivi karibuni Tsh, milioni 30 kwa ajili ya kumalizia
jengo la Mahakama ya Watoto huko Mahonda atawapa kwa lengo la kumazizia ujenzi
huo pamoja na kulengwa vizuri Bajeti yao ya mwaka huu wa fedha. Pia, Dk. Shein
alizindua kitabu cha mwaka cha Sheria.
Mapema Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman
Makungu alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wamesogeza karibu zaidi
huduma za kimahkama kwa wananchi baada ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Mwanzo
Kitulia Wete Pemba pamoja na kuanzishwa
kwa Mahakama ya Biashara.
Jaji Makungu alisema kuwa duniani kote
watu wanawasiliana kwa njia ya mtandao ambao umerahisisha mawasiliano yakiwemo
ya kibiashara, kiuchumi, kielimu na kihabari.
Aliongeza kuwa simu za mkononi zimekuwa
ni kero shuleni, kazini, nyumbani na hata katika nyumba za ibada ambapo baadhi
ya ndoa zimevunjika kutokana na meseji mbaya zilizoonekana katika simu ya mmoja
wa wanandoa.
Pia, katika nchi zinazoendelea intaneti
imekuwa ni kero, imeathiri maendeleo mazuri ya wanafunzi kimasomo na pia,
imeathiri maendeleo mazuri ya wanafunzi kimasomo na pia, imeathiri maisha ya
vijana, watoto na hata watu wazima
kutokana na kuangalia picha chafu na kutumia muda mwingi kuchati na marafiki.
Hata hivyo Jaji Makungu alisema kuwa
mtandao umekuwa na changamoto kubwa kwa Tume za Uchaguzi duniani, ikiwemo zile
za Tanzania na Zanzibar ambapo matokeo ya uchaguzi yamerushwa kwenye mitandao
kabla ya kutangwaza na Tume husika.
Nae Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Said Hassan Said
alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa faida
katika matumizi sahihi ya mitandao pia, kumekuwepo na changamoto kubwa ya
matumizi mabaya ya mitandao katika jamii.
Ili kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao
Mwanasheria Mkuu alitoa wito wa kuheshimu Katiba na Sheria za nchi katika
matumizi ya mitandao ya kijamii, kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi zaidi
katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuongeza uwezo wa kitaaluma
waataalamu wa kiusalama katika usimamizi wa matumizi ya mitandao, kupiga vita
hali hiyo na kutoa mashirikiano kwa vyombo vinavyosimamia sheria ili kuthibiti
hali hiyo.
Viongozi mbali mbali walihudhiiria hafla
hiyo akiwemo pia, Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Shaaban Ali Lila, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Mhe. Jaji Damian Lubuva, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi
Ali Abdalla, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Mhe. Mwinyihaji
Makame Mwadini, Mkurugenzi wa Mshtaka, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mahakimu, Makadhi na viongozi wa dini pamoja na wananchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment